Vielelezo vya shamba hilo vinaonesha kuwa ni mali ya Shule ya Msingi Samunge iliyoko Loliondo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alitoa amri kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka na viongozi wengine wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, kuhakikisha wanamtoa mfanyabiashara huyo ili shule iendelee na mipango yake katika shamba hilo.
Akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Amani Kasone alisema Leminde amegoma kuondoka na anapata huduma zote za maji kutoka kwa viongozi wa Mamlaka ya Maji wa Kata ya Samunge.
Kasone alisema pamoja na jitihada zake za kutoa taarifa kwa viongozi wa vitongoji, kijiji na kata, hakuna jitihada zozote zinazochukuliwa za kumwondoa mfanyabiashara huyo, licha ya Mkuu wa Mkoa, Gambo, kuagiza aondolewe.
Alisema binafsi ameshindwa kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa serikali waliopo karibu. Alisema mfanyabiashara huyo amekuwa akiwatishia walimu kwa panga na mshale, wakifuatilia kuondoka katika shamba hilo.
Mkuu wa wilaya, Taka akizungumza katika eneo la shamba hilo alipotembelea na kuona mazao yaliyolimwa katika shamba hilo na mfanyabishara huyo, alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na uvamizi wa namna hiyo haukubaliki kamwe.
Taka alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ngorongoro, kumsaka na kumtia ndani mfanyabiashara huyo kwa kukaidi agizo la mkuu wa mkoa, lililomtaka kuondoka katika shamba hilo.
Gambo alipokuwa katika ziara ya kikazi katika wilaya hiyo, kuangalia shughuli za maendeleo, moja ya malalamiko aliyoyakuta ni walimu, wanafunzi na wananchi wa kata hiyo ya Samunge, kumlalamikia kuwa Leminde kuwa amepora eneo la shule na walimwomba kutatua tatizo hilo.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment