Advertisements

Wednesday, December 31, 2014

MWENYEKITI WA CHADEMA IRINGA MJINI AINGIA MATATANI TENA, AMTUKANA MWENYEKITI WAKE WA MKOA, ASHITAKIWA

Picha ya Maktaba ikumuonesha Frank Nyalusi (mwenye suti nyeupe) ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Iringa Mjini akiwa chini ya ulinzi wa Polisi

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Iringa Mustapher Msowela amemshitaki mwenyekiti wa chama hicho jimbo la Iringa Mjini, Frank Nyalusi ambaye jana jeshi la Polisi lilifanikiwa kumtia nguvuni kabla ya kuachiwa kwa dhamana.
Nyalusi aliyeshitakiwa katika kituo cha Polisi cha kati cha mjini Iringa jana, anatuhumiwa kumtusi mwenyekiti wake huyo wa mkoa kupitia mitandao ya simu; matusi yanayoendelea kuchunguzwa na jeshi hilo.
Nyalusi amekamatwa kwa tuhuma hiyo ikiwa ni siku chache tu baada ya kudaiwa kutoa tuhuma za uongo kwa lengo la kujipatia umaarufu dhidi ya mfanyabiashara maarufu wa mjini Iringa, Salim Asas ambaye pia ni Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Iringa.


Katika mkutano wa hadhara uliofanywa na Chadema Desemba 21 kwenye uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, Nyalusi ambaye pia ni diwani wa kata ya Mivinjeni alitoa tuhuma zinazowahusisha vijana watatu ambao hata hivyo hakuwataja majina kwamba walitumwa na Asas kwenda kumuua.


Asas kwa kupitia kwa wakili wake, Alfred Kingwe amekanusha tuhuma hizo alizoziita ni za kipuuzi ambazo haziwezi kubebeka hata kwa mzani mdogo wa kupimia madini.


Ili kumsafisha mteja wake, Kingwe alisema ndani ya siku 14 toka akabidhiwe hati ya madai (Demand Note), Nyalusi anatakiwa kuitisha mkutano katika eneo lile lile alilotolea tuhuma hizo na kuzikanusha vinginevyo atafikishwa mahakamani.


Akizungumza na wanahabari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema; “Kuhusu tukio la kumtukana mwenyekiti wake wa mkoa, Nyalusi alikamatwa jana mara baada ya Msowela kuwasilisha malalamiko yake polisi, akahojiwa na kuachiwa baada ya kukamilisha taratibu za dhamana.”


Alisema jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza tukio hilo la kijinai na endapo litathibitika kuwa la kweli, Nyalusi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mivinjeni mjini Iringa atafikishwa mahakamani.


Kuhusu tukio linalomuhusisha na Asas, Kamanda Mungi alisema jeshi la Polisi limefanya mahojiano ya awali na wahusika hao.


“Jambo hili lipo, tunachunguza; yapo maneno Nyalusi ameyatamka kwenye mkutano wao wa hadhara kwamba ametishiwa kuuawa, ametumiwa watu watatu kwenda kumuua wakiwa na visu. Kumtishia mtu ni kosa la jinai na kumtuma mtu kwenda kumdhuru mtu mwingine ni kosa la jinai, kwahiyo tunachunguza” alisema.


Alisema katika mazingira ya uwazi, Polisi inachunguza suala hilo ili kujua Nyalusi alitishiwa katika mazingira gani; alitishiwa na nani na kwanini hakwenda kutoa taarifa hiyo Polisi na kufungua kesi ili Polisi iwakamate wahusika na kulinda maisha yake.


“Lakini tunajaribu kuangalia kama hakutishiwa na ametamka vile katika mkutano wa hadhara, lengo lake lilikuwa ni nini na kama anajua madhara yake kwa jamii iliyosikia taarifa hiyo ni yepi,” alisema.


Alisema kama itabainika taarifa zilizotolewa na Nyalusi ni za uongo, sheria itachukua mkondo wake na kama itadhihiri ni za kweli sheria pia itachukua mkondo wake.


Wakati Kamanda huyo wa Polisi akitoa taarifa hiyo jana, Nyalusi alikuwa nje ya ofisi ya kamanda huyo na alipofuatwa na wanahabari kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa matukio hayo alijibu kwa kifupi akielezea zaidi tukio la kushitakiwa na mwenyekiti wake wa Chadema mkoa kwamba; “mimi sijamtusi mtu, anaweza kusema chochote anachoweza kusema yeye na familia yake, kusema ni hiari yake.

No comments: