Kaimu Mkurugenzi Mtendaji MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele akielezea utendaji wa mabwawa ya majitaka ya Butuja kwa Ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW)
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (kulia) akifafanua jambo wakati wa ziara kwenye mradi wa uondoshaji majitaka Mabatini

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (kulia) na Ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) walipotembelea mradi wa uondoshaji majitaka maeneo ya milimani.
Meneja anayesimamia miradi Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika kutoka Benki ya KfW, Martina Maurer (kushoto) akimsikiliza Meneja Ufundi wa MWAUWASA, Mhandisi Salim Lossindilo (kulia) wakati wa ziara kwenye maeneo yatakayonufaika na mradi.
Muonekano wa Mabwawa ya Majitaka ya Butuja Mkoani Mwanza
Na Mohamed Saif- Mwanza
Mamlaka
ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kupitia Kamisheni
ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) inatarajia kutekeleza ujenzi wa mradi
wa miundombinu ya majitaka na usafi wa mazingira wenye thamani ya Euro
Milioni 5.3 kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa Ziwa Victoria.
Mradi
huo unafadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Serikali ya
Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya KfW na Umoja wa Ulaya (EU)
chini ya uratibu wa LVBC kupitia programu ya Pamoja ya Usimamizi na
Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Ziwa Victoria
(LVB-IWRM).
Hayo
yalibainika hivi karibuni Jijini Mwanza katika kikao kilichoshirikisha
wadau kutoka MWAUWASA, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria na ujumbe
kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) ukiongozwa na Meneja
anayesimamia miradi Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, Martina Maurer.
Akizungumza
katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi
Leonard Msenyele alisema ufadhili huo uliweka vipaumbele mbalimbali
vyenye nia ya uhifadhi wa mazingira kwa miji inayozunguka Ziwa Victoria
kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Mradi
utawezesha ukarabati na upanuzi wa mtandao wa majitaka kwa takriban
kilomita 14.4 sambamba na kuunganisha kaya 1,600, uboreshaji vituo vya
kusukuma majitaka na ununuzi wa vifaa vya usimamizi wa Mfumo wa Majitaka
yakiwemo magari ya kuondoa taka majumbani,” alibainisha Mhandisi
Msenyele.
Mhandisi
Msenyele alisema ufadhili huo unafuatia ushirikiano madhubuti baina ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaayoongozwa na Mhe. Samia
Suluhu Hassan na mataifa ya nje. "Wengi ni mashahidi, mnaona namna
ambavyo Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan anavyoweka msisitizo
kwenye suala la ushirikiano wa kimataifa," alisema Mhandisi Msenyele
Alisema
kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa makubwa kwenye utunzaji wa
Mazingira hususan kupunguza uchafuzi wa Ziwa Victoria. "Mradi huu
utasaidia kuwaondolea adha wananchi ya kujaa mara kwa mara kwa mashimo
ya vyoo na hii itapunguza uchavuzi wa Ziwa letu," alisema Mhandisi
Msenyele.
Kwa
upande wake kiongozi wa ujumbe huo ambaye pia ni Meneja wa Benki ya KfW
upande wa Afrika, Martina Maurer alisema mradi umelenga kupunguza
uchafuzi wa Ziwa Victoria hususan unaotokana na utiririshaji ovyo wa
majitaka.
Akielezea
kuhusiana na ziara yao hiyo ya siku moja Mkoani Mwanza, Maurer alisema
imelenga kujionea eneo la mradi na kujadili namna bora ya utekelezwaji
wake.
"Tunatarajia
kujifunza mengi kuhusu namna mnavyotekeleza miradi yenu hususan ya
utunzaji wa mazingira (uondoshaji wa majitaka) sambamba na kujadili
changamoto zinazowakabili kwenye utekelezaji wa miradi kwa ufumbuzi wa
pamoja na pia kubaini maeneo zaidi tunayoweza kushirikiana," alisema
Maurer.
Akizungumzia
utekelezaji wa mradi, Kaimu Meneja Ufundi wa MWAUWASA, Mhandisi Salim
Lossindilo alitaja maeneo yatakayonufaika na mradi huo kuwa ni Igogo,
Kirumba, Mwaloni, Nyamanoro, Kitangiri na Pasiansi.
Mhandisi
Lossindilo vilevile alitaja maeneo kadhaa ya ushirikiano ikiwemo
upanuzi wa miundombinu ya majitaka kwenye eneo linalozungukwa na Mto
Mirongo ambapo alisema wanatarajia kuunganisha wananchi wapatao 100,000
na mfumo wa majitaka ili kupunguza uchafuzi wa mto huo.
"Tumeandaa
maandiko matano ya miradi itakayonufaisha Wilaya za Ilemela na
Nyamagana yenye lengo la kutunza Ziwa Victoria na inashirikisha
Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela, Bodi ya Bonde la
Ziwa Victoria pamoja na MWAUWASA,” alibainisha Mhandisi Lossindilo
Ujumbe
huo ulipata fursa ya kutembelea maeneo yatakayonufaika na mradi huo wa
Uwekezaji wa Kipaumbele cha Juu (HPI-areas), mabwawa ya majitaka ya
Butuja na mradi rahisi wa uondoshaji majitaka maeneo ya milimani
(Simplified Sewerage System).
Kwa
nyakati tofauti ujumbe huo uliipongeza MWAUWASA kwa hatua mbalimbali
inazochukua katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na hususan wa
maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.




No comments:
Post a Comment