Wednesday, March 11, 2015

UFAFANUZI KUHUSU KASMA MAALUM YA UJENZI WA MIRADI YA BARABARA NCHINI.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale amesema hakuna ufisadi wowote wala malipo tata yaliyofanywa na wizara ya ujenzi kwa makandarasi  na wahandisi washauri katika bajeti ya mwaka 2011/2012.
Eng. Mfugale amesema fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya kasma maalum ya ujenzi wa miradi ya barabara nchini kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 252 kilitumika  kulipa madai ya Makandarasi na Wahandisi washauri.
Eng. Mfugale amesisitiza kuwa Serikali inajenga barabara kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleeo na hulipa makandarasi na wahandisi washauri ili kuwezesha kazi hizo kufanyika kwa wakati na kwa kuzingatia mikataba.
Eng. Mfugale ametoa ufafanuzi huo kufuatia baadhi ya vyombo vya habari kunukuliwa kuwa kumekuwa na ubadhirifu ,au matumizi tata katika malipo ya wakandarasi Wizara ya Ujenzi na kusisitiza kuwa suala hilo lilishajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), katika kikao chake cha Agosti 22 mwaka 2013.
Amewataka watumishi  wa TANROADS kote nchini kuendelea na shughuli zao za ujenzi na usimamizi wa  barabara  bila kuvunjika moyo kwani  hakuna ubadhirifu wowote.
Zaidi ya km 35,000 za barabara hapa nchini  zinasimamiwa na TANROADS kupitia mameneja wake katika mikao 25 nchini kote ambapo takriban KM 11,154 zinajengwa kwa kiwango cha lami katika kipindi  hiki.
Mwisho.
IMETAYARISHWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI.


No comments: