Advertisements

Tuesday, August 23, 2016

Lowassa Apigilia Msumari wa Oparesheni UKUTA ya Sept. 1


JANA Agosti 22, 2016, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Nne, Edward Ngoyai Lowassa alifanya ziara mkoani Mbeya na kuzungumza na wanachama wa Chadema mkoani humo huku akisisitiza suala la maandamamo nchi nzima ambalo chama hicho limeipa jina la Oparesheni UKUTA waliyopanga kuitekeleza Septemba Mosi mwaka huu.

Lowassa alisema haya;

Leo nimezunguka katika majimbo ya Mbeya Vijijini, Vwawa na Tunduma nikiwaeleza kuhusu Operation UKUTA, UKUTA si fujo, UKUTA si machafuko na hatuna haja ya kufanya fujo , tunapiga kelele dhidi ya uvunjwaji wa haki ya kidemokrasia na katiba ya nchi unaofanywa na utawala huu wa awamu ya tano .

CHADEMA ni nani wakapambane na polisi ,polisi ambao ni watoto wetu ,ndugu zetu na hata wake na waume zetu ila tuwahakikishie hatutorudi nyuma pale katiba na haki ya kidemokrasia ikichezewa au kuwa chini ya mtu fulani .

Najua polisi watapiga watu ,wataumiza watu na hata kuua ila niwahakikishie wao na walio na mamlaka wataishia katika mahakama ya Kimataifa .

Siasa ni mazungumzo ,lazima tuzungumze milango yetu iko wazi kufanya mazungumzo ila kwa kuwa hawahitaji na sisi hatutorudi nyuma September Mosi ,tumejiandaa vya kutosha na sasa tuko ngazi ya kaya na wajumbe wetu wanakamilisha kazi katika kaya ili tarehe mosi sauti ya kutosha ipazwe kwa maandamano na mikutano kama tulivyokubaliana katika kata zetu na majimbo nchi nzima .


Haiwezekani hata kidogo mtu mmoja azuie kila kitu ,nchi hii ni mali yetu sote na inaongozwa na Katiba na sheria. Kamati kuu ilipoamua katika suala la UKUTA haikukurupuka , kamati kuu yetu inaundwa na mchanganyiko wa wasomi wa kada mbalimbali ,wazee wenye busara na vijana machachari kamwe hawawezi kukukurupuka na UKUTA ni haki ya watanzania wote.

Pili naomba niwape siri ya ushindi 2020 ndugu zangu na wanachama wenzangu , tutashinda uchaguzi Mkuu 2020 kama tutafanya yafuatayo na kuyasimamia
Kwanza; Umoja ndani ya Chama na wanachama ,tuheshimiane ,tusameheane na tuimarishe chama chetu “chama ndani ya Chama , chama nje ya chama na chama ndani ya Umma “- LOWASSA.

Haya yanakuja wakati Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi likiwa limepiga marufuku maandamano nchini na kuahidi kuwashughulikia ipasavyo wale wote watakao kaidi amri hiyo.

GPL

No comments: