ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 28, 2011

Usiombe ukaoa binti mzuri, aliyesoma lakini asiyejua kupenda!-GPL

Natumaini umzima bukheri wa afya na unaendelea vyema na michakato mbalimbali ya maisha yako. Mimi namshukuru Mungu kwa kunijaalia uzima ambao ndiyo umenifanya leo hii niweze kuwaletea mada nyingine ikiwa ni katika kuwekana sawa juu ya maisha yetu ya kimapenzi.

Mpenzi msomaji wangu, naamini wapo walioshituka kuona kichwa cha habari hicho hapo juu lakini ni ukweli usiofichika ambao leo nimelazimika kuuandika ili wanaume wenzangu wanaotaka kuingia katika maisha ya ndoa wawe makini katika kuchagua wenza sahihi.


Huko nyuma ukimuuliza mwanaume aina ya mwanamke anayetaka kumuoa, kigezo cha kwanza atakuambia lazima awe mzuri. Uzuri unaozungumziwa hapa ni wa sura na umbo.

Hilo halina ubishi kwa kuwa, kila mmoja anataka kitu kizuri, kila mmoja anataka kuwa na mke ambaye akipita naye mbele za watu kila mmoja atatingisha kichwa ikiwa ni ishara ya kumkubali.

Kigezo kingine mwanaume atakuambia anataka kuoa mwanamke anayefanya kazi. Ukiuliza kwa nini, atakuambia ili wasaidiane katika kuyaendesha maisha yao.

Hili nalo ni sahihi kabisa kwa sababu maisha ya sasa ni magumu, kusaidiana katika masuala ya kifedha kuna umuhimu wake. Lakini sasa, ninachotaka kuwatahadharisha wanaume wenzangu ni kutoangalia vigezo hivyo viwili tu kisha wakaingia katika maisha ya ndoa, hakika watajuta.

Nasema hivyo kwa sababu, hakuna wasichana wanaowaumiza vichwa wapenzi wao kama wale ambao wanajijua ni wazuri, wamesoma na wana kazi zao.

Yaani baadhi yao wamekuwa na nyodo zisizokuwa na maana kwa wanaume na wakati mwingine kwa wanawake wenzao. Wanawake hawa wapo huko mtaani na wewe unayesoma hapa utakuwa ni shahidi. Yaani wanajiona wao ndiyo wao na hata kupokea salam wanachagua wa kuwapokelea. Kwa kifupi wanajiona ni keki.

Baadhi ya hawa ndiyo ambao wamekuwa wakiwatesa wapenzi wao wakiamini kwamba hata wakiachwa, hawawezi kupata tabu kutokana na usumbufu wanaoupata kutoka kwa wanaume wengine nje.
Wanaringia kazi zao, wanaringia uzuri wao bila kujua kwamba, mapenzi nayo yana sehemu kubwa katika maisha yao, wengine hawajui hivyo ndiyo maana wanafikia hatua ya kuutumia uzuri wao na kazi zao vibaya.

Sasa hili ni tatizo ambalo linaweza kuyatingisha maisha ya wanaume endapo hawatakuwa makini katika kuchagua wenza sahihi. Unapotaka kuoa, ni vyema ukajiuliza kwanza kama huyo uliyenaye anakupenda kwa dhati, achilia mbali kazi yake na uzuri wake.

Nasisitiza katika hili kwa sababu wakati mwingine nahisi ni heri kuoa mwanamke wa kawaida, asiye na kazi lakini mwenye mapenzi ya dhati ili kujihakikishia amani katika moyo wako.
Asikudanganye mtu kuna wanaume wana fedha zao lakini maisha yao yamekuwa ni ya mateso kutoka kwa wake zao. Hawana sauti kwa wake zao. Wake zao hao wamekuwa ni viburi, wasiopenda kukosolewa, kuelekezwa wala kuulizwa jambo lolote na ikitokea hivyo watakuwa wakali na wakati mwingine kutishia kuvunja uhusiano.

Sasa utawezaje kuishi na mwanamke wa dizaini hii? Si unaweza kujikuta unaumwa vidonda vya tumbo bila sababu?
Ifike wakati tutambue kuwa, mapenzi yanaathiri kwa kiasi kikubwa maisha yetu hivyo tufanye maamuzi sahihi inapofika wakati wa kuchugua mtu wa kuwa naye katika maisha.
Leo nilitaka kusema hilo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi.

No comments: