Advertisements

Wednesday, March 30, 2011

Kamati ya Zitto yalia na General Tyre

Na Tumaini Makene

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Mahesabu ya Shirika ya Umma (POAC), imedhamiria kuinusuru kampuni ya kutengeneza matairi ya General Tyre East African Ltd. kwa
kuchunguza mchezo mchafu unaohisiwa kuwepo katika 'kifo' chake.

Kamati hiyo imeunda kamati maalumu itakayojumuisha wabunge wanne, Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), watakaochunguza namna gani kiwanda hicho kiliweza kujipatia mkopo wa dola za Marekani milioni 10 mwaka 2005, lakini ilipofika mwaka 2008 kikashindwa kuendelea na uzalishaji.


Kampuni hiyo ya General Tyre, iliwahi kusifika katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, kwa uzalishaji na usambazaji wa matairi yenye ubora na kiwango cha hali ya juu, kabla ya kufunga shughuli zake mwaka 2009, miaka minne baada ya kuchukua mkopo wa sh. bilioni 10, kwa msaada wa serikali, kutoka Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Jana kamati hiyo ya POAC ilielezwa kuwa deni hilo sasa limefikia sh. bilioni 21.15 ambapo NSSF wanataka kiwanda hicho kiuzwe ili fedha hizo ziweze kurejeshwa, huku serikali nayo ikisema kuwa kifilisiwe, lakini kamati hiyo imekataa mapendekezo hayo, mpaka uchunguzi huo ufanyike, kwa maslahi ya nchi.

Kati ya sababu ambazo zimekuwa zikitajwa za 'kufa' kwa kampuni hiyo, licha ya kupata mkopo, ni uagizwaji na uingizwaji wa matairi yaliyotumika na kuuzwa rejareja kwa bei ya chini. 

Ingawa sababu nyingine kubwa ambayo imekuwa ikidaiwa 'kuiua' General Tyre, ni mwekezaji aliyepewa kiwanda, akiendesha kiwanda hicho kwa ubia na serikali ya Tanzania, kutotaka kuendelea na shughuli hiyo, kuwa utengenezaji wa matairi hakikuwa kipaumbele chake.

Akizungumza na watendaji wa shirika lililochukua nafasi ya Shirila la Kurekebisha Mashirika ya Umma, Consolidated Holding Corporation (CHC), jana baada ya POAC kupitisha hesabu za shirika hilo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Kabwe Zitto, alisema kuwa kamati hiyo ya kuchunguza 'kifo' cha General Tyre itafuatilia matumizi ya mkopo huo wa NSSF, iwapo ulitumika kama ilivyokusudiwa na taratibu zilizotumika kukopesha.

"Katika suala la General Tyre nashukuru mmetuletea taarifa yake, lakini it is not detailed as expected (si ya kina kama ilivyotarajiwa)...sasa deni limefikia sh. bilioni 21.15...NSSF walikuwa wanataka kiwanda hiki kiuzwe, serikali nao wanataka kifilisiwe. Hatuwezi kuuza kiwanda hiki halafu nchi ibaki kutegemea matairi ya nje.

"Tumeunda timu ya wabunge wanne, kufanya uchunguzi wa kampuni hiyo, itakayokuwa na wabunge wanne, watatu wa kamati hii, mmoja kamati ya viwanda na biashara na mtu wa ofisa ya CAG, watu wa CHC mnatakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha utakapotakiwa na tumeipatia hadidu za rejea tayari," alisema Bw. Zitto.

Alitaja hadidu hizo kuwa ni pamoja na kufuatilia matumizi ya mkopo waliokopa kutoka NSSF, taratibu zilizotumika, mali zilizokuwa zikimilikiwa na kampuni hiyo, msimamo wa serikali kutaka kuifilisi kampuni hiyo, iwapo una maslahi ya umma na kuangalia namna ya kuifufua.

"Tunahisi kuna mchazo mchafu, maana waliomba mkopo lakini wanasema hawawezi kuendesha...tuangalie mkopo ulivyotumika, taratibu za kupata mkopo huo...tunataka nchi ishindane katika kuzalisha bidhaa, tunataka kiwanda hiki kizalishe ajira kwa Watanzania.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: