Mwili wa Atu ukiwa chumbani kwa mtu anayesadikika kuwa ni mpenzi wake, Hafidh Mohammed.
MSICHANA Atu Gabriel mwenye umri wa miaka 20, mwanafunzi wa Chuo cha Eden Hill kilichopo Kwamfipa wilayani Kibaha mkoani Pwani, amekutwa amekufa chumbani kwa mtu anayetajwa kuwa ni hawara yake, Hafidh Mohammed.
Tukio hilo lilitokea April 26, mwaka huu na kukusanya umati huku mwanaume aliyelala na binti huyo akitokomea kusikojulikana.Marehemu anadaiwa kuwa mwenyeji wa Makambako mkoani Njombe.
Akizungumza na waandishi wetu juzi Kibaha, mama wa Hafidh ambaye pia ni mjumbe wa eneo hilo, Zainabu Saidi alisema mwanaye alimweleza kutokea kwa tukio hilo asubuhi kulipokucha na kabla ya hapo, hakuwa akifahamu kama alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo kwa vile aliyekuwa akimfahamu ni mwanamke mwingine ambaye alizaa naye.
“Mimi kwa kweli sikuwa na taarifa yoyote juu ya uhusiano wao na huyu mwanafunzi, nimeletewa taarifa asubuhi na kijana wangu huku akionekana kuchanganyikiwa, nimejaribu kumsihi asikimbie lakini imeshindikana,” alisema mama huyo.
ALIVYOAGA CHUONI
Wanafunzi wa chuo hicho kinachofundisha masomo ya biashara na habari ambao walikataa kutaja majina yao waliliambia gazeti hili kuwa, marehemu Atu aliwaaga anakwenda jijini Dar es Salaam kumuuguza wifi yake aliyelazwa katika Hospitali ya Amana, Aprili 23, mwaka huu.
Hata hivyo, walisema uondokaji wake uliwapa maswali mengi kwani tofauti na walivyotegemea kuwa angebeba mfuko mkubwa wenye nguo za kubadili, yeye aliondoka akiwa na mkoba wake wa mkononi pekee hali iliyoonesha hakuwa akienda mbali.
Walisema siku tatu baadaye walipatwa na mshtuko mkubwa baada ya mlinzi wa hosteli yao kuwaletea taarifa za kifo cha mwenzao kilichotokea katika chumba cha mvulana huyo anayeishi jirani.
MAJIRANI NAO WANENA
Majirani waliozungumza na gazeti hili walisema kwao haikuwa mara ya kwanza kumuona msichana huyo, kwani mara kwa mara alikuwa akifika pale ingawa akishaingia ndani hakuwa akitoka nje.
Walisema mara zote hizo, mwanaume huyo mwenyeji ndiye alikuwa akitoka nje na kwenda kumnunulia chakula.
POLISI WAUPELEKA MWILI HOSPITALI YA TUMBI
Jeshi la polisi liliwasili eneo la tukio na kuukuta mwili huo ukiwa umelala kitandani ukiwa hauna jeraha, lakini pembeni yake kulikutwa vidonge ambavyo havikufahamika ni vya aina gani ambavyo pia vilichukuliwa pamoja na mkoba wake hadi kituonis.
Minong’ono kutoka kwa majirani kuhusiana na vidonge hivyo ilitofautiana, baadhi yao walisema huenda vilitumika katika jaribio la kutoa mimba, wengine walisema inawezekana msichana huyo alipata ugonjwa wa ghafla usiku na mwanaume huyo alikwenda kumchukulia vidonge hivyo ambavyo havikuweza kumsaidia marehemu kupata nafuu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, SACP Ulrrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema juhudi za kumtafuta mwanaume huyo zinaendelea huku madaktari nao wakiendelea na uchunguzi wao ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
GPL
No comments:
Post a Comment