Licha ya kuzuiwa na polisi, Umoja wa Wazanzibari (Zarfa), umesema utaendelea na maandamano ya amani yaliyopangwa kufanyika leo kupinga uhalali wa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar.
Kiongozi wa umoja huo, Rashid Salum Adiy, alisema mjini hapa jana kuwa maandamano hayo yatafanyika leo kama yalivyopangwa.
Alisema maandamano hayo yataanzia viwanja vya Kombawapya kuanzia saa mchana na yatapitia maeneo ya Msikiti Mabuluu, Mlandege na kumalizikia viwanja vya Masiara Suleiman.
Alisema Wazanzibari kwa ujumla wao wameamua kuendelea na mandamano hayo kwa sababu hawajaridhika na maelezo na sababu za polisi kuzuia maandamano hayo.
Alisema lengo la maandamano hayo ni kuwaelezea wananchi nia ya Zanzibar kupigania haki ya uhuru na mamlaka ya Zanzibar, kitaifa na kimataifa.
Adiy alisema Wazanzibari wanapinga Muungano uliopo kwa sababu haukuanzishwa kisheria na pia hauna hati za makubalino, matokeo yake umesababisha sehemu hizo mbili kuungana kisiasa tu.
"Suala la kudai haki hii limeanzia mbali na kwa utaratibu wa kufika hata mahakamani, kumtaka Mwanasheria Mkuu kuonyesha mkataba wa Muungano, ambaye alikiri kuwa haupo,” alisema Adiy.
Alisema hatua ya Wazanzibari kuungana chini ya umoja huo kudai muungano wa kisheria haiendeshwi kwa misingi ya kisiasa kwa sababu umoja wao sio taasisi ya kisiasa.
Lakini katika barua ya Novemba 17, mwaka huu, yenye kumbukumbu Na. W/MGH/55/192 ya kuzuia mandamano hayo, Polisi imehoji uhalali wa umoja huo na kwamba kero za Muungano zina taratibu zake za kujadiliwa wala sio kwa maandamano na pia kwamba yatasababisha uvunjifu wa amani.
“Hatuna lengo la kufanya fujo na ni watu tuko kisheria, polisi wangelituomba tulete majina yetu, na sio kukurupuka kuzuia maandamano kwa kutoa visingizio visivyo vya msingi,” alisema Adiy.
Adiy aliongeza kuwa anatarajia wananchi wengi watashiriki katika maandamano hayo kwa njia ya amani na ameomba polisi watoe ushirikiano.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment