Advertisements

Thursday, April 28, 2011

Mshana amrithi Tido Mhando TBC

RAIS Jakaya Kikwete amemteua Clement Mshana kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). 

Rais Kikwete pia amemteua Katibu Mkuu mmoja wa Wizara na naibu makatibu wakuu 10. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, George Yambesi, Mshana anachukua nafasi ya Tido Mhando aliyemaliza muda wake wa utumishi kwa mujibu wa mkataba. 

Yambesi alisema, uteuzi huo wa Mshana ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), ulianza Alhamisi.
 

Mkataba wa Tido ulimalizika Desemba mwaka jana na kwa mujibu wake wakati huo, aliandikiwa barua ya kutakiwa kuondoka baada ya Serikali kutomwongeza mkataba. 

Tangu wakati huo, nafasi ya Tido ilikuwa ikikaimiwa na Joe Rugarabamu ambaye kwa mujibu wa mabadiliko ya muundo wa TBC mwaka 2007, alikuwa Meneja Biashara na Utawala. 

Mshana alipata kufanya kazi TBC akiwa Mkurugenzi wa Programu na alikaimu nafasi ya Meneja Mkuu anayeshughulikia televisheni. 

Katika hatua nyingine, mbali na uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara na naibu makatibu wakuu 10 wa wizara mbalimbali, Rais Kikwete amemhamisha Naibu Katibu Mkuu mmoja kutoka wizara moja kwenda nyingine. 

Kwa mujibu wa taarifa, uteuzi wa maofisa hao waandamizi wa Serikali ulianza Alhamisi na wataapishwa Jumamosi saa sita mchana. 

Taarifa hiyo ilisema Rais Kikwete amemteua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Job Masima kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo. 

Aidha, amemhamisha Mbogo Futakamba aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji kwenda Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, naibu makatibu wakuu walioteuliwa na Rais ni Aphayo Kidata anayekwenda Ikulu. Kabla ya uteuzi wake, Kidata alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. 

Mwingine ni Hab Mkwizu anayekwenda Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kabla ya uteuzi wake, alikuwa Karani wa Baraza la Mawaziri. Charles Pallangyo anakwenda Ofisi ya Waziri Mkuu. 

Kabla Pallangyo alikuwa Mkurugenzi wa Uratibu – Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, Rais amemteua Mwamini Malemi kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kabla ya hapo, alikuwa Msaidizi wa Makamu wa Rais katika masuala ya Maendeleo ya Jamii na Uratibu wa Malalamiko ya Jamii. 

Mussa Iyombe anakwenda Wizara ya Ulinzi na JKT. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi wa Miundombinu ya Usafiri katika Wizara ya Ujenzi. 

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi katika Wizara ya Ujenzi, Dk. John Ndunguru, anakuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo. John Mngodo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi. Kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula. 

Anna Maembe anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, ambapo kabla alikuwa Mkurugenzi wa Mazingira na Habari wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). 

Sihaba Nkinga ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo baada ya kuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Uchukuzi. 

Aliyekuwa Kamishna wa Nishati na Petroli Wizara ya Nishati na Madini, Bashir Mrindoko, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: