Kiongozi wa kikundi cha makachu cha Furaha Beach Ndugu Nassor Abubakar amesema wameamua kujikusanya pamoja na kuanzisha kikundi hicho wakiwa na lengo la kukitangaza kisiwa cha Pemba kiutalii pamoja na kuepuka kujiingiza katika makundi yasiyofaa kwa kutokuwa na kazi ya kujishuhisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali itaendelea kuunga Mkono juhudi zinazofanywa na wawekezaji kwa kuhakikisha inawawekea mazingira bora ya uwekezaji ili kutimiza malengo waliyokusudia.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wamiliki pamoja na wananchi waliofika katika eneo la Furaha Beach linalomilikiwa na Zanzibar Milele Foundation lililopo Furaha wilaya ya chake Chake Pemba.
Amesema Zanzibar Milele Foundation imekuwa msatri wa mbele katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuisaidia katika mambo mbali mbali ya kiuchumi na kijamii kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais ameziagiza Wizara mbali mbali zinazohusika na baadhi ya changamoto zilizopo eneo hilo la uwekezaji kuhakikisha wanazichukulia hatua za haraka changamoto hizo zikiwemo kufikishwa kwa umeme wa Three Phase, kupimwa na kupatiwa hati ya uhaulisho wa eneo hilo, kuwekwa kifusi barabara iliyopita maeneo hayo pamoja na kufikishwa huduma ya maji safi na salama ili kuweza kuleta ufanisi nzuri wa kazi zao.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewahakikishia vijana wanaopiga makachu katika eneo la Furaha Beach kuwa Serikali itaangalia namna bora ya kuwasaidia hasa katika suala la kupatiwa ujuzi zaidi ili kuweza kufanya kazi hio kwa uweledi na umakini zaidi pamoja na kuitangaza Pemba kiutalii.
Nae Meneja wa Zanzibar Milele Foundation kanda ya Pemba Ndugu ABDALLA SAID ABDALLA amesema lengo la kujengwa kwa Furaha Beach ni kuunga mkono kauli ya Rais Dkt Mwinyi ya kuifungua Pemba kiuchumi kupitia uwekezeji sambamba na kuwapatia wananchi wa furaha na maeneo jirani sehemu ya kupumzikia mara baada ya harakati za kazi za Ujenzi wa Taifa.
Amesema utakapokamilika ujenzi wa eneo la Furaha Beach litatoa fursa kwa wakaazi wa Furaha na maeneo mengine kuweza kufanya biashara zao na kuweza kujiajiri kupitia eneo hilo jambo linalounga mkono adhma ya Rais Dkt Mwinyi ya kuwapatia ajira Laki 3 wananchi wa Zanzibar.
Ndugu Abdulla amesema kuwa changamoto kubwa inayoikabili Zanzibar Milele Foundation katika ujenzi wa Furaha Beach ni kuchelewa kufanyika upimaji na uhaulishaji wa eneo hilo jambo ambalo linakwamisha umalizikaji wa ujenzi huo utakaonufaisha wakaazi wengi wa kisiwani Pemba.
Kwa upande wake kiongozi wa kikundi cha makachu cha Furaha Beach Ndugu NASSOR ABUBAKAR amesema wameamua kujikusanya pamoja na kuanzisha kikundi hicho wakiwa na lengo la kukitangaza kisiwa cha Pemba kiutalii pamoja na kuepuka kujiingiza katika makundi yasiyofaa kwa kutokuwa na kazi ya kujishuhisha.
Amesema mwamko wa upigaji wa makachu kisiwani Pemba unazidi kuwa mkubwa jambo linalopelekea uhitaji wa eneo na vifaa kuongezeka ukilinganisha na awali kilipoanzishwa kikundi hicho.
Aidha NASSOR amesema kikundi chao kimekuwa kikabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo uhaba wa vifaa vya kufanyia mazoezi, vifaa vya usaidizi hasa pale mwenzao anapopatwa na tatizo hivyo wameiomba Serikali kuweza kuwatatulia chanagamoto zinazowakabili ili kuweza kufanya kazi hio kwa ufasaha mkubwa na kuendelea kuitangaza Pemba kupitia mchezo huo.
Imetolewaa na Kitengo cha Habari ( OMPR )
No comments:
Post a Comment