Tuesday, May 28, 2024

TAKUKURU SONGWE YAMSHITAKI MAHAKAMANI OFISA MTENDAJI WA KATA YA CHILULUMO.


Na Ahmad Mmow.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Songwe imemfikisha mahakamani na kumfungulia mashitaka ofisa mtendaji kata wa kata ya Chilulumo, Abunasa Abass Kiobya.

23.05.2024 mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Momba, Mheshimiwa Magreth Kanonyole. Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU mkoa wa Songwe, Simona Mapunda akimsomea Kiobya shitaka hilo namba 13783 la mwaka 2024(13783/2024) alisema mshitakiwa huyo kati ya tarehe 02.05.2018 na 22.11.2019 akiwa na nia ovu alitumia madaraka yake vibaya kinyume cha kifungu cha 31 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(PCCA) sura ya 329 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 kwa kushindwa kupeleka fedha kwa mhasibu wa halmashauri ya wilaya ya Momba kiasi cha shilingi 13,738,600.

Alisema kitendo hicho cha kutopeleka fedha kwa muhasibu wa halmashauri ya wilaya ya Momba ni kinyume cha agizo namba 37(2) na 50(5) la randama ya fedha za serikali za mitaa ya mwaka 2009.

" Pia mshitakiwa anashitakiwa kwa kosa la ufujaji na ubadhirifu. Vitendo ambavyo ni kinyume cha kifungu cha 28(1) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(PCCA) sura ya 329 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022. Kwani mshitakiwa alifanya ubadhirifu wa shilingi 13,738,600 mali ya halmashauri ya wilaya ya Momba zilizofika kwenye himaya yake akiwa ni mtumishi wa umma," alisema Mapunda.

Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa hoja za awali tarehe 12.06.2024. Ambapo Kiobya amekana mashitaka yote na yupo nje kwa dhamana baada ya kutekeleza kikamilifu masharti ya dhamana.

No comments: