
Dodoma. Wakati sakata la Kampuni ya Lugumi kudaiwa kushindwa kutekeleza mradi wa utambuzi wa vidole kwenye vituo vya polisi likipamba moto, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amesema hana uhusiano wowote na kampuni hiyo kama watu wanavyodai.
Kitwanga ambaye alihusishwa na Lugumi kupitia kampuni ya Infosys iliyodaiwa kwamba kiongozi huyo ni mmoja wa wanahisa wakati akiwa mfanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ameeleza kuwa hahusiki na wala halijui suala la Lugumi.
Infosys ambayo imekanusha kuhusika katika sakata hilo imedaiwa kuwa iliisaidia kampuni ya Lugumi kupata vifaa kutoka kampuni ya Dell ya Marekani ili viweze kufungwa kwenye vituo vya polisi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kitwanga alisema anashangazwa jinsi anavyohusishwa kwa maelezo kuwa wakati tukio hilo likitokea mwaka 2011, yeye hakuwa waziri wa wizara hiyo.
“Inanishangaza sana sihusiki na wala silijui hili suala la Lugumi. Wakati linatokea sikua waziri wa wizara hii ndiyo maana huwa sipendi na wala sitaki kuzungumza chochote kuhusu Lugumi,” alisema.
Kitwanga alifafanua kuwa baadhi ya mambo yameanza kubainika baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, licha ya kutotaka kuweka wazi kama suala la Lugumi ni miongoni mwa mambo hayo.
Wakati Kitwanga akieleza hayo Spika wa Bunge, Job Ndugai ameeleza jana kuwa mpaka sasa hajapata mkataba wa kampuni hiyo ikiwa ni takribani wiki moja tangu Bunge kueleza kuwa halikuagiza mkataba huo, bali “Maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo.”
Kampuni ya Lugumi ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati ya 106 zilizotakiwa kufungwa, licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.
Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo.
Utekelezwaji wa mkataba huyo uliwasilishwa jana kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na mwenyekiti wake Aeshi Hilaly alisema wameanza kuupitia na watakapokamilisha wataweka kila kitu wazi. Awali kamati hiyo ilitaka nguvu itumike ili Jeshi la Polisi liwasilishe mkataba huo ambao imeshindwa kuutoa kwa zaidi ya mara mbili, lakini uliwasilishwa jana na wizara husika.
Kwa upande wake Ndugai alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema, “Mimi sijapata taarifa zozote za Lugumi. Jambo hilo bado lipo katika kamati ya bunge.”
Jana Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hillaly alimweleza mwandishi wetu kuwa kamati hiyo ilikutana kwa ajili ya kujadili suala hilo, huku akisisitiza kuwa atakutana na wanahabari kueleza kinachoendelea.
No comments:
Post a Comment