Advertisements

Saturday, September 10, 2011

KUZAMA KWA MELI YA SPICE ISLANDERS

Ndugu Watanzania mnaoishi Marekani na Mexico,

Napenda kuwataarifu kwamba, kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka nyumbani na kwenye vyombo mbalimbali vya habari ni kuwa Watu 620 wameokolewa wakiwa hai na watu wapatao 189 wamefariki dunia katika meli iliyozama ya Mv Spice Islanders iliyokuwa ikitokea Bandari ya Malindi Unguja kuelekea Bandari ya Wete Kisiwani Pemba. Huu ni msiba mkubwa uliolikumba Taifa letu kufuatia kuzama kwa meli hiyo katika mkondo wa Nungwi Kaskazini Unguja.

Kufuatia Maafa hayo Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia kesho tarehe 11 Septemba, 2011 na bendera kupepea nusu mlingoti. Aidha, Ubalozi utafungua kitabu cha maombolezo kwa Watanzania siku ya Alhamisi tarehe 15 Septemba, 2011 hadi siku ya Ijumaa tarehe 16 Septemba, 2011 kwenye Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania iliyopo 1232 22nd Street NW, Washington DC 20037, saa nne kamili asubuhi (10:00 a.m.) mpaka saa kumi kamili alasiri (4:00 p.m).

Tunawaombea majeruhi nafuu ya haraka. Aidha, tunaelewa machungu ya wafiwa kufuatia msiba huu mkubwa. Mwenyeezi Mungu awape subira, faraja na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi.

Tuzidi kumuomba Mwenyeezi Mungu aziweke mahali pema peponi roho za marehemu. Amin.


Mwanaidi Sinare Maajar (Balozi),
Ubalozi wa Tanzania,
Washington, D.C.

No comments: