Advertisements

Saturday, November 1, 2014

MOI: Hatuwakati miguu majeruhi


Kwa muda mrefu sasa, umekuwepo uvumi kwamba Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili(MOI), imekuwa ikiwakata viungo majeruhi wa ajali za bodaboda hasa madereva kama njia ya kuwakomesha.

Tuhuma hizo ambazo zimekanushwa vikali na taasisi hiyo, zilidai kuwa kutokana na majeruhi wa pikipiki kuongezeka, madaktari huamua kuwakata viungo kama miguu.

Matokeo yake, ikadaiwa kuwa baadhi ya ndugu na jamaa wa majeruhi hao huamua kuwapeleka majeruhi katika hospitali binafsi.
Hata hivyo, taasisi hiyo ilisema inapokea majeruhi 600 kwa mwezi na kati yao asilimia 55 wanatokana na ajali za pikipiki.

Hata hivyo, wengi wa wagonjwa hao wanakatisha matibabu yao kwa sababu mbalimbali, ikiwamo matukio ya kutoroka wodini kwa kukosa pesa za gharama ya matibabu.

Akizungumza katika mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa MOI, Patrick Mvungi, alisema ajali za pikipiki zimekuwa changamoto kubwa katika hospitali hiyo na kusababisha madaktari kufanya kazi kwa saa zaidi ya 18 kwa siku.

Mvungi alikuwa akizungumzia suala hilo baada ya kuibuka kwa tuhuma zinazotolewa na waendesha pikipiki kwamba hospitali hiyo inafanya mkakati wa chini kwa chini ya kuwakata miguu majeruhi wa pikipiki hasa madereva wanaofikishwa hospitalini hapo kama njia ya kuwadhibiti.

Kutokana na madai hayo, wagonjwa wengi hukimbiziwa hospitali binafsi kwa ajili ya kwenda kupata huduma.

Hata hivyo, Mvungi, alisema hakuna kitu kama hicho kinaendelea ndani ya hospitali hiyo na kwamba wagonjwa wote wanaofikishwa hapo wanapatiwa tiba kulingana na ushauri na vipimo sahihi vya kitaalamu.

Alisema katika takwimu inaonyesha kwa siku wanapokea zaidi ya wagonjwa 11 wa ajali ya pikipiki sawa na idadi ya 77 kwa wiki moja.

Alisema kutokana na idadi hiyo kuwa kubwa, wodi za hospitali hiyo zinaelemewa kwa kulaza wagonjwa 95 kwa wakati mmoja badala wagonjwa 33 inayotakiwa.

“Idadi hii ni kubwa sana na hakuna siku ambayo ilionekana kupungua, lakini madaktari wanajitahidi kuwahudumia kwa kutumia zaidi ya muda unaotakiwa kitaaluma,” alisema Mvungi.

HAKUNA NJIA YA KUKWEPA MOI
Hata hivyo, mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo ambaye ametaka jina lake lisiandikwe gazetini, alisema mtu aliyepata ajali na kuvunjika viungo hawezi kukwepa kwenda MOI kwa ajili ya tiba.

Alisema hospitali za wilaya na watu binafsi zinaweza kutoa matibabu kwa kiwango fulani ya majeraha, lakini tatizo linapokuwa kubwa lazima atafikishwa hapo kurekebishwa.

“Hapa nchini hakuna hospitali inayounganisha mifupa au mishipa ya fahamu isipokuwa MOI pekee, sasa hao wanaodai kwamba sisi tunakata miguu kama kuwakomoa, wahoji walitibiwa wapi?, huo ni upuuzi,” alisema daktari huyo.

WAGONJWA: TULIKUWA NA HOFU
Baadhi ya madereva wa pikipiki waliolazwa katika wodi namba 17 jengo la Kibasila wakipatiwa matibabu, walisema awali walikuwa na hofu ya kupoteza viungo vyao, lakini hali hiyo ilitoweka baada ya kuona hakuna kitu cha aina hiyo.

Urasa Paulo (22) mkazi wa Makongo, alisema alipata ajali miezi miwili iliyopita baada ya kugongwa na gari akiwa anaendesha pikipiki yake.

Alisema katika ajali hiyo amevunjika mguu wake wa kulia.
“Hapo mwanzo niliogopa kutokana na habari za mitaani, lakini nilipokuja hapa nilihudumiwa vizuri na kufanikiwa kuungwa mguu wangu,” alisema Urasa.

Naye Rajabu Juma (22) Mkazi Kindondoni, ambaye amekatwa mguu wake wa kulia baada ya kupata ajali mbaya ya pikipiki, anasema pamoja na mguu huo kukatwa, hawezi kusikitika kwani madaktari walijitahidi kuunga lakini walishindwa baada ya kuonyesha hali ya kuharibika.

“Walinishauri mguu ukatwe ili kudhibiti afya yangu nilikubali baada ya kuona unaharibika na siyo nilikatwa kwa nguvu,” aliongeza kusema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: