Balozi Mwanaidi Maajar ( wapili toka kulia) akiongea jambo na Watanzania Iowa Bwn. Singo (kulia) na Godlisen (kushoto) waliokutana naye kwenye Chuo Kikuu cha Des Moines Jimboni Iowa kabla ya kuanza Mkutano wa Iowa - Tanzania
mjini Des Moines tarehe 16 Oktoba, 2012, wa pili toka kushoto ni Afisa Habari wa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Mindi Kasiga.
Balozi Mwanaidi Maajar na baadhi yaWatanzania Bwn.Singo ( wapili toka kushoto) na Godlisen ( wakwanza kushoto) waliokutana naye kwenye Chuo Kikuu cha Des Moines Jimboni Iowa kabla ya kuanza Mkutano wa Iowa - Tanzania
mjini Des Moines tarehe 16 Oktoba, 2012.
Balozi Mwanaidi Maajar akisalimiana naDkt. Allan Hoffman, Rais Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Santa Barbara, Carlifornia ambaye naye alijumuika na Watanzania kwenye mazungumzo
hayo na Balozi Maajar kabla ya Mkutano wa Iowa - Tanzania kuanza
Rais wa Taasisi isiyo ya Kiserikaliijulikanayo kama Empower Tanzania Bw. Phil Latesa akizungumza na Dkt. Allan Hoffman na Bw. Singo baada ya mkutano na Balozi Maaar (hayupo
pichani).
Balozi Mwanaidi Maajar akisalimiana naWatanzania waishio Des Moines Iowa.
Afisa Mindi Kasiga katika picha ya pamoja na Balozi Mwanaidi Maajar
Bwn.Singo akipiga picha na Balozi Mwanaidi Maajar
Des Moines, Iowa
BALOZI wa Tanzania nchini
Marekani na Mexico Mhe. Mwanaidi Sinare Maajar amewaasa Watanzania waishio
Jimbo la Iowa mjini Des Moines kujitokeza na kutoa maoni yao kuhusu suala la
uraia wa nchi mbili kwenye mchakato wa mabadiliko ya katiba unaoendelea nchini.
Balozi aliyasema hayo
alipokutana na Watanzania hao kabla ya kuhudhuria Mkutano wa II wa Iowa –
Tanzania pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Chakula ujulikanao kama World Food Prize
unaoendelea mjini Des Moines, Iowa.
Alitoa mfano wa kwake binafsi
alipokuwa mwanasheria na mwanaharakati ambapo kupitia taasisi mbalimbali
walifanikiwa kushawishi na hatimaye kubadilisha sheria zilizowabana wanawake
kuwa na haki sawa na wanaume nchini Tanzania.
“Hakuna ushawishi mzuri
kama ule unaotoka kwenu nyie wenyewe Wana Diaspora, kwani nyie ndio mliovaa
kiatu cha uraia wa nchi mbili na mnajua kinabana wapi” alisisitiza Balozi na
kuwaomba wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao sasa wakati muda unaruhusu
kufanya hivyo.
Aliongeza kuwa Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amethibitisha ugumu uliopo kwa wajumbe wa tume hiyo
kusafiri nje ya nchi kukusanya maoni, hivyo aliwataka Watanzania waishio nje ya
nchi watembelee tovuti ya mabadiliko ya katiba na kutoa maoni yao http://www.katiba.go.tz
Sambamba na kutoa maoni,
Mhe. Maajar aliwaasa Watanzania wa Des Moines kujipanga ili kuunda umoja wa
Watanzania ili waweze kushughulikia masuala yanayowahusu kwa pamoja. Alisema
Marekani ni nchi kubwa na Watanzania waishio majimbo mengine wameitikia wito
huo na sasa kuna Jumuiya za Watanzania kwenye majimbo mengi nchini Marekani.
“Kwenye jimbo hili, ni
muhimu sana kuwa na Jumuiya madhubuti ili kutumia fursa hii inayojitokeza kila
mwaka ya Mkutano wa World Food Prize, kukutana na viongozi wanaokuja kutoka
nyumbani au hata sisi kutoka ubalozini” alihimiza.
Kwa upande wao, Watanzania
waishio mjini hapa walimshukuru Balozi Maajar kwa kukutana nao na kuahidi
kutekeleza yale yaliyoongelewa. Pia walipendekeza ubalozi wa Tanzania
Washington D.C. ujaribu kuboresha njia za mawasiliano ya kisasa kama vile
Facebook na Tweeter ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi ambao kutokana na
kubanwa na kazi, hawapati nafasi ya kutembelea tovuti ya ubalozi.
Mhe. Balozi yupo mjini Des
Moines, IA kwa siku mbili ambapo baadaye leo atahutubia Mkutano wa II wa Iowa –
Tanzania kama mgeni rasmi ulioandaliwa na Empower Tanzania, Taasisi isiyo ya
Kiserikali yenye makao makuu yake hapa Des Moines, Iowa. Kesho tarehe 17 Oktoba
2012, ataendesha mjadala wa Kukata Njaa kabla ya kuhudhuria ufunguzi rasmi wa
Mkutano huu wa World Food Prize.
Mindi Kasiga
Minister Counselor, Embassy of Tanzania Washington DC
Oktoba 16, 2012







No comments:
Post a Comment