Advertisements

Wednesday, December 27, 2017

Meya wa Moshi akanusha kuhamia CCM


Meya wa Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, Raymond Mboya amekanusha tetesi za kujivua wadhifa wake huo na kuhama chake cha Chadema na kuhamia CCM.
Mboya ambaye ni diwani wa Kata ya Longuo ametajwa kwamba ana lengo la kukihama chama hicho, lakini amekanusha na kusema kuhama chama na kuacha kazi sio kuunga mkono Serikali bali ni kuchezea rasilimali za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 27 ofisini kwake jana alisema, taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kutaka kuhama chama sio za kweli na wananchi wapuuze.
“Kila mmoja anaunga mkono Serikali lakini sio kwa kuacha kazi na kumuunga mkono mtu anayefanya kazi” amesema Mboya.
Amesema wanaofanya hivyo hawazitendei haki kazi ambazo wamepewa na wananchi hivyo wanatakiwa kuunga mkono kazi za Serikali kwa kufanya kazi ili kuleta maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Amesema “ tumechaguliwa na wananchi ili tuwatumikie na sio wametuchagua ili tuharibu rasilimali”
Hata hivyo alisema katika kuunga mkono sera ya viwanda, manispaa hiyo inatarajia kuanzisha kiwanda kidogo cha mbolea inayotokana na takataka zinazolalishwa na wakazi wake.
Amesema kiwanda hicho ambacho kitaanzishwa kwa kushirikiana na serikali ya Ujerumani kitajengwa katika eneo la dampo kuu la takataka ambalo liko Kaloleni.
Amesema zaidi ya tani laki mbili za takataka huzalishwa kila siku na katika upembuzi wa awali takataka hizo zinatosha kuanzisha kiwanda hicho.

Chanzo: Mwananchi

No comments: