ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 23, 2013

DCI Mungulu:Bado tunamsaka aliye na kompyuta ya Dk. Mvungi

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu
Jeshi la Polisi nchini limesema halijafanikiwa kumkamata mtu anayedaiwa kuwa na kompyuta mpakato (laptop) ya marehemu Dk. Sengondo Mvungi, aliyevamiwa na majambazi na kujeruhiwa vibaya kwa mapanga na hatimaye kufariki akiwa kwenye matibabu nchini Afrika Kusini.

Aidha, Jeshi hilo limesema linaendelea kuwatafuta wahusika wengine wa matukio mawili ya mabomu yaliyotokea kwa nyakati tofauti mkoani Arusha na kusababisha vifo.

Akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es Salaam baada ya mkutano wake na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI, Kamishna Isaya Mngulu, alisema Jeshi lake halijamtia nguvuni mtu huyo pamoja na kwamba amekwishafahamika.

Novemba 21, mwaka huu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulaiman Kova, alimtaja mkazi mmoja wa Jiji la Dar es Salaam kwamba ndiye anayeishikilia laptop ya marehemu Dk. Mvungi.


Mtu huyo (jina tunalihifadhi), mkazi wa Vingunguti, anadaiwa kuwa ndiye anahodhi ya marehemu aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kova alisema kuwa jeshi hilo limechukua hatua hizo baada ya kufanya uchunguzi wa kina katika upelelezi imegundulika kwamba kompyuta ya marehemu inamilikiwa isivyo halali na mtuhumiwa huyo.

Alisema Jeshi la Polisi Kanda Maalum linaendea kufanya jitihada kubwa kwa lengo la kuipata laptop hiyo na linaendelea kumtafuta mtuhumiwa mpaka atakapopatikana.

Akizungumzia matukio ya mabomu jijini Arusha, Mngulu alisema kuwa mpaka sasa Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtu mmoja tu, anayetuhumiwa kuhusika kwenye tukio la bomu lililotokea kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti Mae 5 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu wanne.

Mngulu alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikwishafikishwa mahakamani na kesi hiyo bado inaendelea.

Kuhusu tukio la bomu lililotokea kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata tano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Juni 14, mwaka huu na kuua watu wawili, Kamishna Mungulu alisema kuwa bado hajakamatwa mtu yeyote kuhusu tukio hilo. Aliongeza kuwa upelelezi kwa ajili ya kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilo bado unaendelea.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa makosa ya uhalifu nchini yameongezeka kwa kutoka 66,252 yaliyoripotiwa mwaka jana hadi 66,906 kwa mwaka huu, ambayo ni ongezeko la makosa 654 sawa na asilimia 1.0 ikilinganishwa na makosa yaliyotokea mwaka jana.

Mngulu alisema kuwa makosa ya uhalifu ni pamoja na mauaji, vitendo vya ubakaji, unyanganyi wa kutumia silaha, uvunjaji biashara haramu buashara ya dawa za kulevya, kupatikana kwa silaha, uhamiaji haramu pamoja na matukio ya ajali za barabarani zilizosababisha vifo.

Mngulu aliongeza kuwa pamoja na makosa hayo jumla ya watuhumiwa 81,626 walikamatwa na kufikishwa mahakamani ikilinganishwa na watuhumiwa 43,674 waliokamatwa mwaka jana ambayo ni ongezeko la watuhumiwa 37,954 sawa na asilimia 86.9.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: