ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 10, 2019

Watu zaidi ya 57 wafariki dunia baada ya lori la mafuta kulipuka Morogoro

Image result for watu wafariki morogoro
Image may contain: one or more people, fire and outdoor
By Lilian Lucas, Mwananchi llucas@mwananchi.co.tz

Morogoro. “Inasikitisha”. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya lori la mafuta ya petroli kupinduka eneo la Msamvu mkoani Morogoro na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta hayo.

Tukio hilo limetokea leo Jumamosi Agosti 10, 2019 ambapo Mwananchi limefika eneo hilo na kushuhudia miili iliyoungua ikiwa imelazwa pembeni ya barabara ya Dar es Salaam-Morogoro wengi wakiwa ni madereva bodaboda na mamalishe wanaofanya shughuli zao hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema karibu watu 57 wamepoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea saa mbili asubuhi.

Ajali hiyo imetokea umbali wa mita 200 kutoka kituo kikuu cha mabasi Msamvu ukitokea Dar es Salaam.

Baadhi ya mashuhuda wamelieleza Mwananchi kuwa baada ya lori hilo kupinduka, watu walianza kuchota mafuta hayo.


Wamesema mmoja wa waliokuwa wakichota mafuta hayo alikuwa akivuta sigara, kwamba ndio chanzo cha mlipuko huo.

Abdallah Msambali amesema aliwaona waendesha bodaboda wakigombania kuchota mafuta kwa kutumia vyombo mbalimbali.

Miili ya waliofariki dunia inaondolewa eneo hilo na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi na Zimamoto na baadhi kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza eneo la tukio Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amesema Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lipo eneo la tukio huku magari ya kuzima moto zaidi ya manne yakiwa eneo la tukio.

“Haijawahi kutokea maafa makubwa namna hivi Morogoro, lori lilikuwa limepakia mafuta ya petroli lilianguka pembeni mwa barabara hapa Msamvu na kuanza kuvuja mafuta ambayo yalisambaa umbali wa mita 100,” amesema Kebwe.

“Baada ya moto kudhibitiwa tutaangalia maiti nyingine zitakazokuwa zimebanwa na lori la mafuta. Madaktari wote waliopo Manispaa ya Morogoro tumeshawapanga hospitali ya Mkoa kutoa huduma kwa majeruhi, wagonjwa wenye nafuu tutawahamishia wodi nyingine kupisha hii dharura,” amesema Dk Kebwe.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

No comments: