Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (mbele), akitoka kuangalia ukarabati wa meli ya Mv. Clarius, katika Bandari ya Mwanza, leo. Meli hiyo inatoa huduma katika visiwa vilivyo kwenye ziwa Victoria.
Muonekano wa Meli ya Mv. Umoja yenye uwezo wa kubeba behewa 22. Meli hiyo inasafirisha mizigo kutoka Bandari ya Mwanza kuelekea Bandari ya “Port Bell” Uganda.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (Wa nne kulia), akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Xavier Kapinga, alipofika Bandari ya Mwanza leo kujionea maendeleo ya ukarabati wa meli ya MV. Clarias katika Bandari hiyo.
Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Xavier Kapinga, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (Wa tatu kushoto mbele) wakati alipokagua maendeleo ya ukarabati wa meli katika Bandari ya Mwanza, leo.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Erick Hamissi, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (Wa pili kulia), hatua zilizofikiwa za ukarabati wa meli ya Mv. Clarius na Mv. Umoja katika Bandari ya Mwanza.
Mafundi wakiendelea na ukarabati wa meli ya Mv. Clarius leo katika Bandari ya Mwanza. Kukamilika kwa ukarabati wa Meli hiyo inayotoa huduma katika visiwa vilivyo katika ziwa Victoria kutarudisha huduma za usafirishaji na abiria katika visiwa hivyo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amekagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya na yakisasa itakayotoa huduma za usafirishaji katika Ziwa Victoria.
Akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Profesa Mbarawa, amewataka wafanyakazi wa Kampuni hiyo kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi ili kazi hiyo ianze mara moja na kukamilika kwa wakati.
“Mkandarasi ameshapatikana hivyo hakikisheni mnatoa ushirikiano na mnafanya uhakiki wa kimahesabu vizuri ili kazi hii ifanyike kwa gharama nafuu, ubora na muda mfupi”, amesema Profesa Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa, amekagua maendeleo ya ukarabati wa meli ya Mv. Clarias na Mv. Umoja ambapo ameeleza kuridhishwa kwake na hatua zilizofikiwa, na hivyo kuwataka MSCL kutafuta mizigo ya kusafirisha kutoka Bandari ya Mwanza kwenda Bandari ya “Port Bell”, nchini Uganda.
“Kukamilika kwa meli kuwiane na kasi ya kutafuta mzigo mwingi ili meli hizi zifanye biashara wakati wote na kuhakikisha Kampuni yenu inapata mapato mengi yatakayowawezesha kujiendesha kwa faida”, amesisitiza Waziri Mbarawa
Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Erick Hamissi, amemhakikishia Profesa Mbarawa, kuwa wamejipanga kufanya ukarabati mkubwa wa meli za Mv. Victoria, Butiama na Liemba ili kuziwezesha meli hizo kufanya kazi katika ubora wake wa awali na kupunguza tatizo la usafiri katika ziwa Victoria na Tanganyika.
“Tumeweka mkakati wa kuhakikisha tunazikarabati meli zetu zote ili ziwe katika ubora unaostahili wakati wote”, amefafanua Bw. Hamissi.
Katika kuhakikisha maendeleo ya kibiashara na kuichumi yanafikiwa katika Ukanda wa maziwa makuu nchini, Serikali imejipanga kuhakikisha inafufua usafiri wa meli za abiri na mizigo katika ukanda huo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment