Advertisements

Monday, August 24, 2015

PAMOJA NA MAUMIVU, HUWEZI KUYAEPUKA MAPENZI

Nianze kwa kuwashukuru wasomaji wote waliotuma ujumbe na hata wengine kupiga, kupongeza na kushauri kuhusu mada ya wiki iliyopita katika safu yetu hii ya XXLove.

Wiki iliyopita tulizungumza kuhusu kitu gani mapenzi yalikufanyia. Leo nitazungumza na wale walioumizwa na mapenzi na kutamani kuyaepuka, wakati ukweli ni kwamba hayaepukiki moja kwa moja isipokuwa labda kwa muda.

Najua wengi mnaweza kushangaa lakini huo ndiyo ukweli wenyewe, pamoja na kuumizwa, kuteswa, kusimangwa, kutukanwa, kupigwa na kufanyiwa vimbwanga vya kila aina kuhusiana na mapenzi, ukweli ni kwamba mapenzi huwezi kuyaepuka moja kwa moja labda upoteze kabisa hamu na hisia juu ya mapenzi, lakini naamini bado itatokea siku moja hisia zako zitanyanyuka tu.

Kwa wale walioshika dini mnaelewa kwamba, Mungu aliumba kila kitu kwa makusudi maalum, ikiwa ni pamoja na kuujaza ulimwengu, mwanadamu wa jinsi ya kike kumfurahisha wa jinsi ya kiume, vivyo hivyo kinyume chake.

Poleni sana wote mnaotamani kuyaepuka mapenzi, akiwemo mmoja wa wasomaji aliyenitumia ujumbe mfupi akidai ameteswa sana na mapenzi, kila mara amekuwa mtu wa kutokwa machozi, amekuwa mtu wa kukosa furaha kiasi cha kutamani hata kujitoa roho, ila Mungu akamnusuru, akaamua kuomba ushauri angalau aepukane na suala zima la mapenzi.

Mwanadamu ameumbwa na mihemko au hisia, kwa namna yoyote ile unaweza kuvumilia kwa muda lakini kuna siku uvumilivu utakushinda. Ndiyo maana hata vitabu vitakatifu vinaeleza kabisa kwamba kama unaweza kuvumilia, basi vumilia ila kama huwezi basi oa na siyo kurukaruka kama wengi wanavyofanya kwa sasa.

Watu wengi sana wamekuwa wakitamani kujiepusha na mapenzi, wanatamani kukaa mbali kabisa na suala zima la uhusiano, kama ni mwanamke, hataki au hapendi kuwa karibu na wanaume. Pia wapo wanaume wa namna hiyo, ukiuliza utaambiwa, ‘nilishaumizwa sana, wanawake siyo watu na mwalimu wao ni mmoja au wanaume wote ni sawa tu na mama yao ni mmoja kwa sababu tabia zao ni zilezile.’

Ni kweli mapenzi yanaumiza sana lakini ukweli ni kwamba pia huwezi kuyaepuka katika maisha yako ya uhai. Inawezekana kukaa kando kwa muda lakini si kuepuka maumivu au misukosuko ya mapenzi.

Sidhani kama kuna uhusiano usiokuwa na mikwaruzo, sina imani kama kuna barabara ndefu isiyokuwa na kona katika dunia hii. Pia sitaki kuamini kwamba kwenye maisha kuna watu wanaofurahia maisha siku zote bila kuwa na chembe ya misuguano penzini.

Kwa taarifa yako, hata huyo unayemuona bosi mtaani au mtu mzima, kuna wakati anateseka na kutokwa machozi kwa sababu ya mapenzi.Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine tamu, pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Facebook kujifunza mengi kuhusu mapenzi.

GPL

No comments: