ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 10, 2012

JK awakuna madaktari

BAADA ya mgomo uliodumu kwa siku tatu kuanzia Jumatano iliyopita, hatimaye madaktari 
wameridhia kurejea kazini mara moja baada ya kuwa na imani ya kutekelezwa kwa madai yao na Rais Jakaya Kikwete. 

Wakati madaktari wakifikia uamuzi huo, mapema jana Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) nalo liliibuka na kutoa tamko la kuwataka kurejea kazini. 

Akizungumza mara baada ya mkutano wa madaktari uliofanyika Don Bosco, jijini Dar es Salaam kwa takribani saa tatu, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Namala Mkopi alisema uamuzi huo umefikiwa na wanachama wao baada ya kupewa mrejesho wa kile 
walichozungumza na Rais.
 

Rais Kikwete juzi alikutana na viongozi wa madaktari Ikulu, ili kuzungumza nao kuhusiana na 
madai yao yaliyosababisha kuwapo kwa mgomo. 

“Jana (juzi) tulikutana na Rais (Jakaya Kikwete) kumweleza madai yetu, akatusikiliza na kutuahidi kuyatekeleza, kutokana na udhati aliouonesha katika kutatua matatizo yetu tumeamua kurejea kazini baada ya mkutano huu. 

“Hatukuwa tunashindana ili kumpata mshindi, lengo letu lilikuwa ni uboreshwaji wa utoaji 
huduma za afya kwa Watanzania. 

Tuna imani na Rais kuwa atayapatia ufumbuzi madai yetu. Tutakuwa tukitoa mrejesho kwa 
wanachama wetu kila hatua tutakayokuwa tumefikia,” alisema Mkopi, ikiwa ni siku moja tangu 
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi iwaamuru kurejea kazini. 

Ingawa hakuwa tayari kueleza kuwa kurejea kwao kazini kumechangiwa pia na amri ya Mahakama, Mkopi pia hakueleza kama wametoa sharti lolote kwa Rais au muda maalumu wa kushughulikia madai yao. 

Naye Katibu wa MAT, Rodrick Kabangira alisema pamoja na kurejea kazini bado hawana 
imani na viongozi wa juu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kuwa hawako tayari 
kufanya nao kazi. 

“Madaktari kwa pamoja tunaona kuwa mazingira ya kufanya kazi na wakuu wa Wizara 
hayatakuwa mazuri kwa sababu hatuna imani nao. Tunawatangaza kuwa ndio maadui 
wa Sekta ya Afya,” alisema. 

Kabangira alisema kuwa pia MAT imemfungia Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii. Dk. 
Lucy Nkya kuwa mwanachama wa chama hicho kwa miaka miwili kutokana na kukiuka 
maadili ya taaluma hiyo. 

Kabla ya kuanza upya kwa mgomo wa madaktari Jumatano iliyopita, awali kulikuwa na 
mgomo ambao ulisababisha Serikali kuwaondoa Katibu Mkuu, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa ambao walipewa likizo ya lazima, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizochangia madaktari hao kugoma. 

Kwa upande wa Waziri, Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Nkya ambao walidaiwa kuwa ndio kiini cha mgomo wa sasa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema watawajibishwa na Rais Kikwete wakati wowote. 

Serikali pia ilitangaza kukubali madai yote manane ya madaktari ambayo yaliwafanya wagome, ikiwa ni pamoja na madai ya kulipwa posho kwa madaktari walioko mafunzoni, posho ya kazi katika mazingira hatarishi, na posho ya kuitwa kazini baada ya saa za kazi, ambayo madaktari wanadai iongezwe kutoka Sh 10,000 walizokuwa wanalipwa. 

Hata hivyo, Serikali ilipandisha posho hizo hadi kufikia Sh 25,000 kwa madaktari bingwa, 
wasio bingwa Sh 20,000 na wenye Stashahada watalipwa Sh 15,000 na watumishi wa kada 
zingine Sh 10,000. 

Madai mengine ni posho ya usafiri, posho ya nyumba ambayo madaktari walitaka walipwe 
asilimia 30 ya mishahara yao, madai ya ongezeko la mishahara hadi Sh milioni 3.5 kwa mwezi, 
kuwa na bima ya afya ambayo walitaka madaktari wote wawe na kadi za kijani za Mfuko wa 
Bima ya Afya. 

Mpaka madaktari hao wanatoa uamuzi wa kusitisha mgomo jana mchana, hali ya huduma 
katika hospitali nyingi za umma nchini iliendelea kuripotiwa kuzorota, kama ilivyokuwa wakati 
mgomo umeshika hatamu. 

Wakati huo huo, Happy Elia, MIJO anaripoti kuwa Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholas Mgaya alisema jana kuwa kuna haja ya madaktari kurejea kazini baada ya Serikali kukubali 
kuzungumza nao. 

“TUCTA inakubaliana na madai ya madaktari kuhusu kuboreshwa kwa mazingira ya kazi 
na malipo bora. Maadamu Serikali imekubali kukaa nao na kueleza azma ya kutafuta suluhisho, 
basi waipe muda Serikali. 

“Tutapenda kuona madai yanayogusa uhai wa mtu kama vile mishahara kwa madaktari walio mazoezini yanashughulikiwa haraka, kama bado haijafanya hivyo TUCTA tunachelea kuunga mkono madai ya madaktari ya kuwataka mawaziri kujiuzulu au kumwagiza Rais kuwafukuza kazi,” alisema. 

Mgaya pia ameitaka Serikali kutafakari chanzo cha migogoro ya wafanyakazi ambayo 
imekuwa ikishamiri kila wakati.


Mwananchi

No comments: