ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 17, 2010

BONGO KUNA MAMBO!


MWANAMKE ambaye jina lake halikufahamika mara moja, amedaiwa kupotea kimiujizi kwenye gari lake baada ya kumsaidia ombaomba.

Baadaye mwanamke huyo anadaiwa kukutwa jana asubuhi ufukweni mwa Bahari ya Hindi akiwa uchi wa mnyama na hawezi kuzungumza.

Askari wa Usalama barabarani waliozungumza na gazeti hili walithibitisha kuwepo kwa tukio hilo wakisema mwanamke huyo alikuwa akiendesha gari aina ya Rav4 akitokea mjini kuelekea Kinondoni.

Walifahamisha kuwa lilipofika kwenye taa za kuongozea magari katika makuano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Umoja wa Mataifa, alisimama na hakuondoka licha ya kuruhusiwa.

Walidai kuwa trafiki aliyekuwa akiongoza magari alimfuata mwanamke huyo na kumuuliza kuna matatizo gani, mwanamke huyo akaonyesha mkono wake uliokuwa umejaa nywele na kusema amepata shida hiyo mara baada ya kumpa fedha ombaomba aliyekuwa karibu na gari hilo.

Kwa mujibu wa habari hizo mwanamke huyo alipotea baada ya ombaomba huyo kumweleza kuwa kama anataka kurudi katika hali yake ya kawaida ambusu na akabubali, lakini mara baada ya kufanya hivyo wakatoweka wote.

Habari hizo zimeeleza kuwa kabla ya kutoweka kimiujiza, ombaomba huyo wa kiume alimfuata mwanamke huyo aliyekuwa akisubiri kuruhusiwa kupita kwenye taa kuongoza magari kwenye makutano hayo na kuomba msaada wa fedha.


Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema, mwanamke huyo alimpa Sh500 na mara baada ya ombaomba kupokea, mkono wake (mwanamke) ukaanza kuota nywele nyingi.

Kitendo hicho kilimfanya mwanamke huyo kushindwa kuondoa gari lake baada ya kuruhusiwa na askari aliyekuwa akiongoza magari eneo hilo.

“Baada ya askari huyo kuona gari hilo limeendelea kusimama
katikati ya barabara, alilisogelea na kumkuta mwanamke huyo akiwa ameduwaa kwenye usukani," alisema shuhuda mmoja wa tukio hilo na kuongeza:

“Ndipo trafiki alipomuuliza umepatwa na tatizo gani na mwanamke huyo akasema, baada ya kumpa huyu kaka (ombaomba) Sh500, mkono wangu umekuwa hivi”.

Taarifa zimeeleza kuwa
baada ya mwanamke huyo kutoa kauli hiyo, ombaomba huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa amesimama pembeni mwa gari, alimtaka ashuke kwenye gari na kumbusu kama anataka kuondokana na nywele hizo.

“Kusikia hivyo, trafiki alimwomba mwanamke huyo ashuke na afanye kama alivyoelezwa lakini, alipombusu tu, wote wawili wakapotea,” shuhuda huyo alisema.

Imeelezwa kuwa baada ya tukio hilo askari huyo alitimua mbio kuelekea kituo cha polisi cha Selander Bridge kuomba msaada.

Hata hivyo ingawa polisi wa kituo hicho walifika eneo hilo hawakuliondoa gari hilo kwa kuogopa kuingia ndani.

Kutokana na woga waliokuwa nao askari, gari hilo lilikaa hadi jioni na lilizimwa na mmoja wa ndugu zake mwanamke huyo, waliofika katika eneo hilo majira ya saa 12 jioni.

Habari zilisema baada ya ndugu zake kufika walikubaliana kwenda Kanisani na Msikitini kwa ajili ya kuomba na leo asubuhi mwanamke huyo alikuwa ufukweni akiwa uchi.

Hata hivyo Kamanda wa polisi mkoa wa Ilala, Faustine Shirogile alikanusha kuwepo kwa tukio hilo na kusema ni la uvumi.

“Hadi muda huu ninapoongea na wewe hakuna mtu yeyote aliyeripoti polisi kuhusu tukio hilo. Huo ni uvumi na tayari umekwisha enea sehemu mbalimbali hata katika tovuti na internet pia,” alisema Shirogile.

No comments: