ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 10, 2011

Shiboli aipaisha Simba kileleni

  Mwaikimba apiga 2, amshika Ngassa
Mshambuliaji Ali Ahmed Shiboli aliipeleka Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuifungia goli la ‘usiku’ katika mechi ya ugenini waliyoshinda 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro jana.
Mchezaji huyo aliyetua Simba Januari akitokea Zanzibar wakati wa kipindi cha uhamisho wa dirisha dogo, aliingia badala ya Mbwana Samatta katika dakika ya 78 na ilimchukua dakika nane kupeleka furaha Msimbazi baada ya kuiwahi pasi safi ya Mganda Emmanuel Okwi na kupiga shuti kali la karibu na lango lililomshinda kipa wa Ruvu, Gudhard Misheku na kwenda moja kwa moja wavuni.
Ushindi huo uliwapeleka Simba kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha pointi 39, moja zaidi ya mahasimu wao Yanga.
Awali, Simba walikosa bao la utangulizi katika dakika ya 34 wakati Okwi alipofanikiwa kuwalamba chenga mabeki watatu wa Ruvu na kushangaza kila mmoja wakati alipomalizia vibaya jitihada zake binafsi baada ya kupiga shuti kali lililopaa juu ya lango.
Katika mechi nyingine ya ligi kuu iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, wenyeji Kagera Sugar walitoka sare ya 2-2 dhidi ya Toto African ya Mwanza.
Magoli yote ya Kagera yalifungwa na mshambuliaji Gaudence Mwaikimba ambaye sasa amekuwa kileleni mwa orodha ya wafungaji baada ya kufikisha magoli 12, sawa na Mrisho Ngassa wa Azam.
CHANZO: NIPASHE

No comments: