ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 11, 2015

KURUKARUKA NI TABIA AU KUNAUMBWA NA KERO?

MAISHA ya ndoa na uhusiano wa kimapenzi ni sanaa yenye umri mkubwa tangu enzi za Adamu na Hawa. Matatizo yamekuwa ni mengi tangu mwanamke wa kwanza aliyeumbwa kwa ubavu wa mwanaume alipokubali kudanganywa na nyoka katika bustani nzuri ya Eden miaka milioni nyingi zilizopita.

Leo hii, sanaa ya mapenzi imeanza kuingia katika ukisasa, wa kidigitali, kiasi kwamba hata staili tu ya maisha, inaweza kuwa chanzo cha kustawi au kubomoka kwa ndoa au uhusiano wa kimapenzi. Kuna ambao kabla ya kuwa pamoja, hawakuwahi kuaminiana, lakini baada ya kuwa pamoja, wamejikuta katika hali ambayo awali wasingeweza kuamini.

Katika maisha yetu, tunajuana. Tunajua jinsi majirani zetu wanavyoishi, hata kama watajaribu kutuonyesha usafi wa uhusiano wao. Wabantu, hatuna utamaduni wa kuishi kwa wanandoa au walio katika uhusiano wa kimapenzi kubusiana hadharani, iwe wakati wa kutoka au kurudi kazini. Lakini baadhi yetu, kutokana na mwingiliano wa tamaduni, tumejikuta sasa tukiiga uzungu.

Siyo jambo la ajabu leo, mtu na mpenzi wake kunyonyana ndimi hadharani na yeyote atakayejaribu kushangaa ataonekana mshamba. Aina yetu ya kusalimiana imebadilika, siku hizi unambusu mtu shavu la kushoto na kulia, huku mkikumbatiana, hata kama ni dada, shangazi, kaka, mjomba na kadhalika!
Tabia hizi zimeleta mambo mengi sana, kwani mtu na rafiki yake, wakienda kwa familia rafiki, nao husalimiana kizungu, mke wangu atamkumbatia mshkaji wangu na kumpiga busu, wakati nami nitafanya hivyo hivyo kwa mkewe jamaa!

Kwa ujumla, siku hizi mke au mume hana tena uoga wa kumbusu au kumkumbatia mtu asiye wake kwa sababu mbona ni jambo la kawaida tu, tena linaloweza kufanyika hata mbele yake!
Wapo wanaotumia fursa hii kufanya ufuska wao.

Wanaweza kuwa wana tabia ya kutoka nje ya ndoa zao, lakini mwenza wake anapohisi kusalitiwa, hutiwa moyo kwa kuambiwa aache mambo ya kizamani kwani kama ameona alama ya lipstick shavuni kwa mumewe, ni jambo la kawaida tu kwani alipigwa busu na bosi wake kazini katika sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake.

Au kama ni mwanamke, mume anapohisi kitu katika ukaribu wake na jamaa wa mtaani kwao, ataambiwa aache hayo mambo watu wasije kumcheka, kwani mke na mume wa mtu kukumbatiana kwenye pikipiki ni jambo la kawaida na wala vicheko baina yao visimkwaze kwa sababu wasingeweza kukumbatiana wakiwa wamenuna.

Kitu cha msingi ni kutambua kuwa wapo wanawake au wanaume wahuni ambao wamezaliwa na tabia hiyo na wengine hujikuta wakiamua kuwa hivyo baada ya kuchoshwa na wenza wao. Na ieleweke kuwa maneno kuwa maji hufuata mkondo yana nafasi ndogo sana katika mapenzi. Yaani eti kwa sababu baba alikuwa ni kiwembe sana basi na kijana wake atafuata nyayo, no!
Ndiyo maana huwa tunasikia mtoto wa kasisi akisifika kwa ufuska wakati mzazi wake ni mtu wa sala muda wote.

Lakini pia ni lazima tukubali kuwa kero za mwenza mmoja zinaweza kusababisha mke au mume kuamua kutoka nje kutafuta unafuu.Mtu anapokosa amani ndani ya nyumba yake, hutamani kuipata nje. Ingawa amani haimaanishi kushiriki mapenzi nje ya ndoa, lakini idadi kubwa ya watu waliokwaruzana na waume au wake zao, huamini kuchepuka kunapunguza kitu wanachokiita ‘stress’.

Kwa hiyo jambo la msingi sana kuzingatia kwa wanandoa na walio katika uhusiano wa kimapenzi ni kwamba jitahidi kadiri unavyoweza, ili usiwe chanzo cha kero kwa mwenzako kwa sababu ukizidisha, utamfungulia milango ya kwenda kutafuta unafuu nje. Na elewa, aina yoyote ya maisha ambayo hayampendezi mwenzako ni kero!

GPL

1 comment:

Anonymous said...

Hivi Luka, 'kurukaruka' maana yake nini?