ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 19, 2011

Takukuru yadaka makada CCM mkutanoni Igunga


 Wadaiwa kukutwa katika mazingira ya kugawana rushwa
  Walikuwa kwenye eneo la mkutano wa kura za maoni
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
Wakati vyama vya CCM na Chadema vikiwa katika mchakato wa kura ya maoni ya kuwapata wanachama watakaowania ubunge katika uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wilayani humo, imewakamata wafuasi watatu wa CCM kwa tuhuma za rushwa.
Watu hao ambao majina yao hayajafahamika, walikamatwa jana baada ya kukutwa na maofisa wa Takukuru wakiwa katika mazingira yaliyoashiria kuwa walikuwa wakigawana rushwa. Watu hao walikamatwa kwenye eneo ambako mkutano mkuu maalum wa CCM wa wilaya wa kura za maoni ya kumpata mgombea ubunge kupitia chama hicho ukifanyika.

Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Igunga, John Ngunangwa, alithibitisha kukamatwa kwa watu.
“Tuliwashikilia kwa muda, baadaye walidhaminiwa,” alisema Ngunangwa alipozungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana.
Alisema watu hao walikamatwa baada ya Takukuru kupata taarifa kwamba walionekana wakiwa katika mazingira yaliyoashiria kuwa walikuwa wakigawana rushwa.
Ngunangwa alisema walikuwa kwenye eneo ambalo zoezi la upigaji kura za maoni za kumpata mwanachama atakayewania ubunge kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi huo na kwamba, uchunguzi kuhusu tuhuma zinazowakabili unaendelea.
Hata hivyo, alisema asingeweza kukumbuka majina na nyadhifa za watuhumiwa hao kwa vile muda ambao alizungumza na mwandishi, alikuwa nje ya ofisi.
CCM ambayo ilifanyia mkutano wake huo katika ukumbi wa Shule ya Msingi Sant-Leo, iliyoko mjini Igunga, uliwashirikisha wajumbe 953 kutoka katika matawi yaliyopo jimboni humo.
Wakati CCM ikifanya mkutano wake, Chadema ilifanya mkutano wake katika ukumbi wa Sakao uliotumiwa na Rostam Aziz kutangaza kujiuzulu ubunge na ujumbe wa Halmashauri ya Kuu (NEC), ya chama hicho.
Mkutano huo wa Chadema uliwashirikisha wajumbe 298 kutoka matawi yote ya chama hicho jimboni humo.
Hata hivyo, mikutano hiyo ya uteuzi ilifanyika wakati mji wa Igunga ukiwa katika giza kwa siku mbili mfululizo kuanzia juzi.
Akifungua mkutano wa CCM, Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) Taifa na mlezi wa chama hicho Mkoa wa Tabora, Mwigulu Nchemba, alisema uteuzi wa mgombea wa chama chake utaangalia mwanachama atakayetekeleza Ilani ya Chama katika miaka minne ijayo na si vinginevyo.
Akijibu tuhuma zilizotolewa na Chadema dhidi ya CCM kwamba imeanza mchezo mchafu, Mwigulu, ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, alisema kauli hizo ni za kuijaribu CCM ili ionekane kama inaweza kuingia uwanjani kwa kushindana wakati kazi bado haijaanza.
Alisema “malalamiko yanayotolewa na baadhi ya vyama hayana msingi wowote kwani serikali ipo tayari katika mkakati wa kutekeleza ahadi zake. Na hakuna muda wa kuwalaghai wananchi ili chama chochote kipate kura.”
Wakati Mwigulu akisema hayo, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa Chadema, Benson Kigaila, aliwataka wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho wilaya, kutokubali kurubuniwa na mtu yeyote atakayejitokeza akiwa na malengo ya kulichukua jimbo hilo.
Hadi tunakwenda mitamboni, majina ya wanachama watatu watakaopelekwa katika CC za kila chama, yalitarajiwa kutangazwa baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika jana jioni.

CHANZO: NIPASHE

No comments: