Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji kilifanyika kwa saa tatu kujadili suala la tarehe iliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar, uliofutwa Oktoba 28, mwaka jana.
Kamati hiyo ambayo ilikuwa na ajenda moja pekee, ilijadili na kutoa uamuzi mzito ambayo yatawasilishwa kwenye Baraza Kuu leo na kutolewa kwa umma.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, aliiambia Nipashe kuwa, maazimio yaliyotolewa na kikao hicho kilichoanza saa nne asubuhi, yataishangaza dunia.
Alisema uchaguzi uliotangazwa na ZEC kuwa utafanyika Machi 20, mwaka huu, ni batili kwa kuwa tayari mshindi wa uchaguzi huo anafahamika ni Maalim Seif.
“Jukumu kubwa la kikao cha Kamati Tendaji kwa mujibu wa Katiba (ya CUF) ni kuandaa ajenda kwa ajili ya kikao cha Baraza Kuu litakaloanza kesho (leo) na baada ya hapo tutatangaza msimamo wetu juu ya uchaguzi huo,” kilieleza chanzo hicho.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa CUF, Silas Bwire, Kamati ya Utendaji ilikuwa na wajumbe 18 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambao ni viongozi waandamizi wa chama.
Baraza kuu ambalo linatarajia kufanya kikao chake leo, litakalopokea ajenda zilizojadiliwa jana, lina wajumbe 60.
Kikao cha Baraza ambacho kitaongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Twaha Tasilima, kitajadili kwa kina ajenda zitakazowasilishwa pamoja na kuzitolea uamuzi.
HALI ILIVYOKUWA CUF
Nipashe jana lilifika katika ofisi hizo za makao makuu ya CUF, zilizoko Buguruni saa tano asubuhi na kukuta ulinzi ukiwa umeimarishwa wakati kikao kikiendelea.
Maofisa wa usalama wa chama hicho walionekana wakiwa nje ya geti la kuingilia katika ofisi za chama, karibu na mlango wa ukumbi wa mkutano na maeneo yote ya ofisi hizo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, eneo ambako magari yanaegeshwa siku zote yalizuiwa kuegeshwa kwa madai ya kuimarisha ulinzi kutokana na uwepo wa Maalim Seif, ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Wiki iliyopita, ZEC ilitangaza tarehe ya kurudiwa kwa uchaguzi uliofutwa Oktoba 28 mwaka jana kuwa utarudiwa Machi 20 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salum Jecha, alisema uchaguzi huo utawahusisha wagombea wa nafasi za urais, uwakilishi na udiwani na kwamba hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wala mikutano ya kampeni.
VIGOGO WAGAWANYIKA ZANZIBAR
Wakati hatima ya CUF kushiriki au kutoshiriki uchaguzi wa marudio inatarajia kufahamika leo, mgawanyiko mkubwa umeibuka miongoni mwa wajumbe wake wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa.
Katika mgawanyiko huo, wamo wanaopinga kushiriki huku wengine wakitaka chama kuangalia upya msimamo wa kususia uchaguzi huo.
Wakizungumza Nipashe kwa mashariti ya kutotajwa majina, baadhi ya wajumbe hao kutoka Pemba walisema msimamo wa kususia uchaguzi una manufaa na hasara kubwa kwa chama na unaweza kuleta mgawanyiko kwa viongozi na wagombea katika majimbo ya uchaguzi.
Mjumbe mmoja alisema iwapo chama kitaamua kushiriki uchaguzi huo, kitakuwa kimejimaliza kisiasa pamoja na kutokuaminika tena na jumuiya ya kimataifa hasa nchiu na taasisi zilizotoa ripoti kuwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka jana ulikuwa huru na wa haki.
Aidha, alisema kitendo kilichofanywa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salum Jecha, cha kufuta matokeo baada ya kuona CCM wako katika mwelekeo mgumu wa kuanguka katika uchaguzi, utakuwa mchezo wa kudumu wakati hauna manufaa katika kuimarisha demokrasia Zanzibar.
Alisema hata wananchi wenyewe msimamo wao wanataka kuona ZEC inakamilisha uchaguzi huo uliofutwa kwa kumtangaza mshindi wa urais katika uchaguzi huo pamoja na matokeo ya wawakilishi na madiwani
Alisema kuwa haiwezekani uchaguzi kurudiwa na kusimamiwa na tume ambayo imepoteza imani kwa wananchi wake na kwamba uchaguzi huo umelenga kuhakikisha CCM inashinda, ndiyo maana wapinzani wanazuiwa kufanya harakati za kisiasa tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo.
Hata hivyo, mjumbe mmoja akiwa na wezake watatu katika mazungumzo na mwandishi wa habari hii, alisema hatua ya kususia uchaguzi italeta madhara makubwa kwa maendeleo ya demokrasia na utakuwa mwanzo wa kufa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema Wawakilishi wengi wametumia gharama kubwa katika majimbo yao na hatua ya kususia uchaguzi inaweza kuleta mgawanyiko mkubwa pamoja na chama kuwa katika wakati mgumu wa kujiendesha kutokana na kutegemea ruzuku na michago ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, wagombea wengi wa uwakilishi hawakubaliani na msimamo wa kususia uchaguzi lakini wanashindwa kujitokeza na kuzungumza hadharani.
Alisema chama kilitakiwa kungalia umuhimu wa kuwa na tume huru ya kusimamia uchaguzi pamoja na jumuiya ya kimataifa kupewa nafasi ya kusimamia kwa karibu uchaguzi wa marudio badala ya kususia.
Mjumbe huyo alisema pamoja na kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa bado imesaidia katika kuimarisha amani na kuondoa chuki na uhasama wa kisiasa na kwamba hatua ya CUF kujiondoa katika serikali kunaweza kuleta matatizo makubwa kutokana na kuwa na uwakilishi wananchi wengi sawa na CCM.
JUSSA ANENA
Akizungumzia mgawanyiko huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema kutokana na ukubwa na uzito wa mgogoro wa uchaguzi, mgawanyiko ni jambo ambalo halikwepeki kwa chama kikubwa kama hicho.
Alisema uongozi wa chama uko makini katika kujadili ajenda ya mgogoro wa uchaguzi na kuwataka viongozi na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa na moyo wa subira wakati Baraza Kuu la Uongozi la Chama linajiandaa kutoa kauli ya mwisho juu ya hatima ya uchaguzi huo.
Jussa alisema uamuzi utakaotolewa na Baraza Kuu ndio utakuwa mwongozo kwa wagombea wote wa chama pamoja na wanachama na watu wanaokiunga mkono chama.
Alisema mchezo aliyoufanya Jecha wa kufuta matokeo ya uchaguzi kwa manufaa ya CCM, haukubaliki katika misingi ya demokrasia na utawala bora.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment