ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 19, 2011

Wafanyakazi Kilombero wagoma, kiwanda chasitisha uzalishaji wa sukari

Shamba la miwa Kilombero
Zaidi ya wafanyakazi 1,500 wa kiwanda cha sukari cha Kilombero (ILOVVO), mkoani Morogoro, ambao ni wakatamiwa wa kiwanda hicho, wamegoma kwa muda usiojulikana, kwa siku ya nne mfululizo sasa, ili kushinikiza uongozi kuongeza mishahara ambayo walidai ni midogo isiyolingana na kazi ngumu wanazofanya.
Kufuatia mgomo huo, kiwanda kimoja kati ya viwili vinavyozalisha sukari K1 kimefungwa kutokana na kukosa miwa.

Kiwanda kingine cha K2, kwa sasa kinazalisha sukari kwa miwa kutoka kwa wakulima wa nje, ambayo hata hivyo haikidhi mahitaji ya viwanda vyote viwili ya kusaga tani zaidi ya 700,00 kwa siku.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Evarist Ndikilo na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Halima Dendego, walilazimika kufika kiwandani hapo jana ili kuwasihi kuacha mgomo huo kwa kuwa Serikali imeanza kuushughulikia madai yao, lakini wafanyakazi walipingana nao na kuendelea na mgomo.
Madai mengine wanaolalamikia ni wananchi wanaozunguka kiwanda hicho kuwa na vitendo vya uhalifu ukiwemo uporaji, ubakaji na uharibifu wa mashamba ya miwa tuhuma ambazo walizikana vikali.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wafanyakazi hao, Andrew Mwaisenye, alisema wamegoma baada ya kiwanda kupuuza madai yao ambayo walishawasilisha mapema mwaka huu.
Alisema wakatamiwa wamekuwa wakinyonywa malipo yao huku wakifanya kazi ngumu na kuwanufaisha wenzao wachache wa kada ya juu.
Naye Mashaka Mwaipaja, alisema mgomo huo umekuja ili kushinikiza uongozi wa Kiwanda hicho kuongeza malipo kutoka ya sasa ya Sh. 4,400 wanayolipwa kwa siku hadi Sh. 7,000 hadi Sh. 10,000 kwa siku, kiasi alichodai wanalipwa wenzao wanaofanyakazi kwa wakulima wa nje. Kufuatia hali hiyo, wakuu hao wa Wilaya walikutana na menejimenti na viongozi wa vyama vya wafanyakazi ili kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Baada ya kikao, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Ndikilo, aliwaeleza wafanyakazi kwamba serikali imeazimia kumaliza mgogoro huo na kuwaomba warejee kazini, lakini walishikilia msimamo wao wa kugoma na kususia kikao.
Hata hivyo, walirejea baadae ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Dendego akakiri kwamba serikali ilikuwa inashughulikia mgogoro huo bila kujua madai ya msingi ya wafanyakazi hao.
Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Issa Machibya, kulazimika kuitisha kikoa cha dharura mjini Morogoro jana baina ya wafanyakazi hao na kuwasihi kuendelea na kazi wakati serikali ikishughulikia madai yao.
Machibya alisema serikali ya Mkoa wa Morogoro itakutana na menejimenti ya kiwanda hicho ili kutafuta muafaka.
CHANZO: NIPASHE

No comments: