ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 19, 2011

Serikali yaiweka Ligi Kuu njia panda


Yafunga Uwanja wa Taifa, TFF yachanganyikiwa
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF), Angetile Osiah
Serikali imeiweka njia panda Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kutoa taarifa ya kustusha ya kuufunga mara moja Uwanja wa Taifa, ikiwa ni siku moja tu kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.
Klabu za Simba na Yanga zilizopaswa kuutumia Taifa kama uwanja wao wa nyumbani, sasa zimetakiwa kutafuta viwanja vingine vya nje ya jiji la Dar es Salaam baada ya uwanja waliokuwa wakiutumia awali wa Uhuru kufungwa pia.
“Kiukweli jambo hili limetuchanganya. Hatujui cha kufanya. Ni maamuzi yatakayotuathiri sana na hata ligi kwa ujumla,” alisema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF), Angetile Osiah wakati akizungumza na NIPASHE jana jioni.

Mapema jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa walipokea barua kutoka serikalini juzi ikieleza kwamba uwanja huo hautatumika tena ili kupisha matengenezo ambayo mwisho wake haukutajwa.
"Wizara imesema kuwa uwanja huo utakuwa katika matengenezo baada ya kuharibika wakati wa michuano ya Kombe la Kagame (klabu bingwa Afrika Mashariki) iliyofanyika mwanzoni mwa mwezi uliopita. Hivyo, kwa sasa wote waliokuwa wameomba kuutumia wanatakiwa kutafuta viwanja vingine," alisema Wambura.
Aliongeza kuwa tayari TFF jana iliziandikia barua ya kuzijulisha klabu za Simba na Yanga zinaozutumia uwanja huo kama wa nyumbani, na pia African Lyon, Azam, JKT Ruvu, Moro United na Villa Squad ambazo ziliomba kutumia uwanja huo kwa mechi zao dhidi ya Simba na Yanga.
Hatua hiyo iliyotokana na maamuzi yaliyofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo itaiathiri pia mechi ya Septemba 3 ya kuwania kufuzu fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN 2012) kati ya timu ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Algeria ambayo sasa, TFF imeihamishia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Timu nyingine (mbali na Simba na Yanga) zimekubaliwa kutumia uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam kwa mechi zao nyingine lakini zilitakiwa kutafuta viwanja vingine mikoani kwa ajili ya kuchezea pale zitakapokuwa wenyeji dhidi ya klabu za Simba na Yanga.
Yanga ambayo inaanzia nyumbani keshokutwa Jumapili, itatakiwa kufanya maamuzi ya haraka ili kuwakaribisha wageni wao JKT Ruvu wakati Simba itaanzia ugenini jijini Arusha kuivaa JKT Oljoro kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Osiah alisema hawajui hali itakuwaje pindi klabu iliyotakiwa kucheza na timu kama Yanga jijini Dar es Salaam itakapotakiwa kusafiri hadi Mwanza, kwa mfano, kucheza mechi hiyohiyo na kisha kwenda kucheza mkoa mwingine kabla ya kurejea tena Mwanza kucheza dhidi ya wenyeji waliokuwa wakifahamika kabla ya ligi kuanza, klabu ya Toto African ya mkoani humo.
Wakizungumza na NIPASHE jana, baadhi ya wadau wa soka nchini walisema kwamba hatua hiyo ya Serikali ni ya ghafla mno na hivyo itahatarisha mechi nyingi za ligi na hata ufanisi wa timu ya taifa.
Msemaji wa klabu ya Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisema uamuzi wa Serikali utaiweka njia panda ligi hiyo ambayo ratiba yake ilipangwa kwa kuzingatia kuwa Simba na Yanga zitacheza Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa Serikali inapaswa kutambua hali za klabu kiuchumi na kwamba, wakilazimika kufanya maamuzi ya ghafla kama hayo wanapaswa kutenga fungu la kugharimia matumizi ya klabu ya ziada ili kuokoa ligi kuu isisambaratike.
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kuwa wao bado hawajapata taarifa rasmi za kufungwa kwa uwanja huo, lakini alisema mabadiliko hayo yanaongeza mzigo wa gharama kwa klabu.
Kwa kawaida, TFF hupanga ratiba kwa kuzingatia jiografia ya eneo husika ambapo timu inayotoka mkoani kwenda kucheza na Simba jijini Dar, kwa mfano, hupangiwa pia kucheza na timu nyingine zinazocheza Dar au karibu na Dar kama Azam, Moro United, Yanga na Villa Squad.
Kutokana na kufungwa kwa uwanja wa Taifa, ni wazi kwamba utaratibu huo uliolenga kupunguza mzigo wa gharama kwa klabu utavurugika na kutishia ufanisi wa ligi hiyo inayoanza kesho.
Jitihada za gazeti hili jana kumpata Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Seith Kamuhanda ili azungumzie uamuzi huo wa kuufunga uwanja wa Taifa zilishindikana.
CHANZO: NIPASHE

No comments: