Mada ya uraia pacha imechukua sura mpya ndani na nje ya
Tanzania hasa katika kipindi hiki ambapo wadau mbalimbali wameshirikishwa
kuchangia katika uandikwaji wa katiba mpya ambayo itaunda sheria mpya au
kurekebisha zile za zamani zitakazowaathiri watanzania wote popote waishipo
duniani. Kuna masuala mengi ambayo
yanahitaji utafiti, uelimishwaji wa umma na wabunge wa baraza la katiba
kuhakikisha kuwa sheria zinazopitishwa zitalinda maslahi ya nchi pamoja na haki
za msingi za kila mwananchi mzawa na kuboresha sheria zinazozungumzia raia
wapya ambao si wazawa ya Tanzania. Katika vifungu vifuatavyo, nitajaribu kutoa
maelezo kuhusu baadhi ya hoja ambazo zimepelekea suala zima la ujumuishwaji wa
uraia pacha kuvuta hisia tofauti.
Watakaopewa uraia
pacha wataigeuza Tanzania shamba la bibi
Hii ni moja kati ya hoja nyingi ambazo kundi la watanzania
wanaopinga uraia pacha wamekuwa wakiitumia kueleza jinsi gani urai pacha
utakavyoathiri uchumi na maliasili za nchi. Hoja hii
inaukweli ndani yake iwapo
tu nchi haitakuwa na sera na sheria za kulinda uchumi kwa maslahi ya taifa. Si
hivyo tu, hata kama nchi itakuwa na sheria lakini kama hazitasimamiwa kwa ufanisi
wa makusudi, kutoka kwa wale waliopewa
majukumu ya kuzisimamia, bila shaka nchi yetu itakuwa shamba la bibi.
Pamoja na hoja hii kuwa na nguvu, siamini kama hii ni sababu
tosha ya kutopitisha sheria ya uraia pacha kwa mamilioni ya watanzania ambao
walichukua uamuzi wa kwenda kutafuta elimu, kazi na maisha bora ambayo yalikuwa
ni vigumu kuyapata katika mazingira wajiyoondokea. Ukweli wa mambo ni kuwa hawa wananchi
walioondoka kwenda nje ya nchi na kujifunza, kupata uzoefu wa nadharia na
vitendo katika nyanja na fani tofauti ni rasilimali yenye thamani ambayo ni
lazima ienziwe na kujengewa mazingira bora pale wao au watoto wao watakapoamua
kurudi kulinufaisha taifa. Ni wazi kuwa taifa letu bado linahitaji wasomi
katika fani mbalimbali ambao wanaufahamu mpana na uwezo wa kufanya maamuzi
yenye maslahi ya taifa. Zaidi ya wasomi, kuna wanadayaspora wengi waliojenga
biashara kubwa nje ya Tanzania ambao wana hamu kubwa kurudi kwao kuziendeleza
biashara zao na kutoa ajira kwa maelfu ya raia wenzao ambao. Uamuzi huu unakuja
kutoka kwa watu waliona uzalendo na mapenzi ya nchi yao na itasikitisha kuona
kama bunge la katiba litashidwa kulielewa hili.
Walioondoka Tanzania
hawana uzalendo
Hii ni hoja nyingine ambayo hutumiwa na wale wanaopinga urai
pacha, na ni kweli kusema kuwa baadhi ya watanzania walioondoka hawakuwa wazalendo
na nchi yetu. Vile vile kuna watanzania
wengi waliopo Tanzania ambao hawana Imani wala uzalendo na taifa letu. Kuna
mifano mingi ambayo inaipa nguvu hoja hii. Kwa mfano nilishangazwa kuona
misururu mirefu ya magari yakivuka mpaka kuelekea Kenya wakati wa uchaguzi wa
kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995. La
ajabu zaidi, wale waliokuwa wakivuka mpaka walikuwa watanzania wenye asili ya
asia na baadhi ya wazungu wakihofia kutokea machafuko kufuatia matokeo ya
uchaguzi. Wengi wa hawa jirani zetu wa kiasia wana uraia wa zaidi ya nchi mbili
na hawa ndio walioigeuza nchi yetu shamba la bibi kwa kukosa uzalendo na
Tanzania na wako tayari kukimbia pale kunapotokea hali ya wasiwasi. Hawa bado
wana hisia na mapenzi ya nchi mama walizotoka tukikubali au tukikataa.
Watanzania wengi waliopo ughaibuni bado wana mapenzi na
uzalendo wa kutosha na nchi yao na ndio maana japo kuwa kuna baadhi yetu
wasiounga mkono uraia pacha idadi yao ni ndogo kuliko wale wanaotaka uraia
pacha. Bado watanzania waishio ughaibuini wanaguswa na majanga yanayotokea
Tanzania na mara nyingi hufanya harambee kuchangisha pesa kusaidia wahanga,
watoto yatima, mahospitali, mashule, kuchimba visima, kujenga barabara na
orodha ya hisani hizi ni ndefu. Urai pacha utatupa nguvu, uhuru na moyo zaidi
wa kusaidia nchi yetu kwa hali, mali, na fikra. Katika miaka ya karibuni kuna
matawi mengi ya vyama vya siasa vya Tanzania ambayo yameanzishwa kwa Imani
kuwa hii itakuwa moja ya njia ya kufikisha
mawazo yetu katika ujenzi wa taifa. Haya hayatokei bila ya kuwa na mapenzi na
uzalendo na nchi mama.
Watanzania wa
ughaibuni hawachangii uchumi na ni hatari kwa usalama wa Taifa
Mchango wa wanadayaspora katika uchumi wa nchi za kiafrika
na mahususi Tanzania ni mkubwa na unaotambulika na mashirika yote makubwa ya
fedha duniani. Katika utafiti uliofanywa
na taasisi ya Brookings wa mwaka 2013, imeyakinishwa kuwa waafrika waliopo
dayaspora hupeleka zaidi ya dolla billion arobaini kwa mwaka ambao huingia moja
kwa moja katika uchumi tofauti na misaada toka nchi wahisani ambayo sehemu
kubwa huishia kwenye urasimu na kukuza deni la taifa. Watanzania pekee hutuma
zaidi ya dolla 300 kila mwaka moja kwa moja katika uchumi na kusaidia kwa kiasi
kikubwa kuukuza uchumi wa taifa. Hiki kiasi kinachangia asilimia 2.4 ya pato la
taifa.
Kiasi hiki cha pesa zinazoletwa nchini itaongezeka iwapo sheria
ya uraia pacha itapitishwa na hoja hii inapewa nguvu kwa mifano hai toka nchi
kama za Uganda, Nigeria na Kenya ambazo mara baada ya kupitisha sheria ya uraia
pacha wanadayaspora wao wamekuwa
wakituma pesa zaidi ya mara dufu walizokuwa wakipeleka wakati hawana uraia
pacha. Kwa maelezo ya takwimu, wakenya
wameongeza kutuma pesa kwenye uchumi wa Kenya hadi kufikia dolla milioni 791
kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 3.8 ya uchumi wa taifa, waganda wanatuma
dolla milioni 642 kwa mwaka sawa na asilimia 6.9 wakati wanaigeria hutuma billion 5, 397 sawa na asilimia 4.7 ya
pato la taifa. Kwa mtaji huu mchango wa watanzania wa dayaspora ni wa kujivunia
na kuenziwa kwa kupitisha sheria ya uraia pacha. Sisi wanadayaspora hatuna nia
mbaya na nchi yetu na takwimu zinajieleza wazi.
Vizazi vya watanzania
waishio ughaibuni havina haki ya uraia pacha
Hii ni hoja ambayo haina msingi na inapingana na sheria ya
uhamiaji iliyopo sasa ambayo inampa uraia mtoto ambae amezaliwa na wazazi au
mzazi ambae ni raia wa jamhuri ya Tanzania. Watoto hawa wana uhuru wa kuukubali
au kuukataa uraia wa Tanzania pale wafikishapo miaka kumi na nane (18). Kwa
vile sheria ya sasa ya uhamiaji inamvua uraia wa Tanzania mtu yoyote anaekubali
uraia wa nchi nyingine wanadayaspora wanalishawishi bunge la katiba kuwafikiria
mamilioni ya watoto wa watanzania ambao watapenda kuwa na haki ya nchi ya
wazazi wao pale watakapoamua kurudi katika ujenzi wa taifa au hata pale
watakapoamua kuja kutembelea ndugu na jamaa zao wasitakiwe kuwa na visa kwani kwa
kufanya hivyo itakuwa ni kuwawekea vizingiti katika kushiriki kikamilifu katika
kuienzi nchi yao.
Imeandikwa kwa niaba ya watoto wetu waliozaliwa au kukulia
ughaibuni.
Na Baba Wangenya,
Maryland USA
1 comment:
Blogger
wazanzibari mbona wanao uraia pacha na kwa nini tunagombania uraia pacha wa nchi mbili tu kwa nini kusiwe na quad-triple kwa sababu wengi wetu tumekalia kidunia zaidi.
Watu wanaacha kujadili hoja ya msingi wanakwenda kujadili details za hoja kwanza? Huu sijue ni ulimbukeni wa design gani. Urai pacha utatishia usalama, usalama gani, elezeni usalama gani, Rais hata lindwa au jeshi hakuna? Au usalama wa nchi ni matumbo yao? Eti watu watahujumu. Kuhujumu nini nchi hii, wakati wahujumu namba moja wa ni hao hao viongozi pamoja na sheria mbovu za nchi ambazo hawataki kuzibadili. Hivi hawa jamaa akili za kufikiri wanatoa wapi? Wasomi wote mashuhuri na wenye sifa wamesomeshwa nchi za nje, elimu yetu, sheria zetu, kila kitu ni copy and paste, sasa unategemea nini.
Dodoma kuna mtu mwenye akili?
Tanzania bara itakuwa ya mwisho katika hili la urai pacha katika afrika nzima kwani zimesalia nchi nane tu la kujiuliza nchi zote hizo zilizojisajili katika uraia pacha wao hawajali usalama wa nchi zao? au hawana uzalendo hata hao warusi na wachina ambao ndio tuliowafuata katika ukomunisti wameamua na kuona hili lina manufaa kwa nchi zao lakini sisi mmhhhmmhh bado tunawasha mwenge na kuukimbiza nchi nzima unategemea nini hapo.
nawakilisha tuuuu
August 31, 2014 at 9:34 PM
Anonymous Anonymous said...
To be fair, wengine hata uraia pacha usingetutosha, kwani tupo kidunia zaidi, labda wangetupa quadruple-quintuple citizenship.
Au uraia wa Umoja wa Mataifa tu.
sijui watanzania ni watu wa aina gani, alikuja kikwete hapa DC miezi michache iliyopita akasema uraia pacha haujapigiwa kelele za kutosha na upinzani hawautaki, mimi nkawa nawaambia watu kikwete muongo, watu oho hujui, huna adabu, sasa hapa tunaona wapinzani ndo hawautaki au ccm, mimi naona mitanzania hasa inayoishi DMV isipewe maana hata kufuatilia mambo ya tz kwa undani hayafuatili, ni kufuata upepo tu na yakidanganywa kidogo yanafurahia, nimeangaika sana kuwaeleza hali halisi maana mm sikutoka bongo mda mrefu lakini hayaelewi, kikwete akija yanamchekea tu na kumsifu sifu bila mpango yakidhani atawapa uraia wa nchi mbili kumbe hawajua anageuka geuka kama kinyonga.
Na pia kwa muktadha huo lile dawati la DIASPORA pale wizara ya mambo ya nje walifute, maana diaspora ni akina nani kama hawatambuliki..?! Zile hela za kuendesha dawati(kitengo) zipelekwe zikasaidie miradi ya maendeleo na tuache siasa za kudanganyana na unafki.
Mimi nlishasema na nawaambia watanzania kama unaishi nje amua moja tu unaikacha tz unachukua uraia wa nchi nyingine unapiga kazi, unajisaidia wewe na jamii yako nyumbani maisha yanaenda ila kuwategemea akina kikwete, membe, wasira, lukuvi, nape na ccm eti waje wakupe uraia wa nchi mbili nk ni kupoteza muda na akili ya kutafuta maendeleo yako.
Na jumuia za watanzania zilizoko nje sasa zitarudi kwenye malengo ya kuanzishwa kwao, na kuacha kujipendekeza kwa viongozi kusikokuwa na sababu, kiongozi aheshimiwe tu lakini sio kujipendekeza kwake kusikokuwa na msingi nadhani sasa mmeona.
Name/URL
Anonymous
Publish Your Comment Preview
Post a Comment