ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 10, 2011

Albino afungwa minyororo kwa miaka mitatu kuhofia kuuawa

Mlemavu wa ngozi (albino), Mariam Juma (29), mkazi wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, amekuwa akiishi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo akiwa amefungwa minyororo miguu na wazazi wake kwa hofu asitoke nje akauawa na watu wenye imani za kishirikina.
Mlemavu huyo, alifungwa minyororo hiyo na baba yake mzazi, Juma Ngwatu, ambaye kwa sasa ni marehemu kwa madai ya kuimarisha usalama wake kutokana na mauaji ya albino yanayoendelea.
Aliendelea akiishi katika hali hiyo hadi juzi Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mathew Nasei, kufanikisha kupatikana kwa funguo zilizokuwa zimefungia minyororo hiyo miguuni.

Baada ya Mkuu wa Wilaya kufika anakoishi Mariam katika Mtaa wa Msikitini Kata ya Masuguru, alimuamuru mama mzazi wa binti huyo, Amina Mtunguja, kutoa funguo hizo. Awali, mama huyo alisisitiza kuwa hajui mahali zilipo funguo hizo kutokana na marehemu mumewe kutomuonyesha alikoziweka.
Mkuu wa Wilaya alisema kitendo hicho ni cha kinyama na serikali ya wilaya hiyo inafanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha familia hiyo kufanya hivyo.
“Sisi kama viongozi wa wilaya suala hili limetuhuzunisha sana katika kumbukumbu zetu hatukuwahi kujua kama kuna mtu anateseka kiasi hiki. Lakini tunalishughulikia kwa kuhakikisha kwanza binti huyu anapata matibabu ya kina tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo,” alisitiza.
Binti huyo kwa kipindi chote alifungwa na minyororo miguuni na kufungwa ndani ya moja ya vyumba vya nyumbani kwao.
Akizungumza katika mahojiano na NIPASHE, mama wa binti huyo, Mtunguja, alisema binti yake alianza kukabiliwa na matatizo ya akili mwaka 1996 akiwa darasa la saba na kwamba walihangaika naye kwa kipindi kirefu bila mafanikio.
Mama huyo alisema sababu ya Baba wa Mariam kufikia kumfunga mwanawe minyororo hiyo ni baada ya binti yao kuanza kufanyiwa vitendo vya kinyama jambo ambalo waliliona kuwa ni hatarishi kwa maisha yake.
Naye Josephat Torner Mratibu wa Kituo cha kulelea watoto na vijana wenye ulemavu (YDCP) aliiomba serikali kuchukua hatua za makusudi ili sheria ichukue mkondo wake kwa wahusika kwa madai kuwa kitendo hicho ni kinyume na haki za binadamu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: