ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 9, 2019

WANANCHI WAMLILIA LUKUVI WAPATIWE SHAMBA LA MWEKEZAJI KILOSA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale wakati akitoka eneo la Kiwanda cha Mwekezaji Farm Africa Agro Focus Ltd Kilosa Morogoro jana. Kulia kwa Lukuvi ni Mkuu wa wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa kijiji cha Magomeni wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro (hawapo pichani) jana alipokwenda kusikiliza malalamiko ya wakazi wa kijiji hicho kuhusiana na shamba la Mwekezaji Farm Africa Agro Focus Ltd. Kushoto ni ya Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi.

Na Munir Shemweta, WANMM KILOSA
Wananchi wa kijiji cha Magomeni kilichopo tarafa ya Kilosa Mjini wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro wametoa kilio chao kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi wakitaka kupatiwa shamba la Mwekezaji Farm Africa Agro Focus Ltd marufu kama kwa Karamagi kwa madai kuwa mwekezaji wa shamba hilo ameshindwa kuliendeleza.
Wananchi hao wamemueleza Lukuvi kuwa kijiji hicho hakina ardhi ya kutosha kuwawezesha wananch hao kujishughulisha na kilimo na eneo kubwa katika kijiji hicho ni eneo la shamba la Farm lenye ukubwa wa ekari 13,000.
Wananchi hao wa kijiji cha Magomeni walitoa kilio chao kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi jana tarehe 08 Novemba 2019 wakati Lukuvi akiwa katika ziara yake wilayani Kilosa kuendelea na jitihada za kutatua migogoro ya ardhi katika mkoa wa Morogoro.
Wamedai kuwa pamoja na Muwekezaji kuwa na eneo kubwa lakini ameshindwa kuliendeleza kama taratibu zinavyotakiwa na badala yake sehemu kubwa ya shamba hilo imebakia kuwa pori ingawa limeendelezwa katika eneo la usoni.
Mmoja wa wananchi hao Ismail Masudi alimueleza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa kwa muda mrefu wananchi wa kijiji cha magomeni wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa kutokana na mgogoro wa muda mrefu kati ya muwekezaji na wananchi wa kijiji hicho.
‘’Wananchi tumepiga kelele sana ya kusaidiwa, Mwekezaji ana eneo kubwa lakini wananchi wanakosa maeneo ya makazi na ya kufanyia shughuli za kilimo huku sehemu kubwa ya shamba ka mwekezaji ikiwa ni pori’’ alisema Masudi
Mwananchi mwingine Hatibu Musa alisema kilio kikubwa cha wakazi wa kijiji cha Magomeni ni eneo la kulimia wakati idadi ya wakazi inaongezeka na wananchi wamehangaika kwa takriban miaka 5 na mgogoro huku wakidai mwekezaji hana tija.
Kwa upande wake Wzairi wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi kumuomba mwekezaji wa shamba hilo kupunguza ekari 3000 kati ya 10,000 alizokuwa nazo kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa kijiji cha Magomeni.
‘’ Badala ya kuanza kufuta shamba, Mwekezaji arudishe ekari 3000 kati ya 13,000 alizokuwa nazo tunataka kasi ya uendelezaji uendelee maana haiwezekani miaka nanne ni ekari 2000 tu zilizoendelezwa’’ alisema Lukuvi
Alisema, haingilii maamuzi ya mahakama yaliyompa ushindi Mwekezaji na wala hataki wananchi kupingana na maamuzi ya mahakama bali hali hiyo inafuatia mwekezaji kushndwa kuliendeleza shamba kama taratibu zinavyotakiwa ambapo uendelezwaji unatakiwa kufanyika moja ya nane kila mwaka jambo alilolieleza muwekezaji huyo alishindwa kutekeleza.
Taarifa kuhusiana na shamba hilo zinaeleza kuwa Mwekezaji wa sasa Farm Africa Agro Focus alikabidhiwa shamba mwaka 2013 na hadi kufikia sasa ni ekari 2000 pekee kati ya 13,000 ndizo zilizoendelezwa kwa kulima zao la Korosho.

No comments: