Mbunge wa CCM atuhumu wafadhili wanamwaga fedha nchini
Jaji Mkuu Mstaafu Samatta asema Katiba ya sasa ya kidikteta
Slaa, Warioba, Salim wakutana faragha mdahalo wa katiba
Jaji Mkuu Mstaafu Samatta asema Katiba ya sasa ya kidikteta
Slaa, Warioba, Salim wakutana faragha mdahalo wa katiba
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, ameishutumu Ujerumani kwamba, imeiahidi Chadema na wanaharakati kwamba, itawapa fedha ikiwa watafanya fujo na kuvuruga mchakato wa katiba.
Lusinde alitoa madai hayo mazito wakati akichangia muswada huo bungeni jana asubuhi.
Hata hivyo, hakutoa uthibitisho wowote kuhusu tuhuma hizo dhidi ya Ujerumani, ambayo ni moja ya nchi washirika wa maendeleo wa Tanzania.
Alihoji kuwa watu hao (Chadema na wanaharakati) watapata wapi bajeti na uhalali wa kuendesha mchakato wa katiba.
Alipotakiwa na NIPASHE kueleza kama anao ushahidi juu ya madai hayo, Lusinde, alisema hayuko tayari kuzungumzia suala hilo nje ya Bunge kwani kama kungekuwa na shaka juu ya aliyoyasema angeombewa mwongozo palepale bungeni.
Juhudi za kumpata Balozi wa Ujerumani kuzungumzia madai hayo, ziligonga ukuta, baada ya kuelezwa na maofisa wa ubalozi huo kuwa muda wa kuzungumza naye ulikuwa umekwisha.
CHADEMA WAMPUUZA
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mnyika, amesema madai yaliyotolewa na Lusinde ni kisingizio cha serikali na chama chake kuwanyima wananchi wengi fursa ya kuchangia maoni yao katika muswada wa katiba.
Aliongeza kuwa Chadema ilipoliweka suala la katiba mpya katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka jana, hakuna aliyetoa madai kuwa inapewa fedha na nchi za nje na kusisitiza kuwa madai ya Lusinde hayana msingi wowote.
Samatta na udikteta wa katiba
Jijini Dar es Saalam joto la katiba mpya limeendelea kuongezeka baada ya kufunguliwa kwa mdahalo wa nafasi na umuhimu wa katiba katika maisha ya Watanzania, uliofunguliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, jijini Dar es Salaam jana.
Jijini Dar es Saalam joto la katiba mpya limeendelea kuongezeka baada ya kufunguliwa kwa mdahalo wa nafasi na umuhimu wa katiba katika maisha ya Watanzania, uliofunguliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, jijini Dar es Salaam jana.
Katika mdahalo huo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kuhudhuriwa na viongozi mashuhuri wastaafu, wakiwamo, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Jaji Joseph Warioba na Dk. Salim Ahamed Salim, Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta, alizungumzia udhaifu wa katiba ya sasa na kusema ni ya kidikteta.
Jaji Samatta alisema katiba hiyo inalazimisha Spika wa Bunge atokane na vyama vya siasa hali ambayo inamfanya akose uhuru wa kutekeleza majukumu yake kwa kuwa atalazimika kuikisaidia chama chake.
“Kama mimi ningekuwa natunga Katiba Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asingetokana na chama chochote cha siasa ili kumpa fursa ya kufanya kazi bila kuangalia chama anachotoka,” alisema
Alisema kuna nchi kadhaa duniani ambazo Spika wake hatokani na chama chochote cha siasa, lakini bado Bunge linakuwa na nguvu na kufanya kazi zake vizuri. Alifafanua kuwa athari za Spika kutokana na chama ni pamoja na kutekeleza maagizo na maelekezo ya chama kilichomfikisha katika kiti hicho na kwamba Katiba mpya ijayo inapaswa kuangalia vitu kama hivyo.
Aidha, Samatta alisema suala la tume ya uchaguzi kuwa idara ya serikali nao ni udhaifu wa katiba kwani inashindwa kuwa huru.
Pia alisema Rais kuwa sehemu ya bunge ni udhaifu mwingine wa katiba ya sasa na kusema kimsingi katiba hiyo inaruhusu udikteta wa wengi dhidi ya wachache.
Alisema Katiba ya sasa ni ya kidikteta kwa kuwa inashindwa kuweka wazi haki mbalimbali za wananchi zikiwemo za kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa bila kupitia kwenye vyama.
Kuhusu malumbano yanayohusiana na muswada wa kuunda tume ya kuratibu maoni ya kuandika katiba mpya yanayoendelea hivi sasa hapa nchini, Samatta, alitaka maoni ya wananchi yaheshimiwe na yawe ndiyo ya mwisho.
“Maoni ya wananchi lazima yawe ndiyo ya mwisho ili hatimaye Katiba nzuri ambayo inakubalika na pande zote iweze kuandikwa,” alisema Samatta.
Naye Dk. Salim ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere alitaka vyama vyote vya siasa wakati vikijadili muswada wa katiba vifikirie kwanza na kuweka mbele maslahi ya nchi.
Alisema vyama vya siasa lazima vijue katiba mpya ni kwa faida ya Watanzania wenyewe na sio kwa ajili ya vyama.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema vyombo vyote vya dola vipo chini ya katiba, lakini kwa hali ilivyo imekuwa kinyume chake.
Alisema Rais Jakaya Kikwete anataka kujitengenezea katiba yake mwenyewe jambo ambalo sio sahihi na badala yake wananchi waachiwe waamue wenyewe wanataka ya namna gani.
Akifungua mdahalo huo, Makamu wa Rais Dk. Bilal, aliwataka Watanzania kutogombana wakati wa kujadili muswada wa kuunda tume ya kuratibu maoni ya kuandika katiba mpya.
Aliwataka wananchi kutobaguana kwa misingi ya dini, ukabila na rangi, badala yake wawe na dhamira ya kweli ya kuendeleza umoja wao na mshikamano.
Katika eneo la mdahalo, Dk. Salim na Jaji Warioba walifanya mazungumzo ya faragha na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa.
Haikuweza kujulikana mara moja viongozi hao walizungumza nini, lakini picha zilizopigwa zinaonyesha wakiwa katika mazungumzo ya kina. Dk. Slaa alipoulizwa na NIPASHE walizungumzia nini hasa, alilitaka gazeti hili kuwasiliana na viongozi hao wastaafu.
CHADEMA: MUSWADA USIPITISHWE LEO
Chadema imemuomba Spika Makinda leo azuie Bunge lisipitishe muswada wa katiba kwa kuwa umekosa uhalali.
Mnyika aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Spika anaweza kuzuia Bunge kukaa kama kamati kupitisha muswada kwa kutumia kanuni za Bunge namba 86(3) a na b, 87 na 90 ambayo inamruhusu mtoa hoja kuiondoa hoja yake.
Alisema kuruhusu muswada huo kupitishwa, kutasababisha kuwapo na michakato mingi ya katiba, ambayo itafanywa na makundi na taasisi mbalimbali. Muswada huo wenye lengo la kuweka utaratibu wa kuundwa kwa Tume ya Katiba, ulisomwa kwa mara ya pili bungeni Jumatatu wiki hii na Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani na kujadiliwa hadi jana mchana.
Wabunge wataupitisha baada ya kipindi cha maswali na majibu, baada ya Waziri Kombani kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge.
Hata hivyo, mjadala wa muswada huo ulidorora, baada ya wabunge wa Chadema na wawili wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila (Kigoma Kusini) na Felix Mkosamali (Muhambwe) kuususa.
Wabunge hao walisusa kutokana na kunyimwa fursa ya kupewa mwongozo na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kabla na wakati wa kusomwa kwa muswada huo.
Hoja, ambazo zilitarajiwa kuwasilishwa na wabunge hao, John Shibuda (Maswa Magharibi-Chadema); John Mnyika (Ubungo-Chadema) na Felix Mkosamali (Muhambwe-NCCR-Mageuzi), ni kutaka muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza ili wananchi wengi wapate fursa ya kuuchangia.
Wabunge hao waliungana na wanaharakati, ambao pia walitaka muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza kutokana na kufanyiwa marekebisho makubwa, baada ya kuondolewa bungeni Aprili 5, mwaka huu.
Wachangiaji wote wa vyama vya CCM na CUF walitumia muda mrefu kuilaani Chadema na wanaharakati kwa madai kuwa wanapotosha wananchi.
NCCR-MAGEUZI KUZUNGUKA NCHI NZIMA KUPINGA MUSWADA
Katika hatua nyingine, Chama cha NCCR-Mageuzi, kimepinga muswada huo na kimesema kitaanza mikutano nchi nzima inayolenga kutoa ujumbe kwa Watanzania waanze mchakato wa kuandaa Katiba Mpya waitakayo.
Mwenyekiti wa wabunge wa chama hicho, David Kafulila, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa walifikia uamuzi huo katika kikao cha sekretarieti ya halmashauri kuu ya chama chake ambapo wataanza mikutano hiyo keshokutwa (Jumapili) jijini Dar es Salaam.
Alisema walikubaliana kuwa mchakato wa kujadili katiba mpya lazima uanze kwa kusomwa kwa mara ya kwanza kwa sababu msingi wa kutafsiri katika lugha ya Kiswahili ni kuishirikisha jamii.
“Tungependa umma uelewe kuwa tunapotaka kusomwa kwa mara ya kwanza nikutaka wananchi waweze kujadili muswada huu,” alisema Kafulila.
Alisema kusomwa kwa mara ya pili kunaondoa mantiki ya muswada huo kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
“Bado ni wito wetu kwa Rais kwamba suala hili ni la kitaifa haliwezi kuwa la kiitikadi na kwamba uamuzi wowote na jinsi mambo yanavyoendelea ndani ya Bunge ya kuendesha jambo hili katika misingi ya itikadi inaondoa uhalali wa jambo lenyewe wa mchakato wenyewe,” alisema.
Alitoa wito kwa serikali kutafakari upya muafaka kati yao (wabunge wa NCCR-Mageuzi na Chadema, vyama vyote vya siasa vilivyopo ndani ya Bunge, ili mchakato wa katiba uweze kwenda vizuri.
“Ni wito wetu wabunge wa chama tawala na wabunge wengine watazame jambo hili kwa mapana, kwamba linagusa wananchi wote na sio vita wala ushindani wa chama na chama kwa hiyo ni jambo linalohusu Watanzania na si jambo linalohusu Chadema na NCCR-Mageuzi,” alisema Kafulila.
Alisema mjadala wa muswada huo unavyoendeshwa na chama kimoja, ni ushahidi wa kutosha kwamba jambo hilo linapoteza uhalali wake.
“Vikao vya Bunge vinabeba sura ya Kamati Kuu ama Halmashauri Kuu (ya CCM) kuliko sura yake ambayo ni Bunge la Tanzania,” alisema Kafulila ambaye ni mbunge wa Kigoma Kusini.
Kafulila aliyeongozana na Mkosamali na Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alisema kama muafaka hautafikiwa wa namna ya kuendesha suala la mchakato wa katiba mpya, ambayo itawafanya Watanzania kukubaliana, NCCR- Mageuzi iko tayari kuwashawishi wadau wengine wa katiba na demokrasia walioko katika medani za kisiasa na nje kutengeneza njia nyingine ya kushughulikia.
Alisema watatengeneza njia mbadala ya kufikia katiba mpya na kwamba watawashawishi wadau wengine waanze mchakato ambao utaenda sambamba na mchakato wa serikali ili waweze kuwafikisha Watanzania katika katiba wanayoitaka.
“Ni kwa sura hiyo kama serikali haitasikiliza na kufikia muafaka huo umma utapiga kura ya kutokuwa na imani na katiba ambayo inapendekezwa katika mchakato huu,”alisema.
Alisema wataanza kazi ya kutuma ujumbe kwa Watanzania kuanza mchakato wa katiba mbadala hiyo baadala ya Bunge.
Kafulila alisema wataanza kazi hiyo mkoa wa Dar es Salaam na kwamba mchakato huo utakwenda sambamba na mchakato wa serikali wa kuandaa katiba mpya.
“Tutaanza na Dar es Salaam siku ya Jumapili kwa kuandaa mikutano ya kutoa ujumbe wa kuwataka Watanzania tutengeneze mchakato mwingine sambamba na huu serikali unaufanya sambamba na mingine,” alisema.
Wabunge hao na wa Chadema wamesusia mijadala ya muswada huo unaotarajiwa kuhitimisha leo.
HATIMA YA JAIRO LEO
Wakati huo huo, Bunge leo litapokea taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa na Spika Makinda kuchunguza tuhuma dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, David Jairo.
Jairo anadaiwa kuchangisha fedha kutoka taasisi zilizoko chini ya wizara yake kwa ajili ya kushawishi wabunge wapitishe bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha.
Kamati hiyo ambayo iliongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM). Wajumbe wengine wa kamati hiyo, ni Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM); Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema) na Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF).
Ilichunguza kuingiliwa kwa madaraka ya Bunge, baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kumsafisha Jairo nje ya Bunge, ambako ndiko tuhuma hizo zilipoibuliwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment