ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 4, 2026

MCHECHU: HAKUNA UCHUMI BILA UHIFADHI


Na. Edmund Salaho/Ruaha 


Msajili wa Hazina ambaye pia ni mlezi wa Great Ruaha Marathon na mwakilishi wa Mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba katika mbio hizo Bw. Nehemiah Mchechu amebainisha kuwa uchumi wa Taifa unategemea uhifadhi huku akiongeza kuwa Mto Ruaha Mkuu ni moja ya mito muhimu zaidi nchini unaotoa uhai kwa Hifadhi ya Taifa Ruaha, unaosaidia wananchi katika shughuli za kilimo na mifugo, ikiwa ni pamoja na kuwewezesha uzalishaji wa umeme na kuchangia ustawi wa wananchi nchini.

Mchechu, ameyasema hayo leo Julai 04, 2026 wakati akizindua mbio za kimataifa zinazofanyika katika Hifadhi ya Taifa Ruaha maarufu kama "Great Ruaha Marathon".

Aidha, Mchechu ametoa rai kwa Watanzania kujijengea tabia ya kutembelea Hifadhi za Taifa, kujivunia utanzania na kuwa mabalozi wa nchi yao.

"Tunataka Watanzania wengi zaidi watembelee hifadhi zetu, wajivunie urithi tulionao na wawe mabalozi wa utalii wa nchi yao” alieleza Mchechu.





Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Gibril Mwishawa amebainisha kuwa utalii wa michezo umekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje na kuelezea kuwa TANAPA imeweka mikakati madhubuti katika zao hilo jipya la utalii.

"Duniani kote, matukio makubwa ya michezo hutumiwa kuongeza idadi ya watalii, kuvutia wawekezaji, kukuza biashara na kuijenga taswira ya nchi kimataifa, TANAPA tumejidhatiti vilivyo kuhakikisha tunavutia watalii wengi kupitia zao hili la utalii wa michezo"

Mratibu wa Great Ruaha Marathon Bw. Hamim Kilahama amesema  "Great Ruaha Marathon si mashindano ya riadha pekee. Ni jukwaa la kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kulinda mazingira, kuhifadhi vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkuu, kuendeleza utalii wa Kusini mwa Tanzania. Tunatumia michezo kama chombo cha kuleta mabadiliko chanya katika jamii, ikiwa ni mara ya tano mfululizo Great Ruaha Marathon imefungua ukurasa mpya wakuitangaza Ruaha kupitia utalii wa michezo".

Hifadhi ya Taifa Ruaha ni moja kati ya Hifadhi kubwa barani Afrika. Ni hazina ya kipekee yenye idadi kubwa ya wanyama kama tembo, simba, chui, mbwa mwitu wa porini, twiga, nyati na mamia ya aina za ndege wanaovutia watalii kutoka kila pembe ya dunia.




















No comments: