Advertisements

Wednesday, January 30, 2013

WABUNGE WALIO CHOMEWA NYUMBA ZAO HUKO MTWARA WAANGUA KILIO

WABUNGE waliochomewa nyumba na mali zao katika vurugu zilizotokea Mtwara juzi; Anna Abdallah na Mariam Kasembe, jana waliangulia vilio walipotakiwa na mwananchi kuzungumzia tukio hilo.
Nyumba za wabunge hao wa Viti Maalumu na mali zingine kadhaa za taasisi mbalimbali, ni miongoni mwa vitu vilivyoharibiwa katika vurugu hizo ambazo pia zilisababisha vifo vya watu wanne wilayani Masasi.

Akizungumza kwa huzuni, Anna alisema hajui sababu za uharibifu huo, hasa ikizingatiwa mwenyewe amekuwa huko kwa karibu siku tatu na hakuona dalili za uhasama wowote dhidi yake.

Anna ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho alisema: “Nina siku ya tatu hapa Masasi na nimeshiriki mkutano wa halmashauri kwa mwaliko na wakati wote, sikuhisi chochote hivyo siwezi kujua sababu ya chuki iliyofanya nyumba yangu ichomwe moto,” alisema.

Alipotakiwa aeleze hali ilivyokuwa, alisema, “Wavamizi hao walipora kila kitu nyumbani kwangu yakiwamo mapazia, kabla ya kumwaga petroli kila chumba na kuwasha moto.”

Aliendelea kueleza,” Kila kitu kiliteketea. Inatia uchungu kwani nyumba hiyo niliijenga kwa kudunduliza fedha kidogo kidogo nikiwa mkuu wa mkoa.”

Anna alisema, kundi hilo la vijana lilivamia nyumbani kwake saa 4:00 asubuhi na kuanza kupora mali kwa kupita chumba kimoja baada ya kingine.

“Hali si nzuri. Kila kitu kimeibwa na nyumba imechomwa moto, hakuna kilichobaki. Walichukua kila kitu na itanichukua muda mwingi kujua thamani halisi ya hasara iliyopatikana,” alisema.

Kauli ya Kasembe
Naye Kasembe alipokea simu ya mwandishi wa habari hii kwa kilio na kuikata huku akisema, “Jamani niacheni… Mwenzenu naumia…!”

Alipopigiwa tena baadaye, alisema anashangazwa na tukio hilo ambalo limemfika bila kutarajia na kumtia hasara kubwa.

“Wamepora kila kitu katika nyumba na kuichoma moto, sijui atakuwa nani huyu, kwani sina tatizo na wapiga kura wangu na sina mgogoro na mtu yeyote. Nashindwa hata kuhisi nani kafanya uchochezi,” alisema Kasembe.

Alisema wakati wa vurugu hizo, ndugu zake akiwamo mama yake, walikimbia na kwenda kujihifadhi hotelini, lakini mpaka sasa hawajui wataishi vipi baada ya nyumba hiyo kuteketezwa kwa moto.

“Jana wanafamilia walilala hotelini na leo tupo nje ya gofu la nyumba yangu ambayo imeteketea kabisa kwa moto, tunasubiri majaaliwa mengine, lakini nimechanganyikiwa kwa kweli na sijui ni kitu gani hiki, siamini,”alisema.

Polisi waeleza uharibifu
Watu 44 wanashikiliwa na polisi wilayani Masasi kufuatia vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Maria Mzuki alisema watu hao wamekamatwa kwa wakituhumiwa kujihusisha na vurugu hizo zilizosababisha uhalibifu mkubwa mali.


Polisi wakati wa fujo za Mtwara.

Taarifa ikufikie kwamba Waziri mkuu Mizengo Pinda amefanikiwa kutuliza jazba za wakazi wa Mkoa wa Mtwara kwa kuwaeleza kuwa kiwanda cha kusindika gesi ghafi kitajengwa kijijini Madimba mkoani humo ili mabaki yatokanayo na gesi hiyo yatumike kuvutia uwekezaji wa viwanda, hii ikiwa ni kauli tofauti na ya madai ya wakazi hao ambao hasira zao zilichangiwa na taarifa kwamba kiwanda hicho kingejengwa Dar es salaam.

Kwenye mkutano wa majumuisho uliofanyika january 29 2013 Waziri mkuu baada ya kusikiliza madai ya wananchi hao kwa siku mbili mfululizo, amesema hakuna tone la gesi ghafi itakayosafirishwa kwa njia ya bomba.

Namkariri akisema “Imani yangu ni kwamba maelezo yametosheleza, mtakua na kiwanda chenu cha kusindika, mtakua na kiwanda cha kusafisha, mtakua na hayo matawi kadhaa kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kwa ajili ya usindikaji wa viwanda”

Mwanzoni madai ya wakazi wa Mtwara yalikua ni kupinga usafirishaji wa gesi ghafi mpaka Dar es salaam wakieleza kwamba huo mpango utafukuza wawekezaji wa viwanda Mtwara ambao ungechochewa na upatikanaji wa malighafi baada ya kusafishwa kwa gesi.

Jengo la Mahakama lililotelekezwa.

Pia wananchi walipinga ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kinyerezi Dar es salaam na badala yake wakataka hiyo mitambo ijengwe hukohuko Mtwara.

Kwenye mstari mwingine Waziri Mkuu aliwataka wananchi kumsamehe mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali mstaafu Joseph Simbakalia kwa kauli alizotoa december 21 2012 katika kikao cha kamati ya ushauri pale alipoombwa kuyapokea maandamano ya wakazi wa mkoa huo december 27 ambapo aliwaita wapuuzi na wahaini.

Waziri mkuu katika majumuisho yake aliambatana na Waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya kazi profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Uchukuzi Dr. Harrison Mwakyembe, Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi Dr. Shukuru Kawambwa na Waziri wa mambo ya ndani Dr. Emmanuel Nchimbi.

Katika hizo siku mbili pia Waziri mkuu alikutana na vyama vya siasa vya upinzani, chama cha Mapinduzi CCM, viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo, Wafanyabiashara, Madiwani na wenyeviti wa mitaa pamoja na Wanaharakati.

No comments: