Kaimu Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Tatu Burham
Jumla ya Watanzania 1,064 waliozamia nchini Afrika Kusini, bila kuwa na vibali, wamerejeshwa nchini katika kipindi cha mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Tatu Burham, idadi yao inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na urahisi wa kufika kwenye nchi hiyo kwa njia zisizo rasmi.
Mathalani, alisema mwaka 2010, Watanzania waliorudishwa walikuwa ni 700, lakini kwa sasa wameongezeka.
Alifafanua kuwa wengi huenda huko kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutafuta maisha mazuri na wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.
Burhan aliongeza kuwa zoezi hilo huwa ni gharama kwa serikali, kwani tangu kuwakamata kuwahudumia chakula wakiwa mahabusu, mazungumzo baina ya serikali mbili na usafiri wa kuwarudisha nchini, hufanyika kwa kusaidiana gharama.
“Hatari iliyopo ni uwezekano wa mahusiano baina ya nchi na nchi kuvunjika, serikali zote tunachangia gharama za kuwarejesha, hadhi ya nchi inashuka,” alisema.
Alisema mara wanapofikishwa hapa nchini, hupelekwa mahakamani kujibu kosa la kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria na suala hilo huachiwa mahakama.
Aliongeza kuwa waathirika wakubwa wa suala hilo ni vijana kutokana na kushawishiwa kupata maisha mazuri kwa haraka.
Alisema idara hiyo ina mpango wa kutoa elimu kwa kutumia vyombo vya habari na maonyesho mbalimbali ili wasiwe wepesi kushawishika. Alisema kwenye nchi za Ulaya idadi yao ni ndogo ukilinganisha na Afrika Kusini ambako ni karibu.
Kwa upande mwingine, alisema idadi ya wahamiaji haramu wanaoingia nchini kwa sababu mbalimbali wengine kwa kupita njia na kuishi, inaongezeka kila mwaka.
Alisema mwaka 2011 walikamatwa wahamiaji haramu 3,480 na mwaka jana walikuwa 4,765.
Hata hivyo, alisema wageni kutoka nchi mbalimbali walioingia kwa malengo ya matembezi na kikazi ni 967,994 na Watanzania waliotoka kwenda nje ni 976,800.
Burhan alisema waliopewa vibali vya ukazi ni 16,882 kwa mwaka 2011.
Aidha, aliwataka Watanzania kupenda kufuata sheria na taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uwapo wa wahanga wa biashara ya binadamu na wahamiaji haramu kwa manufaa ya taifa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment