ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 19, 2011

`Madai ya walimu ni zaidi ya pick-up`

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia.
Serikali imepokea taarifa ya madai ya stahili za walimu zaidi ya Sh. bilioni 29, wanazoidai na kusema inafanya uhakiki kujiridhisha baada ya kuwasilishwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), zaidi ya gari moja aina ya Toyota Pick –Up.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, alitoa kauli hiyo bungeni jana kuwa Agosti 16, mwaka huu, Serikali ilipokea majina na madai ya stahili za walimu baada ya kuwasilishwa na CWT.

“Madai ya walimu tumepokea tarehe 16 Agosti, mwaka huu lakini ni mzigo wa makaratasi zaidi ya Pick-Up, kwa hiyo kwa sasa tunahakiki upya ili tujiridhishe kwanza ndiyo tuanze mchakato wa kulipa hizo stahili,” alisema Ghasia.
Waziri Ghasia alikuwa akijibu swali la nyongeza mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, aliyetaka kupata kauli ya serikali ni lini italipa madeni ya walimu wanayoidai zaidi ya sh. bilioni 29.
Katika swali la msingi, mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vincent Nyerere, alitaka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya kuboresha hali ya walimu nchini, kwa lengo la kuwa na walimu bora watakaoweza kufanya kazi yao kwa uadilifu mkubwa na kuwa na matokeo mazuri kwa wanafunzi wanaowafundisha.
Akijibu, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema Serikali imeweka mikakati ya kuinua taaluma, mazingira ya kazi ya ualimu na maslahi yao.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuimarisha miundombinu ya shule kwa kukamilisha majengo ambayo hayakukamilika wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) awamu ya kwanza, ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, maabara na vyoo.
Katika majibu yake, Mulugo alisema walimu zaidi ya 200 wa masomo ya Fizikia, Kemia, Biolojia na Hisabati, wamepata mafunzo ya kuwajengea uwezo kati ya mwezi Julai 2010 hadi Julai, mwaka 2011.
Mulugo alisema serikali itawapa motisha ya Sh. 500,000 walimu wanaopangiwa kufanya kazi katika maeneo yenye mazingira magumu kwa mara ya kwanza.
CHANZO: NIPASHE

No comments: