ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 18, 2011

Unatarajia nini kutoka kwa mume/ mke wako mtarajiwa?-2

NATAMANI sana kuona maisha ya vijana wa sasa yakiwa hayana migogoro, hasa ya mapenzi. Ni furaha yangu kuona vijana wakifanikiwa katika kazi zao na maisha yao kwa ujumla. Rafiki zangu, maisha bora au utaratibu mzuri wa maisha unatokana na uhusiano mwema wa mhusika na mwenzake.

Kama ulikuwa hujui, leo chukua hii elimu, kijana/mtu ambaye amegombana na mpenzi wake usiku uliopita, sikuyake huwa nzito sana kazini. Kila anachokifanya hukumbuka ugomvi wa usiku.


Kama mtu ataondoka nyumbani akiwa hana maelewano na familia yake, ni wazi kwamba siku yake itatawaliwa na giza. Hata kama atajitahidi kuficha, lakini itafikia mahali atashindwa. Kazi inahitaji utulivu.

Ndivyo ilivyo katika maisha, lazima upate mwenzi sahihi ambaye atakupa furaha badala ya mateso. Hapa ndipo tunapojadili jambo moja kubwa na muhimu sana; amani na furaha ya ndoa.

Je, wewe unatarajia nini kwenye ndoa yako ijayo? Unahitaji mafanikio au kuvurunda kila siku kwenye biashara zako? Kama unataka kuwa bora, lazima pia uwe na mwenzi sahihi. Rafiki zangu wengi wanajiandaa kwa mazuri tu kwenye ndoa zao.
Hawana mpango na changamoto na migogoro, hapo watakuwa wanakosea sana.

Kama mnakumbuka vizuri, wiki iliyopita nilieleza kwanza sababu za kujadili mada hii, namna ambavyo baadhi ya watu wanawaza na tatizo lilipo, ambapo imeonekana wengi wanaishi na wapenzi wao kabla ya ndoa, maisha ya kuigiza tu! Yaani anaonesha tabia za ‘kupaka rangi’ lakini akishaingia ndani anabadilika.

Kitu kikubwa ambacho nilikifafanua wiki iliyopita ni tabia ya kuishi maisha yako halisi bila kuigiza. Kufanya hivyo kutampa nafasi mpenzi wako naye aishi maisha yake ya kawaida, mwisho kila mmoja atamjua mwenzake.
Nini kingine zaidi ya hayo? Tuendelee na somo letu...

KEMEA MAPEMA MATATIZO
Katika kuishi kwako maisha yako halisi, mwenzako naye atakuwa kama wewe. Hiyo ni hatua nzuri maana itakuwa rahisi sana kwako kugundua tabia za mwenzako. Hapo utazijua nzuri na mbaya.

Acha kulea matatizo, bila kujali jinsi, mwambie mpenzi wako tabia ambazo hazikufurahishi. Ili aweze kubadilika kwa urahisi zaidi, unatakiwa kumwambia kwa utaratibu, lakini pia umpe sababu za wewe kukataa tabia zake hizo.

Akiendelea nazo kuwa mkali, wakati mwingine ukali unasaidia. Kwa kukemea, kama ni kweli anakupenda na anahitaji uhusiano wenu uendelee, basi lazima atabadilika. Akifanya hivyo itakuwa vizuri zaidi kwako, maana utakuwa na uhakika angalau kwa asilimia chache kwamba mpenzi wako anakusikiliza.

TABIA ZA ASILI
Rafiki zangu, lazima ufahamu kwamba wakati unapambana na tabia za mpenzi wako zisizokupendeza, zipo tabia nyingine ni za asili. Hazibadiliki. Sasa hapo lazima uwe makini kwa mambo mawili; Mosi, zitakuathiri?

Pili, ni tabia zitakazokugombanisha na jamii? Maana kuna tabia nyingine zinavumilika, lakini je, hazitaleta athari kwa majirani zenu watarajiwa? Haya ni mambo ya kuyatafakari kabla ya kuingia kwenye ndoa.

Mathalani, kuna baadhi ya watu wana viburi au dharau za kuzaliwa! Hata umfanyeje, habadiliki. Unaweza kumwuliza kitu akanyamaza. Ni tabia ya kiburi, lakini kwa sababu amezaliwa akiwa na tabia hiyo, hawezi kuiacha. Sasa hapo lazima ujiulize, utawezana naye?
Utaweza kumvumilia na kiburi chake kwa maisha yenu yote? Huu ni mfano tu rafiki zangu, zipo tabia nyingi za asili, ambazo kwa nafasi yako unaweza kuzichunguza kwa mpenzi wako kabla ya kuchukua uamuzi mzito wa kuingia kwenye ndoa. 

KUWA MKWELI
Ukweli ni silaha, ni haki na siku zote humfanya mtu awe huru. Kama kuna jambo ambalo hujalipenda kwa mpenzi wako, haraka mwambie. Acha kukaa na vitu moyoni. Si utaratibu mzuri.

Hata kama nguo zake hazikufurahishi mwambie: “Baby yaani kiukweli ukivaa hizo jeans zako hupendezi kabisa. Nadhani uanze kuvaa suruali za vitambaa.”

Hapo utakuwa umemwambia ukweli wako, kukubaliana na wewe au kukataa kutatokana na mapenzi yenu wewe na yeye. Kama anakupenda atakusikiliza. Kwani anamfurahisha nani huko barabarani zaidi yako? Kuwa mkweli.

UTARATIBU WA KAZI
Suala la kazi kwa baadhi ya wanandoa huwa ni tatizo. Utakuta mwanaume amemkuta binti wa watu anafanya kazi, wamependana na kufunga ndoa. Ghafla anamwambia mwenzake aache kazi! 

Ndoa nyingi hasa changa huingia kwenye mgogoro huu. Kwangu mimi, wanandoa wote kufanya kazi ni bora zaidi, maana ile maana ya usaidizi wa mwanamke inakuwa imekamilika. Kwa maisha ya sasa mama kukaa nyumbani siyo ‘dili’ tena.

Hata hivyo, ili kuepusha matatizo, suala hili ni vyema mkajadiliana mapema. Kaa na mwenzako, mwulize: “Lakini dady, vipi kuhusu kazi baada ya kufunga ndoa?”

Anzisha huu mjadala na mwisho muwe na majibu yenye usawa. Mkubaliane kwa pamoja. Vijana wa mtaani wanasema, ‘kwa roho safi’. Hii itakusaidia maana mgogoro huu utakuwa umeisha kabla hata ya ndoa yenu.

Nimeandika sana, lakini mambo ya kujadiliana bado hayajaisha ila nafasi yangu imeishia hapa. Hadi wiki ijayo rafiki yangu, nitahitimisha mada hii, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.

No comments: