ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 28, 2011

Barua za watuhumiwa ufisadi CCM bado kitendawili

Suala la kuwakabidhi barua makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotuhumiwa ufisadi za kuwaarifu kuondolewa katika uongozi wa chama, limezidi kuwa gumu kwa chama hicho.
Hali hiyo imedhihirika, baada ya sekretarieti mpya iliyoingia madarakani mwezi huu, kuendelea kutupiana mpira juu ya lini kazi hiyo itakamilishwa.

Wakati kukiwa na taarifa kwamba, barua hizo zimeishaandaliwa na kumfikia Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzani Bara, Pius Msekwa mezani kwake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye jana alipoulizwa na NIPASHE kuhusu suala hilo alijibu kuwa hajajua siku wala tarehe ya kuanza kuwakabidhi watuhumiwa hao.
Akizungumza na NIPASHE jana, Nnauye alithibitisha barua hizo kufika mezani kwa Msekwa.
Hata hivyo, alipoulizwa ni lini wahusika watazipata, aligoma kuzungumza na kusisitiza kwamba, hakuna mabadiliko ya suala hilo.
Kama nilivyotoa taarifa yangu jana (juzi) kwamba barua hizo zipo kwa Msekwa hakuna mabadiliko yoyote mpaka sasa yaani jana mchana,” alisema Nnauye.
Nnauye, alikaririwa na vyombo vya habari juzi akisema kwamba, tayari barua hizo zimeshaandaliwa na kwamba, wahusika wangekabidhiwa jana.
Barua hizo zinalenga kuwaondoa makada watatu wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya CCM na kuwataka wajiondoe katika nafasi za uongozi ndani ya chama hicho.
Suala hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Halmashauri Kuu (NEC) CCM, yaliyofikiwa katika kikao chake kilichofanyika hivi karibuni, mjini Dodoma.
NEC iliagiza ndani ya siku 90 makada wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi wawe wamejiondoa katika nafasi zao ndani ya chama, ambapo sekretarieti yake ilianza kwa kutangaza dhana ya chama hicho ya ‘kujivua gamba’.
Wananchi wamekuwa wakifuatilia kauli hizo za CCM za kujivua gamba pamoja na kuwachukulia hatua watuhumiwa wote wanaokichafua chama kutokana na tuhuma za ufisadi zinazowakabili muda mrefu sasa.
Kwa upande wao, viongozi wa dini mwishoni mwa wiki iliyopita, walimshauri Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kuhakikisha chama hicho kinajivua gamba kwa vitendo.
Viongozi hao, ambao walimwalika Rais Kikweye katika tamasha la Pasaka na kuwa mgeni, walipata fursa ya kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili apate nguvu na ujasiri kwa kushirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha chama kinavuliwa gamba na kubaki kipya.
CHANZO: NIPASHE

No comments: