KATIBU Mkuu wa Klabu ya Yanga, Dr. Jonas Tiboroa akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, kulia ni Mkuu wa kitengo cha habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro.
Kwa miaka mingi sasa klabu Kongwe za Simba na Yanga zimekuwa zikiibiwa bila kujua zinapoteza mamilioni ya pesa kila mwaka kupitia uuzwaji wa jezi zenye nembo ya klabu yao (Logo), Lakini kama kweli mpango huu hautaishia midomo tu basi Yanga itakuja kuwa bonge la Timu Tajiri Tanzania kupitia jezi zake.
Akizungumza na Shaffihdauda.com, Katibu mkuu wa klabu ya Yanga SC, Dr Jonas Tiboroa amesema kuwa tayari uongozi umesajili nembo (logo) 16 ambazo zinatumika katika jezi za timu hiyo.
Kufatia usajili wa Logo hizo basi Yanga itakuwa imefanikiwa kupiga marufuku uuzwaji ovyo wa jezi zao kitu ambacho kitasaidia kuingiza pato klabuni moja kwa moja kwa kuingia mkataba na wafanya biashara ambao watataka kujihusisha na uuzaji wa jezi hizo.
“Nikuambie tu Jezi unazoziona mitaani bado muda mfupi zitakuwepo na muda mfupi hazitakuwepo, Namanisha kwamba tumesajili nembo (logo) zetu, Kwa maana hiyo sasahivi tunahaki ya kumzuia mtu yeyote ambaye atafanya biashara ya hizo jezi kama sio muhusika wa Young Africans” Amesema Dr Jonas Tiboroa ambaye sio siri amekuja kwa kishindo kikubwa Yanga.
Akizungumzia ugumu uliokuwepo katika uongozi wa zamani namna ya kuzuia Biashara hiyo kufanyika, Dr. Tiboroa amesema kuwa walikuwa wakiongea tu bila kuchukua hatua kitu ambacho kimefanya Yanga ipoteze pesa nyingi sana.
“Inawezekana walikuwa wanasema wanaenda kusajili lakini hawendi, Sisi tumesajili kwahiyo ukienda leo BRELA utakuta nembo zetu zipo pale 16, na tumefanya hivyo kutokana tumekuwa tukipoteza mapato mengi sana kwa vitu ambavyo kama klabu tungeweza kufanya wenyewe” Amesema Dr Tiboroa ambaye amekuja kufanya mapinduzi Yanga SC.
Akizungumzia umuhimu wa kusajili nembo hizo kama klabu Dr. Tiboroa amesema kuwa “Hauwezi kufanya biashara na makampuni makubwa kama Nembo yako haijasajiliwa kibiashara, Usije ukamlaumu mtu wa mtaani anayetumia nembo yako kwa sababu wewe hujataka kuwa na haki ya nembo yako kwa kuisajili” Amesema Dr Tiboroa ambaye hababaishi katika Soka la Tanzania.
Dr Tiboroa amesema kuwa zamani ilikuwa vigumu kuzuia biashara ya jezi za Yanga Mitaani kwani ili uweze kufanya biashara lazima uwe umesajiliwa lakini wao logo zao zilikuwa kwenye makaratasi tu.
“Ni kweli ni ngumu kwa maana biashara yoyote lazima iwe imesajiliwa, kwa maana hiyo ili uweze kuitumia nembo kwenye biashara lazima iwe imesajiliwa kw miaka mingi nembo zetu zimekuwa zikijulikana kwenye makaratasi lakini nembo kama nembo ilikuwa haijulikani sehemu yoyote kama inaweza kufanya Biashara” Amemalizia Dr. Tiboroa.
Ukweli ni kwamba Yanga na Simba ndio timu kubwa ambazo zinaongoza kwa mashabiki, hivyo endapo zoezi hilo litsimamiwa vyema basi Yanga itakuwa imebika teke kopo la Umasikini kwa kuuza jezi moja kwa moja kutoka klabuni kama ilivyo kwa Mbeya City na Azam FC ambao wao kidogo wamefanikisha.
CREDIT:SHAFFIHDAUDA.COM
No comments:
Post a Comment