Anayedaiwa kupiga video iliyosababisha kukamatwa kwa Rwakatale ( pichani ) maarufu kwa jina la Ludovik Joseph amekamatwa mkoani Iringa .kijana huyo anadaiwa kuwa ni mhitimu wa chuo kikuu cha DUCE
Ndugu zangu,
Usiku huu nikiwa kwenye shughuli ya shule ya watoto wangu pale Highlands Hall Iringa nilifikiwa na habari kuwa Kijana Ludovick amekamatwa na polisi kuhusiana na tuhuma za kuhusika na kuteswa mwandishi Absalom Kibanda.
Namfahamu kijana Ludovik tangu akiwa Chuo Kikuu ( DUCE). Ni mmoja wa Watanzania wengi walionifahamu kupitia kazi zangu za magazetini.
Kwangu Ludovick ni kijana mtaratibu na mpole sana, na hata niliposikia habari hizi kwa namna fulani nimeshtushwa nazo.
Ludovick ambaye amekuwa akiishi Dar ni mmoja wa vijana waliokuwa wakinisaidia kwa kujitolea kwenye kazi zangu za mitandaoni, hususan kwenye Mjengwablog na website ya Kwanza Jamii. Amekuwa na mchango mkubwa, na hata katika miezi ya karibuni,ndiye yeye aliyekuwa akifanya kazi ya kuingiza magazeti kwenye Mjengwablog kila asubuhi.
Akiwa Dar na mimi nikiwa Iringa, Ludovick hakuwa mwajiriwa wangu kama wanavyodhani wengine, bali , amekuwa ni mmoja wa vijana waliokuwa tayari kunisaidia kwa kazi za hapa na pale ikiwamo kunipelekea invoice kwa watangazaji kwenye Mjengwablog.
Mara nyingi nimekuwa nikimtambulisha kama ' Msaidizi wa Mwenyekiti'.
Na jana nilimwomba aje Iringa aniletee vitabu vyangu vya invoice na risiti kwa vile nilitarajia ugeni wa kutoka TMF- Mfuko wa Ruzuku kwa vyombo vya habari. Kwamba huenda vitabu hivyo vingehitajika wakati wa mazungumzo na watendaji wa TMF yaliyofanyika leo asubuhi.
Hata hivyo, katika hili lililomtokea, siwezi hapa kumtetea wala kumtia hatiani. Maana, naye ni binadamu kama wengine, siwezi kusema kuwa ninamfahamu sana. Kwa vile yuko mikononi mwa vyombo vya usalama , nina imani, kuwa vyombo hivyo vitafanya kazi yake ili kutusaidia katika kupata ukweli wa jambo zima.
Na kama ni kweli kwa namna yoyote ile itathibitishwa kuwa ameshiriki njama za kupanga mikakati hiyo ya kigaidi, basi, ahukumiwe kwa dhambi hiyo.
Ni mimi:
MAGID MJENGWA
No comments:
Post a Comment