Advertisements

Wednesday, March 30, 2011

Babu Loliondo atoa wasia kwa wagonjwa

Mzee wa kabila la wasonjo, Simbaje Wabao (81) akinywa dawa kwa Mchungaji Ambilikile Masapila katika kijiji cha Samunge, Loliondo, mkoani Arusha jana
Waandishi Wetu
MCHUNGAJI Ambilikile Masapila anayetoa tiba ya magonjwa sugu katika Kijiji cha Samunge, Loliondo amewataka wagonjwa kuendelea kutumia dawa za hospitali hata baada ya kunywa dawa yake.Akizungumza kijijini hapo jana, Mchungaji Masapila alisema hakuna madhara kwa mgonjwa kuendelea na dawa zake za awali hata baada ya kunywa dawa yake na kwamba si vyema kuacha ghafla kutumia dawa hizo.“Hii dawa yangu inatibu, lakini haizuii kunywa nyingine, unaweza kunywa na ukiona umepona kabisa usiendelee kunywa dawa hizo,” alisema. 

Vurugu zazuka Samunge
Polisi jana walilazimika kutumia nguvu za ziada kuwadhibiti watu waliokuwa wamefunga barabara ya kuelekea katika Kijiji cha Samunge na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.Barabara kuu ya kuingia katika kijiji hicho ilikuwa katika msukosuko kiasi cha baadhi ya watu kutishiana kwa silaha.Habari zilizolifikia Mwananchi zilisema, ulitokana na baadhi ya magari kutaka kuingizwa kwenye foleni bila kufuata utaratibu.

"Hapa kuna watu wanajifanya wao ndiyo Serikali au wao ndiyo kila kitu, sote ni wagonjwa na tunataka kwenda kwa Babu kunywa dawa, sasa kama mtu anafikia hatua ya kututishia sisi kwa bastola Serikali iko wapi?" alihoji mmoja wa watu, Heriel Mushi mkazi wa Mwika, mkoani Kilimanjaro.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ngorogoro (OCD), Listone Mponjoli jana alilazimika kuongoza askari wenzake kuendesha doria katika barabara hiyo ili kudhibiti dalili za uhalifu ambazo zimekuwa zikiripotiwa, pamoja na kuyaelekeza magari kukaa upande mmoja wa barabara ili kuruhusu kutumika kwa upande mwingine.

Katika doria hiyo, OCD Mponjoli alijikuta katika wakati mgumu pale wananchi walipozuia hata gari lake kupenya kuelekea eneo la Kibaoni, wakidai kwamba hawana imani naye kwani polisi wamekuwa wakivusha watu kinyemela na kuwawahisha kunywa dawa.Kulikuwa na vizuizi vya miiba vilivyokuwa vimewekwa kudhibiti upitaji holela wa magari katika eneo lililopo umbali wa kilometa kama tatu kutoka nyumbani kwa Mchungaji Masapila.

Mvutano mkubwa ulizuka katika mpaka wa Vijiji vya Samunge na Yasimbito ambako wasafiri walitumia magari yao kuziba barabara na OCD Mponjoli alipofika katika eneo hilo alizuiwa, hali iliyozusha mabishano makali baina yake na raia.Mkuu huyo wa polisi wa wilaya alisema ukaidi wa watu wanaokwenda kunywa dawa ndiyo chanzo cha vifo vinavyotokea kwani hata gari la kubebea wagonjwa wanaozidiwa linalosimamiwa na Chama cha Msalaba Mwekundu, limekuwa likizuiwa kwa madai kwamba 'linachakachua foleni'.

"Hatuwezi kuacha hali hii iendelee, lazima tuimarishe usimamizi wa usalama wa watu. Tukiachia raia waamue kufanya kila kitu, haki haiwezi kutendeka. Lazima watu waache ubinafsi wajue kwamba polisi tupo kwa ajili ya kutoa msaada kadiri tutakavyoona inafaa," alisema Mponjoli.Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali aliliambia Mwananchi kuwa watu wanaokwenda Samunge kunywa dawa, wamekuwa wakali kiasi cha kuzuia utekelezaji wa shughuli nyingine zisizohusiana na utoaji wa tiba ya Mchungaji Masapila.

"Hapa ni wilayani kuna shughuli nyingi, sasa watu wanaokwenda pale Samunge wamefunga ile barabara ya kuingia pale kijijini na tunashindwa kutekeleza majukumu mengine ya kijamii kwa sababu tu ya hii tiba,"alisema Lali na kuongeza:
"Tunawaomba wananchi wanaofika kijijini pale wawe na uelewa kwamba ile barabara ilikuwapo kabla ya kuanza kutolewa kwa tiba ya Baba Mchungaji, hivyo inafaa iendelee kutumika kwa shughuli nyingine hata kama siyo za tiba."

Serikali yamkuna Mchungaji
Mchungaji Masapila ameelezea kufurahishwa kwake na matokeo ya utafiti uliofanywa na Serikali uliothibitisha kwamba dawa anayotoa ambayo inatokana na mti wa mugariga haina madhara.Akizungumza na Mwananchi jana asubuhi alisema hata hivyo, kwamba hakushangazwa na matokeo hayo kwani tayari Mungu alikwishamthibitishia kwamba dawa hiyo haina madhara yoyote kwa binadamu.“Naishukuru Serikali maana naona wananiunga mkono, hii ni dawa kutoka kwa Mungu na wala sio mti pekee na nilijua wakipima hawatakuta madhara yoyote kwani Mungu alikwishanieleza kuwa watapima wataalamu wa ndani na nje ya nchi dawa hii na watakuta haina madhara,” alisema.

Alisema dawa ambayo anatoa imekuwa na mafanikio makubwa katika afya za watu, kwani wanampa taarifa za kupona magonjwa mbalimbali hata yale ambayo hakutegemea kwamba yataponywa na dawa hiyo.“Watu wenye vidonda vya tumbo wanapona, kina mama wanapata mimba, watu wanapona kifafa, pumu, kansa na magonjwa mengine, hivyo hili linathibitisha ubora wa tiba hii,” alisema.Mchungaji Masapila pia alisema kazi ambayo amekuwa akifanya kwa saa zaidi za 13 kila siku, haimsumbui akidai kwamba tayari alikwishamuuliza Mungu kwamba atawezaje kutoa tiba kwa watu wengi ilihali ni mzee na akaelezwa kuwa ataongezewa nguvu.

Ushuhuda waliopona 
Baadhi ya watu ambao tayari wamepata tiba jana waliendelea kutoa ushuhuda. Mmoja wao ni Hassan Kaniki Mkazi wa Dar es Salaam ambaye alisema tangu amekunywa dawa hiyo Alhamisi iliyopita amepona ugonjwa wa kisukari.Kaniki alisema kwa zaidi ya miaka mitano amekuwa akitumia dawa za kisukari lakini tangu juzi, sukari imeshuka na kufikia 5.5 jambo ambalo halijawahi kutokea.

“Tangu juzi nakunywa soda, nakula wali nakula nyama na situmii dawa. Nimepona kabisa, sijui labda baadaye,” alisema Kaniki ambaye bado alikuwa Samunge akisubiri familia yake kupata tiba.

Mkazi mwingine wa Dar es Salaam, Merere Mwambene naye alidai kuwa amepona ugonjwa wa kisukari na kwamba tangu juzi jioni alipokunywa dawa hiyo alikunywa soda na jana asubuhi alikunywa chai yenye sukari bila kuathirika.
"Kabla sijanywa dawa nisingeweza kukaa muda wote huu bila kujidunga dawa na ilikuwa nikipitisha muda tu, macho yalikuwa mazito na kuanza kushindwa kuona kabisa, lakini hali ni tofauti tangu nilipokunywa dawa."
Mgonjwa mwingine ni Jonathan Magesa kutoka Mwanza ambaye amekuwa akisumbuliwa na pumu. Alisema tangu ametumia dawa hiyo anajisikia kupona na hatumii tena dawa.

Pemba walilia 
Wakazi wa Pemba, wamemwomba Mchungaji Masapila kuwasogezea huduma ya tiba ya magonjwa sugu ili nao wanufaike nayo.Baadhi ya wakazi hao waliofika kwenye ofisi za gazeti hili zilizopo katika Jengo la Bandari, Tanga walisema wamekuwa wakifuatilia kwa karibu tiba hiyo kupitia vyombo vya habari na kugundua kuwa kimsingi ina ukweli.

Mmoja wa wakazi hao, Shaame Ussi alisema baada ya kusikia kuwa dawa hiyo inaponyesha na kuwaona hata viongozi wa Serikali wanainywa, ni vyema sasa huduma hiyo ikawasogelea watu ili wanufaike nayo.Ussi alisema ingekuwa vyema kama mchungaji huyo angeipeleka huduma hiyo mkoani Tanga ili kuwawezesha wakazi wa Pemba kuipata.

Habari hii imeandikwa na Salim Mohamed, Neville Meena na Mussa Juma wa Gazeti la Mwananchi, Samunge

No comments: