Advertisements

Wednesday, March 30, 2011

Wanasiasa waenguliwa Tume ya Katiba Mpya

Mwandishi Wetu
MUSWADA maalumu wa kuunda Tume ya kukusanya maoni na kupendekeza muundo wa Katiba mpya ya Tanzania, unatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la Aprili, mwaka huu.Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa muundo wa tume hiyo hautawashirikisha wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Madiwani wala kiongozi yeyote wa kisiasa.

Tume hiyo inayotarajiwa kuwa na wajumbe 30, itaundwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na wajumbe wake watakuwa ni wanataaluma, hususan wanasheria na kwamba suala la jinsia litazingatiwa.


Taarifa hizo zinaeleza pia kuwa Tume itaundwa na idadi sawa ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na Visiwani na inatarajiwa kuwa na majukumu mbalimbali ikiwamo kuwahamasisha watu kujua maana na muundo wa Katiba.

Majukumu mengine ya tume hiyo yaliyotajwa kwenye muswada huo ni kukusanya maoni kutoka kwa wananchi, kuchunguza na kuainisha muundo wa Katiba kulingana na mifumo ya kisiasa, kidemokrasia, uongozi, sheria za kiutawala na Serikali.

Mara baada ya Bunge kupitisha muswada huo, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuusaini na kuiunda haraka iwezekanavyo tume hiyo ili ifikapo Juni mwaka huu ianze kazi yake.Kamati hiyo itatoa rasimu ya katiba hiyo mpya ikipendekeza pia muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano utakavyokuwa.

Mchakato wa kuunda tume hiyo unakuja baada ya Rais Kikwete kuwataka wananchi kuwa watulivu akisema suala hilo litaratibiwa kwa umakini ili kuwa na katiba bora ambayo itawasaidia Watanzania kwa muda mrefu.

Tamko la Rais Kikwete la kuunda tume hiyo ndilo lililozima wimbi la madai ya Katiba mpya lililoshika kasi miongoni mwa watu wa kada mbalimbali ikiwamo wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida.Katika mijadala hiyo, Katiba iliyopo imeelezewa kuwa imepitwa na wakati na haiendani na mahitaji ya mazingira ya sasa ya nchi.

Vuguvugu hilo lilianza mara baada ya Uchaguzi Mkuu, Novemba mwaka jana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kudai kuwa Katiba ya sasa haitoi haki ya kidemokrasia kwenye uchaguzi.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: