Advertisements

Saturday, May 30, 2015

MWENYEKITI MSAIDIZI WA TUME YA UCHAGUZI YA BURUNDI ATOROKA

Mwenyekiti Msaidizi wa Tume ya Uchaguzi ya Burundi anayedaiwa kutoroka, Spes Caritas Ndironkeye.

Nia ya rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuwania urais wan chini humo kwa muhula wa tatu imezidi kuigharimu nchi hiyo baada ya ripoti kutoka nchini humo zikidai kuwa Mwenyekiti Msaidizi wa Tume ya Uchaguzi ya Burundi ametoroka na hajajulikana alipo.

Ofisa mmoja wa Tume hiyo ameiambia redio moja ya Ufaransa kuwa, Spes Caritas Ndironkeye alipanda ndege ijumaa ya jana na haijulikani alipo na kama alijiuzulu au la.

Tume hiyo ya uchaguzi ina maofisa wakuu watano na inaweza kuendelea kufanya kazi hata baada ya kuondoka kwa mmoja wao.


Hata hivyo taarifa zinaelezea kuwa huenda ofisa wa pili wa Tume hiyo naye akajiondoa na hivyo kulemaza shughuli za kiutendaji za Tume hiyo.

Juma lililopita kanisa katoliki nchini Burundi lilitangaza kujiondoa kwenye harakati zozote za uchaguzi mkuu uliokumbwa na utata siku moja tu kabla ya umoja wa Ulaya kuondoa maofisa wake katika shughuli hizo za uchaguzi nchini humo.

Kanisa katoliki ni kiungo muhimu katika suala la amani na demokrasia nchini Burundi tokea kuanzishwa mazungumzo ya amani ya Arusha mnamo miaka ya tisini.

Umoja wa Ulaya ulikuwa umetuma maofisa wa kusimamia na kuhakikisha kuwa uchaguzi huo ni wa huru na haki.

Taarifa hiyo imetokea wakati ikisalia wiki moja tu uchaguzi wa Wabunge na Madiwani ufanyike nchini humo.

Haya yamearifiwa wakati maandamano dhidi muhula wa tatu wa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza yanaendelea kufanyika katika mitaa kadhaa ya mji mkuu Bujumbura kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Makundi ya kutetea haki za binadamu, yanasema kuwa zaidi ya watu 20 wamefariki wakati wa ghasia za maandamano, tangu rais Pierre Nkurunziza alipotangaza mwezi uliopita kuwa anapania kuwania tena kiti cha urais kwa muhula wa tatu, kinyume na katiba ya Burundi.

Uchaguzi wa urais umepangiwa kufanyika Juni tarehe tano, huku ule wa urais ukiwa mwishoni mwa mwezi huo wa Juni.
NA BBC

No comments: