Wednesday, June 8, 2016

NAIBU SPIKA DK. TULIA ACKSON ATANGAZA KUKATWA POSHO WABUNGE WA UPINZANI WANAOSUSIA BUNGE

 Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson akitangaza bungeni jDodoma jioni kwamba wabunge wa upinzani waliokuwa wakitoka bungeni posho zao zitakatwa kwa siku zote walizotoka.  Uamuzi huo uliotokana na muongozo uliotolewa na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy, umeshangiliwa sana na wabunge wa chama tawala.


Hatimaye Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson ametoa maamuzi kuhusu hoja ya wabunge kulipwa posho au kutolipwa wanapoingia Bungeni na baadae kutoka nje kwa shughuli zisizo za Kibunge.

Akisoma muongozo wake muda mfupi kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge jioni hii baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango kusoma Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, Dk. Tulia alisema kuwa wabunge wanaofanya vitendo hivyo hawatalipwa posho.

Alitoa uamuzi huo baada ya kurejea kanuni za Bunge akitumia kanuni ya tano fasili ya kwanza ya toleo la mwaka 2006 na maamuzi yaliyowahi kufanywa na Spika waliotangulia katika hali kama hiyo.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy (CCM), ambaye alitoa muongozo bungeni akitaka wabunge wa upinzani waliokuwa wakitoka nje kila mara wakatwe posho kwani wanalipwa bila kufanya kazi hivyo kuliingizia taifa hasara.


“Hivyo basi, kwakuwa jambo hili halikubaliki, na kwakuwa miongozo kadhaa imeshatolewa kuwasihi waheshimiwa Wabunge wasitoke nje ya ukumbi wa Bunge kwa shughuli zisizo rasmi. 

"Naagiza kwamba wabunge wote wanaojisajili kisha kutoka ukumbini kwa kususia vikao vya Bunge, hawatastahili kulipwa Posho kwa siku zote ambao wamekuwa wakijisajili kuingia ukumbini na kisha kutoka ukumbini,” alisema Naibu Spika.

Wabunge wa Upinzani wamekuwa wakitoka nje ya Bunge muda mfupi baada ya kuingia Bungeni katika vikao vyote vinavyoongozwa na Naibu Spika kwa madai kuwa hawana imani naye kwakuwa amekuwa akiongoza Bunge kwa ubabe na kuwapendelea wabunge wa CCM.

No comments: