ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 18, 2011

Baba mkubwa aua mtoto kwa kipigo

  Mwalimu abaka mtoto wa chekechea
Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinaendelea kukithiri nchini, baada ya mtoto wa miaka tisa kuuawa na baba yake mkubwa kwa madai ya kumuibia pesa na mwingine wa miaka minne kulawitiwa na mwalimu wa shule ya sekondari.
Katika tukio la kwanza, Vicky Christopher (9), mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kambarage ya Jijini Mbeya, ameuawa kikatili na baba yake mkubwa baada ya kufungwa mikono na kupigwa kisha akafungiwa kwenye kiroba kabla hajapoteza maisha.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Alice Mdesa, alidai jijini Mbeya jana kuwa mwanaye alikufa baada ya kupigwa na baba yake mkubwa, Sheddy Mdeka (40).

Alice ambaye anaishi Dar es Salaam, alidai alipigiwa simu juzi na majirani wa eneo alilokuwa akiishi mwanaye na kupewa taarifa za mauaji hayo.
Kufuatia taarifa hizo, mama huyo alidai kuwa alisafiri kwenda Mbeya na alipofika alikuta mwanae amekufa huku akiwa na alama za kufungwa kamba mikononi na miguuni. Mama huyo alidai taarifa alizopata kutoka Polisi zinadai kuwa baada ya mtuhumiwa kumpiga mwanae, alimweka ndani ya kiroba na kumfungia ndani siku nzima hadi majirani walipogundua na kumchukua wakamkimbiza hospitalini.
Alidai walipomfikisha Vicky katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, madaktari walikataa kumpokea wakitaka wahusika waanzie Polisi na kupewa fomu No. 3 (PF3) kabla ya kumpatia matibabu.
Mama huyo alidai kuwa majirani hao waliamua kwenda Polisi na mwanae ili kupewa fomu hiyo, na ndipo mtoto huyo alipofariki dunia akiwa katika kituo cha Polisi cha Kati jijini Mbeya wakisubiri kupewa fomu hiyo.
Alidai baada ya kufika Polisi aliwaomba azungumze na mtuhumiwa na aliporuhusiwa alimuuliza sababu za kumpiga mwanae hadi akamuua.
Alidai mtuhumiwa alimweleza kuwa mtoto aliiba Sh. 3,500 za jirani yao na kuwa baada ya kumbana alizirejesha na ndipo alipoamua kumuadhibu.
Alice alidai mwili wa mwanaye ulitarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina jana kabla ya mazishi.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Anacret Malindisa, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuongeza kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi.

MWALIMU ADAIWA KULAWITI MTOTO
Katika tukio la pili, Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Nyumbu, Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, (jina linasitiriwa kwa sasa), anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Temeke kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa shule ya chekechea mwenye umri wa miaka minne (jina linahifadhiwa).
Mwalimu huyo, mkazi wa Mtaa wa Mandela (zamani Wailes), Wilaya ya Temeke, anadaiwa kufanya kitendo hicho juzi mchana.
Mama mzazi wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa), alidai tukio hilo lilitokea juzi mchana, nyumbani kwake. Mwalimu huyo alikuwa mpangaji wake.
Alidai kuwa alibaini kubakwa kwa mwanaye baada ya kumtafuta bila mafanikio kwa lengo la kumuandaa kwenda madrasa.
Mama huyo alidai kuwa baadaye mtoto huyo alijitokeza na kueleza kuwa alikuwa chumbani kwa Mwalimu huyo.
Mtoto huyo alidai akiwa chumbani kwake, Mwalimu huyo alimlaza kitandani na kumvua nguo zote na kumfanyia kitendo hicho kisha kumweleza kuwa asimwambie chochote mama yake.
" Baada ya kumfanyia vibaya alimfundisha asiseme chochote. Lakini ni kama alikuwa kamfundisha aniambie, alipofika tu aliniambia nilikuwa kwa Mwalimu. Amenilaza kitandani, akanivua nguo na yeye akavua halafu...,” alidai mama huyo huku akilia.
Alidai kuwa walimuita Mwalimu huyo mbele ya mumewe na kukiri kumfanyia mtoto kitendo hicho kama alivyowasimulia.
Mama huyo alidai kuwa Mwalimu huyo alidai alifanya kitendo hicho baada ya kupitiwa na shetani.
Walitoa ripoti kituo cha Polisi Chang’ombe na kisha kumpeleka mtoto wake hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Alidai kuwa Polisi walimkamata mtuhumiwa huyo akiwa anahamisha vitu vyake kwenye vyumba alivyokuwa amempangisha.
Baadhi ya majirani waliomshuhudia Mwalimu huyo akiwa chini ya ulinzi wa polisi, walilaani kitendo hicho cha kinyama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime, alipoulizwa jana, alisema hadi kufikia jana mchana, taarifa kuhusu kukamatwa kwa mwalimu huyo kutokana na kitendo hicho zilikuwa hazijafika ofisini kwake.
"Hiyo taarifa sina. Natoka kwenye kikao ndio narudi sasa hivi," alisema Kamanda Misime.
CHANZO: NIPASHE

No comments: