ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 3, 2012

Tunaweza kuifuta CHADEMA *Wassira awaonya kutovuruga amani nchini


Na Raphael Okello, Bunda

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira, amesema Serikali ina uwezo wa kumuomba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa ili akifute Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kama kitaendeleza siasa za kuvuruga amani ya nchi.

Alisema Watanzania walikubali mfumo wa vyama vingi kwa nia njema ya kuleta demokrasia ya uhuru wa kutoa maoni na kulumbana kwa hoja bila kuvuruga amani, utulivu au kufanya uchochezi.


“Katiba ya nchi inatoa haki kwa vyama vyote vya siasa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kwa kuzingatia taratibu na sheria ya nchi badala ya kujiamulia na kufanya fujo,” alisema.

Aliongeza kuwa, uhuru wowote una mipaka yake kwani sheria hairuhusu kila mtu, kikundi cha watu au chama chochote kufanya wanavyoona inafaa na kutoa shutuma za kichochezi.

“Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa, Seriokali ina uwezo wa kuipa CHADEMA kadi ya njano na kama itaendelea kucheza rafu uwanjani, itapewa nyekundu.

“Sisi tulipewa dhamana na wananchi ili kulinda amani, utulivu na
mshikamano wa Taifa, hatupo tayari kuvumilia vitendo visivyokoma vya kuvuruga amani na utulivu....tunaiomba CHADEMA waheshimu sheria ya mchezo vyama vingi,” alisema.


Bw. Wassira ambaye anafanya ziara ya kutembelea wapiga kura jimboni kwake, aliyasema hayo wakati akijibu maswali ya wakazi wa Kijiji cha Bukama, Kata ya Nyamuswa, wilayani Bunda.

Wakazi hao walitaka kujua Serikali kama walizni wa amani na utulivu wa nchi inaonaje mwenendo wa CHADEMA ambapo swali hilo liliulizwa na Bw. Samwel Msika, mkazi wa Kijiji cha Bukama.

“Wewe Bw. Wassira ni miongoni mwa viongozi Serikalini, hivi sasa umesema Serikali inahimiza amani, mshikamano na utulivu wa nchi, je mwenendo wa CHADEMA kufanya fujo mnauonaje ni salama, mmeukubali, mnauunga mkono au mnauzungumziaje,” alihoji.

Wakazi wengine wa kijiji hicho, walimtaka Bw. Wassira kutoa ufafanuzi juu ya kanuni za Bunge kama zinatoa fursa kwa wabunge kutoa maneno ya kashfa kwa kiongozi wa nchi.

Walidai ni hatua zipi ambazo zinachukuliwa kwa baadhi ya wabunge wanaotoa maneno hayo kwani wapo baadhi yao ambao hivi karibuni walifanya hivyo bungeni mjini Dodoma.

“Tunataka kujua msimamo wa Serikali na hatua zinazochukuliwa kwa baadhi wa viongozi serikalini pamoja na wabunge ambao hivi karibuni walidaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuficha fedha za umma nje ya nchi,” alisema.

Akijibu hoja hizo, Bw. Wassira alisema pamoja na mambo mengine, kanuni na miongozo ya Bunge inakataza wabunge kutoa kauli za kashfa dhidi ya Rais na mbunge anayefanya hivyo, anachukuliwa hatua na Kamati ya Maadili ya Bunge.

Alisema zipo taratibu za kujadili utendaji wa Rais bungeni kwa Spika kupelekewa hoja badala ya kutoa maneno ya kashfa. Kuhusu mafisadi alisema uchunguzi unaendelea na wote ambao ushahidi wao utapatikana watashtakiwa.

Aliongeza kuwa, Serikali imekuwa ikichukua hatua ambapo hadi sasa, wapo baadhi ya Mawaziri ambao wamefikishwa mahakamani akiwataja Bw. Daniel Yona na Bw. Bazir Mramba na kuhadharisha wananchi kutofanyia kazi uzushi na chuki binafsi za wanasiasa.

Majira

5 comments:

Anonymous said...

Hizo pesa zilizofichwa nje ya nchi mbona wassira hakuzitolea maelezo? anachojua ni kutishia kuifuta chadema. Kwanini CCM isifutwe kama hiyo ni case? kwa kuwa wanaua wananchi na pia ni mafisadi? CCM wakiona wanakaribia kushindwa wanaanza kuua demokrasia.

Unknown said...

hii habari ya muda kidogo

Aliweiwei Machibya said...

Wasira acha vituko huenda unazeeka vibaya , Msajili wa Vyama akithubutu kuchukua hii nchi itaenda pabaya zaidi ya hapa ilipo. ninawaza kwa sauti kuuu.

Anonymous said...

We mzee unazeeka vibaya.....andaa funeral yako waache chadema kabisaa.

Anonymous said...

mwache Hafute chadema itatokea kama RWANDA !!!!!!!!