ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 19, 2011

Yanga yakiri Simba inatisha

Kocha msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro
Wakati kocha msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro akikiri kwamba timu yake ilizidiwa katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii waliyocheza dhidi ya mahasimu wao Simba na kulala 2-0, kocha Moses Basena wa ‘Wekundu wa Msimbazi’ amejigamba kuwa moto wao hautazimika hadi watakapotwaa taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Simba iliyoanza saa 2:00 usiku juzi, Minziro alisema kuwa kasi ya wapinzani wao katika kipindi cha kwanza na makosa madogo ya safu yao ya ulinzi ni sababu mojawapo zilizowaathiri na hatimaye kujikuta wakifungwa na watani zao wa jadi.

Alisema vijana wao walizinduka katika kipindi cha pili na kuonyesha soka safi, lakini bahati haikuwa yao na hivyo anakubali kuwa walizidiwa.
"Ndio soka ilivyo… ina matokeo ya aina tatu na wenzetu walitumia vizuri nafasi walizopata. Nalazimika kukubaliana na matokeo,” alisema Minziro, beki matata wa zamani wa Yanga.
Aliongeza kuwa matokeo hayo hayatawaathiri katika mechi za ligi kwani bado wana kiwango bora na anaamini kuwa watafanya vizuri katika kila mechi.
Kocha mkuu wa Yanga, Sam Timbe, alisema kuwa mechi ya juzi ilikuwa ngumu, lakini bahati haikuwa yao kwani wapinzani wao walitumia vyema nafasi walizopata.
Timbe alisema watafanya marekebisho ya kasoro zilizojitokeza na anaamini kuwa watafanya vizuri wakati watakapokutana kwenye mechi yao ya mzunguko wa kwanza wa ligi itakayopigwa Oktoba 29.
Kocha wa Simba, Basena, alisema ushindi walioupata dhidi yaYanga wataundeleza pia katika ligi kuu ya Bara, wakianzia na mechi ya keshokutwa Jumapili dhidi ya JKT Oljoro watakayocheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika juzi na kuipa Simba taji lake la kwanza, Basena alisema kwamba amefurahi kuona kuwa timu aliyokuwa akiijenga imeanza kuonyesha matunda yake na wapenzi wanatakiwa kusubiri ili kuona mafanikio makubwa zaidi.
"Huu ndio mwanzo wa Simba mpya. Na mengine mazuri yatafuata kwa msimu mzima, tunahitaji kucheza katika kiwango cha juu zaidi ya hiki tulichokionyesha, " alisema kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uganda.
SUNZU
Mshambuliaji Felix Sunzu kutoka Zambia ambaye alitengeneza bao la kwanza lililofungwa na Haruna Moshi ‘Boban’ na kufunga mwenyewe la pili, alisema kwamba amefurahi kuifungia timu yake hiyo mpya na anaamini kwamba watafanya vizuri kwenye ligi ya Bara.
Sunzu, Mzambia mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ambaye alitua Simba hivi karibuni akitokea El Hilal ya Sudan, alisema amedhamiria kuendeleza makali yake mbele ya lango la wapinzani ili mwishowe amalize akiwa mfungaji bora na kutwaa kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
KASEJA
Kipa na nahodha wa Simba, Juma Kaseja, alisema kuwa ushindi wa juzi umewafariji kwani walicheza vizuri na pia, walipata fursa ya kulipiza kisasi cha kufungwa na Yanga katika mechi yao ya hivi karibuni ya fainali ya Kombe la Kagame.
COSTA
Beki Victor Costa ‘Nyumba’ aliyerejea Simba msimu huu akitokea Msumbiji alikokuwa akicheza soka la kulipwa, alisema kuwa licha ya kufurahishwa na ushindi wao dhidi ya Yanga, anaamini kuwa hakuonyesha kiwango chake halisi na hivyo wana Simba wategemee mambo makubwa zaidi kutoka kwake
CANNAVARO
Beki wa kati wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema kuwa mechi hiyo ilikuwa kama ya mazoezi kwao kwa ajili ya msimu ujao na haamini kama matokeo yake yatawaathiri.
FABREGAS
Kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ alisema mechi ilikuwa ngumu lakini pia timu yake ya Yanga haikuwa na bahati ya kupata mabao.
NSAJIGWA
Nsajigwa alikiri kwamba wapinzani wao walikuwa na kasi zaidi kipindi cha kwanza na hivyo kuwapa wao wakati mgumu wa kukabiliana nao.
Aliongeza kuwa pamoja na kufungwa, bado timu yao ni nzuri na anaamini kuwa itafanya vizuri katika mechi za ligi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: