ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 8, 2019

Bosi TBS awasimamisha kazi watumishi wawili kituo cha Namanga

By Happy Lazaro, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Arusha. Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Yusuph Ngenya amewasimamisha kazi watumishi wawili wa shirika hilo wa kituo cha mpaka wa Namanga kwa tuhuma za kuruhusu uingizwaji wa mifuko mbadala isiyokidhi viwango.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Jumatano Agosti 7, 2019, Dk Ngenya amewataja watumishi hao kuwa ni msimamizi wa kituo hicho kilichopo mpakani wa Tanzania na Kenya, Emmanuel Kiwango na mwenzake, Jenifa Jackson.

Amesema kuwa mzigo wa mifuko hiyo mbadala ulikamatwa Agosti 5, 2019 baada ya kupitishwa na wasimamizi wa shirika hilo kituoni hapo wakati wakijua kuwa haikidhi viwango.

Dk Ngenya amesema kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya wananchi kutoka Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro kutokana na kuwepo kwa utitiri wa mifuko hiyo mbadala isiyokidhi viwango.

“Nimeamua kuwasimamisha kazi watumishi hawa wakati uchunguzi ukiendelea kufanyika. Inaonekana kama wameweza kupitisha mifuko hiyo wakati wakijua kuwa haikidhi viwango, ni jambo ambalo wamezoea kufanya hata kwa bidhaa nyingine,” amesema.

Amebainisha kuwa TBS haiwezi kuvumilia watu wa namna hiyo, kwamba hayupo tayari kufanya kazi na watumishi wa aina hiyo.

No comments: