HOTUBA YA 1 YA M/KITI BAADA YA UCHAGUZI MKUU WA 10/17/09
Awali ya yote napenda kumshukuru M/Mungu kwa kutujaalia kukutana hapa na kufanikisha yale yote tuliyoyakusudia.
Siku ya leo vilevile ni siku muhimu sana kwa familia yangu,kwani ni siku ambayo tulipata mtoto wetu wa kwanza na hii leo Wa’el anatimiza miaka saba. Happy Birthday Wa’el and many more to come, inshallah.
Kwa wale ambao, waliitikia mwito tokea awali. Kwa wale ambao walishiriki baada ya kujenga imani juu ya mwito. Kwa wale ambao hawakuitikia lakini waliheshimu maamuzi ya ndugu zao walioitikia. Kwa wale ambao walisimama kidete kwa kuulinda mwito huo. Kwa marafiki wa Watanzania na wangependa kuona mafanikio yao. Na kwa ninyi nyote mliohudhuri hapa
Napenda kusema ushindi huu wa leo ni ushindi wenu na ninyi ndio mnaostahiki pongezi.
Mafanikio ya kufikia uchaguzi wa leo ni matumaini ya kudumisha Umoja na kuboresha malengo ya jamii yetu. Matokeo ya uchaguzi ni dalili ya muongozo bora na wenye dira. Kwa mara nyingine tena, Watanzania wameweza kudhihirisha kuwa wanaouwezo wa kuingiza ndoto zao kwenye nadharia na kuwa shauku kubwa kwa jamii ya Watanzania North Carolina.
Najua wapo katika jamii ambao bado hawajaridhika na hali halisi, na kupata majibu ya maswali yao.Najua bado wapo katika jamii ambao hawajaona umuhimu wa kuwepo kwa Jumuiya.
Jumuiya hii ni yenu na imekusudia kuwafaidisha Watanzania bila kujali maeneo wala umaarufu. Mawazo ya wote yana nafasi sawa na ninyi ndio waamuzi wa muelekeo wa Jumuiya hii.Tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuwapa majibu sahihi na kuwajengea umuhimu wa kujiunga katika UTNC. Na ni imani yangu na nyinyi mtakuwa wa wazi na wa kweli ili tushirikiane kwa pamoja katika kuijenga jamii yetu iliyobora.
Napenda kutoa shukurani kwa familia yangu kwa moyo wao mkunjufu wa kukubali kubeba kadhia za jamii, bila shaka yote kwa upande wangu yangekuwa ni hadithi na ndoto kama si hiyari na ustahamilivu wenu. Hii ni kutokana na kuelewa umuhimu wa jamii bora na kuiamini ari yangu. M/Mungu aendelee kuwapa moyo wa ustahamilivu na upendo.
UTNC imeweza kukuza njia za mawasiliano na kuwa mstari wa mbele katika mambo ya kijamii. kuanzia ya dharura mpaka ya furaha.
Muheshimiwa M/Kiti wa zamani,Wajumbe wa bodi wa zamani,napenda kuwapa pongezi kwa uongozi wenu na kazi nzuri ya kujitolea mlioifanya katika jamii yetu. Bila shaka Wanajumuiya wanatambua na kuheshimu mchango wenu. Ni matumani yangu mtaendelea kwa karibu na huru kushiriki kulisukuma gurudumu hili kwa pamoja. Nawakaribisha katika kuendelea kushiriki katika uongozi wangu huu.
Wanajumuiya na wageni waalikwa, ahsanteni sana kwa ushirikiano wenu, na zaidi kwa maamuzi bora mliyoyafanya leo. Naamini maamuzi haya msingeyafanya kama msingekuwa na imani na mimi. Mlikuwa na uwezo wa kuamua vinginevyo, lakini mkaona kuwa mimi ndiye yule mnayemtarajia.
Kuna ngudu zetu ambao walipatwa na misiba,napenda kutumia nafasi kuwatambua na kuwapa pole.Napenda mjue kuwa UTNC ipo pamoja nanyi siku zote. Haito watupa wala kuwaacha nyuma. M/Mungu awaweka ndugu zetu waliotutangulia mahala pema. Na awape nguvu katika kuishinda mitihani hii na mingine.
Vilevile napenda kuwapongeza Wazazi kwa wageni waliowapata.Hongereni kwa zawadi adhwimu za watoto wapya.Pongezi hizi vilevile ziwafikie Mababu na Mabibi kwa vikuu hivyo, Aunty yangu Rahma na Uncle Amour nao wamebahatika na mjukuu wa wao wa kwanzo. M/Mungu awawekee, awajaalie wawe watoto bora na wenye manufaa katika jamii
Napenda kuwatambua na kuwapongeza ndugu zetu waliofanya maamuzi muhimu katika maisha yao ya kufunga mkataba wa maisha na wapenzi wao ya ndoa. Nawatakieni maisha marefu na mazuri.
Napenda kutumia nafasi hii kuwatambua na kuwapongeza wenzetu ambao walikuwa katika nguzo muhimu ya maisha yao na zaidi ni kwa nchi yetu changa ya Tanzania,na si nguzo nyingine isipokuwa ya kuhitimu masomo. Na vilevile napenda kuwapongeza wale ambao wapo katika harakati ya kuelekea katika njia hii tukufu.
Lengo la Elimu sio tu kuzidisha daraja lako la kiuchumi, hali halisi ya leo inadhihirisha hilo. Elimu inakuza daraja muhimu la ustaarabu, tafakuri na muono bora katika kuyaendea mambo. Kundi la watu wenye Elimu ni muhimu sana na ni nguzo kwa jamii. Jamii inapokosa kufaidika na Elimu ya Mwanajamii tu kwa sababu Elimu yake imekuwa biashara. Jamii inapokosa kufaidika na Elimu ya mwanajamii tu kwa sababu elimu yake inamfanya awe na mtazamo wa kimaisha usowiana na jamii. Kwa hakika huo ni ufukara wa hali ya juu na mwana Elimu huyo hubaki kuwa ni tatizo na kadhia ya jamii yake.
Wazee wanapokosa kulinda mila na desturi zinazouliwa kwa maendeleo ya kiuchumi na Technologia.Wazee wanapoigawa jamii kwa kuchagua kundi lipi ni bora na lipi si bora. Wazee wanapokosa ahlaki za kijamii na kuvamia ujana.Vijana wapokosa kujitolea katika jamii yao na kutumia nguvu zao kwenye mambo yasiyo na lazima wala haraka. Vijana wanapokosa kutambua umuhimu wa mchango wao na kuendelea kudharau kila kitu. Kina mama wanapokosa kuwa walezi wa jamii. Viongozi wanapoigeuza kuwa kazi ya kujitolea ni kazi ya hiyari na kutoelewa umuhimu wa kutimiza ahadi wanazoziahidi au kuona wao ndio Jumuiya .
Jamii inakosa muelekeo na kubaki katika kiza cha makhasiriko makubwa. Na sio Wanajamii tu wanaopoteza nafasi muhimu ya maendeleo, Na ndugu zetu wa Tanzania ambao mahitaji yao yanakamilika kutokana na mafanikio yetu. wanakosa bahati ya kufaidika kwa kuwepo kwetu sisi huku na wanabaki kutapatapa na kuendelea na ukata wa maisha.
Tukiendelea kutoshinikiza nguvu za makusudi za msukumo wa maendeleo katika mambo muhimu na yenye haraka. kuna uwezekano ya mabadiliko kutokuja kabisa au kuchelewa kuja. Inawezekana tunaishi bila ya kuzingatia nafasi zetu katika jamii kuwa ni muhimu sana na nyeti katika maendeleo ya jamii. Jambo ambalo mabadiliko yake hayaji bila kila mmoja wetu kukata shauri kwa kuleta msukumo huo.
Wadogo zetu na watoto, mila na desturi za wazazi wenu ndio nguzo za ushirikiano na upendo mnaouona katika jamii yenu.Msizitupe,jitahidini kuziiga mtafanikiwa katika kuishi na watu vizuri na kuwa raia wema.Kuna mengi mazuri yaliyo nje ya mila na desturi zenu,na mengi mabaya. Mkizidisha mapenzi kwa wazazi wenu na kuwa wa wazi kwao,watawasaidia kuchagua katika hayo ili muendelee kuwa mifano bora.
Kufanikiwa kwa Jumuiya hii ni kufanikiwa kwa Mtanzania mkazi wa North Carolina kiuchumi, kiafya, Kielimu, Kijamii na Kitamaduni
Wazee wetu wanasema;”Elimu ya mmoja ni ujinga,na utajiri wa mmoja ni ufukara” Mtu mmoja hatoshi kuleta maendeleo,lazima jamii ishirikiane, lazima kila mmoja aone umuhimu wa kuchangia kihali na mali katika maendeleo,ndipo yatakapo kuja. Tumekuwa ni wenye kuhoji Chama kitatufanyia nini?,Chama hakiwezi kukufanyia chochote ikiwa ujakijenga kufikia hali hiyo.Hiki chama ni cha Watanzania wa North Carolina,hakuna mwingine yeyote atakaye kijenga,isipokuwa wewe Mtanzania NC.
Tupo katika kurasa muhimu sana katika historia ya Tanzania.Sisi ni kizazi ambacho ima kimeshuhudia uhuru wa Tanzania au tunaishi na walio shiriki kuleta uhuru Watanzania. Ukitaka kuliona hili katika miaka yetu hiyo ya mtondogoo.Rejea historia ya The founding fathers wa taifa la kimarekani.
Inawezekana si kosa lako Tanzania kuwa na asilimia 60 ya masikini wa kutupwa, inawezekana si kosa lako Tanzania kutokuwa na umeme wala maji,inawezekana si kosa lako Tanzania kuwa na mapapa penguzi. Inawezekana kuwa si kosa lako Tanzania mpaka leo watu wengi wanakufa kwa Maleria. Lakini kumbuka makosa haya waliyafanya wazazi wetu kutoshiriki vilivyo katika kuijenga nchi yao .Jambo ambalo linahatari ya sisi kulirudia kosa hilo hilo. Na sisi leo tusiposimama na kuamua kutosubiri kesho. Elewa matatizo haya yataendelea na hali ya nchi yetu itaendelea kuwa mbaya zaidi na zaidi.
Mimi naamini niya tunazo na uwezo tunao, naomba ushirikiano wenu ya kufuta historia ya kuamini magumu na makubwa yatasubiri kesho.
Mimi naamini niya tunazo na uwezo tunao,naomba ushirikiano wenu wa kujenga Jumuiya bora na yenye kujitegemea yenyewe,Jumuiya yenye dira na kuifikia hiyo dira.
Hivyo basi katika kipindi cha uongozi wangu,nimekusudia kuunda msingi imara ya Jumuiya yetu.Jamii inafaidika na kuona umuhimu wa kuwepo kwa Jumuiya Nimekusudia kukuza mfuko wa Jumuiya kufikia $25,000.00.
Nimekusudia kukuza njia za mawasiliano na Watanzania wote wanaoishi North Carolina na nje ya North Carolina. Nimekusudia Tanzania ifaidike na kuwepo kwetu sisi huku na sisi Tufaidike na nchi yetu
ya Tanzania.
Hakuna lililokubwa au linaloshindikana, panapopatikana ushirikiano wa hali na mali tutashinda.
Ahsanteni sana
Mungu ibariki UTNC,Mungu ibariki North Carolina,Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment